Ndugu walia askari polisi kutoweka siku 41

Ndugu walia askari polisi kutoweka siku 41

Muktasari:

  • Ni takriban siku 41 sasa hakuna anayejua alipo Emmanuel Govela, ofisa wa polisi aliyekuwa mkuu wa Kituo cha Polisi cha Mji wa Kiserikali Mtumba.


Dodoma. Ni takriban siku 41 sasa hakuna anayejua alipo Emmanuel Govela, ofisa wa polisi aliyekuwa mkuu wa Kituo cha Polisi cha Mji wa Kiserikali Mtumba.

Si ndugu wala mwenye nyumba alikokuwa anapanga, ambaye anaweza kuelezea alipo ofisa huyo mwenye cheo cha ukaguzi (Inspekta), yaani nyota mbili, suala ambalo ndugu hao wameliacha kwa Jeshi la Polisi, wakiamini ndilo litakalofanikisha kupatikana kwake.

Govela (39) hajaonekana hadharani kwa zaidi ya siku 41, huku ndugu wakisema mawasiliano yake ya mwisho yalikuwa Juni 26, 2021 na katika kipindi hicho hayuko nyumbani kwake wala kituoni kwake.

Kilichoacha utata zaidi ni kuwa simu yake na vifaa vingine kama vitambulisho na waleti vilikutwa ndani ya chumba alimokuwa akiishi.

Govela alihamishiwa Dodoma mwishoni mwa mwaka jana na kupangiwa kazi katika Kituo cha Polisi cha Mtumba akitokea Babati mkoani Manyara.

Hadi jana hakukuwa na taarifa yoyote iliyotolewa na Jeshi la Polisi wala majibu yenye kuashiria mahali alipo askari huyo.

Maelezo ya ndugu

Mdogo wa askari huyo, Athuman Govela amelieleza Mwananchi ambalo limefuatilia suala hilo kwa takriban majuma mawili sasa kuwa waligundua kutoweka kwa ndugu yao baada ya kukosa mawasiliano naye kwa muda, hali ambayo haikuwa kawaida yake.

Alisema alipoanza kufuatilia kwa ndugu wengine, kila mmoja alionyesha kwamba hajawasiliana naye kwa muda.

“Mimi kwa mara ya mwisho niliwasiliana naye Juni 22, 2021 na pia mdogo wake mwingine anayesoma Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) alikuwa amemtafuta na kumkosa, ndipo nikamwambia mama, wakati huo mama naye alishampigia mara kadhaa hampati, ndipo mashaka yakaanza,” alisema.

Kwa mujibu wa Athuman, mdogo wao wa UDOM alikuwa amemuomba askari huyo fedha kwa ajili ya kulipia gharama za mahafali, naye akamuahidi kumpa mwishoni mwa mwezi wa Juni, lakini alipoona fedha hazijatumwa ndipo akaanza kumtafuta.

Alisema walipomkosa kwenye simu, Julai 22, 2021 walikwenda kwa mwajiri wake ambaye ni Jeshi la Polisi ambako walitoa taarifa.

Alisema Julai 23, 2021 waliongoza na maofisa wa polisi kwenda mahali alipokuwa anaishi ndugu yao na walikuta mlango umefungwa.

Baada ya kushauriana na mwenye nyumba, alisema waliuvunja mlango, na ndani ya nyumba walikuta simu, pochi ya fedha iliyokuwa na Sh70,000 na vitambulisho vyake vya kazi vyote vikiwa kitandani, jambo linalowapa hofu zaidi juu ya maisha ya ndugu yao.

Ndugu huyo alisema siku ya pili walirudi wakiwa na gari la polisi kwa ajili ya kuchukua vyombo vya ndugu yao lakini waliamua vibaki mikononi mwa polisi hadi watakapopata ufumbuzi kuhusu maisha yake.

“Kitendo kile kiliniumiza na kuustua moyo wangu, hata hivyo tunaendelea kumuachia Mungu kwani ndiye atakayegawa juu ya yote aliyoyafanya kaka yangu kwa kadri ya huruma yake,” anasema.

Athuman alisema hadi sasa hawana taarifa za wapi aliko ndugu yao na ugumu zaidi unaongezeka baada ya kuona tukio hilo linakuwa na usiri mkubwa na kuwa licha ya kutoonekana, hawakuwahi kuulizwa alipo hadi ndugu walipotoka kijijini kumtafuta.

“Sina maana kuwa tunawatuhumu polisi, lakini kinachotushangaza ni ule usiri mkubwa au kutojali uliokuwepo hadi tunakuja sisi kulalamika, jambo hili limetupa mshangao kidogo kujua kulikoni,” alisema Athuman.

Alisema yeye na mama yao walifika polisi na kuzungumza na mkuu wa polisi wa wilaya ambaye aliwapa matumaini kuwa ameongeza kikosi imara na wanatumia mitambo ya kiintelijensia kumsaka ofisa huyo na akawaomba wawe watulivu katika jambo hilo.

Alipotafutwa tena jana, Athuman alisema bado hawana taarifa za alipo kaka yao na kwamba familia haijakata tamaa kujua ukweli.

Mwenye nyumba hajui

Mmiliki wa nyumba aliyokuwa anapanga askari huyo, alisema “kwangu aliingia Januari 2, 2021 lakini siwezi kusimulia zaidi juu ya maisha yake kwa kuwa mimi siishi katika nyumba hiyo ila ina wapangaji tu, lakini taarifa za kupotea kwake ninazo hata mimi na kwa jinsi ilivyo kuna utata,” alisema Hassan Sumbi.

Sumbi alisema mwishoni mwa Juni alimtafuta Govela kupitia simu yake ya mkononi lakini hakumpata hewani na hata wakati mwingine alimpigia dalali aliyempeleka, pia naye hampati.

Alisema kabla ya hapo hakuwahi kusikia jambo lolote baya juu ya mpangaji huyo na wenzake, lakini pia hakujua kama alikuwa ni polisi hadi alipoitwa nyumbani kwake (baada ya kupotea) akawakuta polisi na ndugu watatu wa mpangaji huyo wakiomba ruhusa ya kuvunja mlango.

“Nilipofika waliniuliza kama kitasa changu wakivunja ni gharama gani nikawaambia ni 20,000, wakavunja. Wote tuliingia ndani na kuona simu na pochi ya pesa vikiwa juu ya kitanda, ndipo polisi waliondoka navyo pamoja na sare za jeshi, baadaye ndugu walikuja kuchukua vitu vyao. Kwa hiyo chumba changu kiko wazi kwa sasa,” alisema Sumbi.

Sumbi anasema nyumba awali ilikuwa ‘gesti’ kabla ya kuibadilisha matumizi, hivyo vyumba vyake ni vidogo na wapangaji wake wanakaa muda mfupi wakipata nyumba wanaondoka na kuwa Govela alikuwa kwenye harakati za kuhama.

Majibu ya polisi

Kwa wiki ya pili sasa Mwananchi limefanya jitihada za kuwasiliana na polisi kuhusu suala hilo bila mafanikio.

Awali, simu ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Onesmo Lyanga ilipokewa na mtu mwingine ambaye alisema ameachiwa ofisi, lakini yeye si msemaji katika jambo hilo na kuomba asubiriwe Kamanda atakaporejea ofisini.

Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu malalamiko ya ndugu kuhusu kutoweka kwa askari huyo na kwamba mwajiri wake ambaye ni Jeshi la Polisi amekaa kimya, alisema hakuna mtu ambaye amekaa kimya kwa jambo hilo na kuomba ndugu waulizwe vizuri, kwani huenda taarifa za kutoonekana kwa askari huyo zilitolewa na polisi.

Wiki hiyo, gazeti hili lilimpigia simu mara kadhaa Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, David Misime lakini simu yake iliita bila majibu.

Juzi Jumanne Agosti 3, 2021, gazeti hili lilimtafuta tena Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma, Onesmo Lyanga ambapo simu yake ilipokelewa na aliyejitambulisha kuwa msaidizi wake na alipoulizwa kuhusu suala hilo, aliuliza maswali kadhaa kisha akaahidi angepiga simu baada ya muda kidogo, lakini hakupiga na alipopigiwa tena simu haikupokewa.

“Ulisema una shida na RPC, unaitwa nani kutoka chombo gani, huyo polisi anaitwa nani kutoka kituo gani, taarifa mmepata wapi, basi nakupigia muda si mrefu,” alisema.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, Anthony Mtaka alipoulizwa kuhusu suala hilo, alisema hana taarifa za kupotea kwa askari huyo, lakini akashauri watafutwe polisi ambao wanaweza kulisemea zaidi.

“Hiyo taarifa ni ngeni kwangu, sijaipata bado lakini katika jambo hilo nadhani ukimpata Kamanda wa Polisi wa mkoa anaweza kuwa na majibu zaidi katika jambo hilo, nashukuru pia kwa taarifa hii,” alisema Mtaka.

Waziri Simbachawene

Gazeti hili pia jana lilimtafuta kwa njia ya simu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene ambaye naye simu yake iliita bila kupokewa.