Neema yanukia sekta ya gesi Zanzibar

Neema yanukia sekta ya gesi Zanzibar

Muktasari:

  • Matumaini hayo yatapatikana baada kampuni hiyo kuchakata data za mtetemo (3D Seismic) katika eneo la PZ Block ambalo limezunguka visiwa vya Unguja na Pemba.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti wa Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia (ZPRA) visiwani Zanzibar imeonyesha matumaini ya kugundua gesi futi za ujazo trilioni 3.8(TCF) chini ya kampuni ya RAK Gas kutoka Raskheima, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

Matumaini hayo yatapatikana baada kampuni hiyo kuchakata data za mtetemo (3D Seismic) katika eneo la PZ Block ambalo limezunguka visiwa vya Unguja na Pemba.

“Kwa sasa kampuni iko katika matayarisho ya kukusanya data hizo na kuzichakata, data za 2D zinaonyesha kuna uwezekano wa kupata hizo 3.8TCF, kazi ya utafutaji wa data za 2D ilianza 2017,” amesema ofisa msimamizi wa data za gesi kutoka ZPRA, Maryam Amour Suleiman.

Pia, mamlaka hiyo imeingia mkataba na kampuni ya Schlumberger kwa ajili ya kuchataka data za awali za mtetemo (2D Seismic), zilizopo eneo la Utra, kina kirefu cha bahari. Data hizo zilikusanywa kwa mara ya kwanza miaka ya 1950.

“Mkataba uko katika hatua za mwisho, watafanya kazi ya kutafsiri data hizo, ndio tutaona uwezekano wa kupata mafuta au gesi, kazi hiyo itafanyika kati ya Agosti hadi Desemba mwaka huu na Januari huenda tukapata taarifa hizo,”amesema Meneja wa Kitengo cha Mahusiano ZPRA, Khamis Juma Khamis.