NEC yaanza maboresho daftari la wapigakura

New Content Item (1)

Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Ramadhan Kailima

Muktasari:

  • Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeeanza mchakato wa maboresho ya daftari la wapiga kura ikitangaza kuwa na mifumo inayosomana.

Dodoma. Tume ya Taifa ya Uchaguzi imetenga siku saba kwa ajili ya kufanya maandalizi ya daftari la kudumu la wapiga kura ambapo imeita wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa.

Kazi hiyo inatarajia kufanyika katika kata Ng’ambo iliyoko Halmashauri ya Manispaa ya Tabora ambayo itakuwa na vituo sita na nyingine itakuwa ni Kata ya Ikoma iliyoko Halmashauri ya Rolya yenyewe itakuwa na vituo 10 kwenye kazi hiyo itakayoanza Novemba 24 na kuhitimishwa Novemba 30, 2023.

Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Ramadhan Kailima amesema kazi ya uhakiki kwenye vituo hivyo itakuwa ikianza saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 na akaomba vyama vyenye usajili kwa kuwa na mwakilishi katika kila kituo kitakachokuwa na kazi hiyo.

Kailima amewaambia waandishi wa habari leo Ijumaa Novemba 10, 2023 kwamba kazi hiyo itafanyika kwa majaribio katika kata hizo ili kuona namna ambavyo wanaweza kufanya kwa maeneo mengine nchini kwa lengo la kuboresha madaftari wakati taifa linapoelekea kwenye uchaguzi.

“Zoezi hili litafanyika kwa lengo la kupima uwezo wa vifaa na mifumo ya uandikishaji itakayotumika wakati wa ubireshaji wa daftari la kudumu la wapigakura unaotarajiwa kufanyika nchini nzima kwa tarehe na ratiba itakayopangwa na Tume,” amesema Kailima.

Amesema uboreshaji wa daftari hilo utahusisha kuandikisha raia wa Tanzania mwenye umri wa miaka 18 na kuendelea au ambaye kipindi cha uchaguzi atakuwa na umri wa miaka 18 na kuyataja makundi ambayo watapata nafasi ya kufanya maboresho ni waliohama kutoka eneo moja kwenda jingine, waliopoteza au kadi zao kuharibika, wanaorekebisha taarifa zao na kuondoa wapigakura waliopoteza sifa.


Mkurugenzi amesema, tume inakwenda kutumia BVR Kits zenye vifaa vinavyowasiliana ili kuchukua na kutunza taarifa za wapiga kura kwani vifaa hivyo vimeboreshwa tofauti na zile zilizotumika kwenye maboresho ya daftari la kudumu la wapigala mwaka 2015 na 2019.


Akijibu swali kuhusu mfumo wa upigaji kura kwa njia ya kielekroniki, amesema kwa sasa Tume ya Uchaguzi haijafikiria kuwa na mfumo huo wanaamini kuwa hauendi kumaliza malalamiko ya wagombea aliowaita wasiokubali kushindwa hata waliposhindwa.

Ameeleza kuwa hata nchi ambazo zimekuwa na matumizi ya mfumo huo nako kumeendelea kuwa na malalamiko kila baada ya kumalizika kwa uchaguzi akisema wapo watu ambao kazi yao ni kulalamika kwa maelezo hawakubali kushindwa hata waliposhindwa.