Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NEMC yaibua fursa za kiuchumi kwenye taka na urejelezaji

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Balozi Baraka Luvanda.

Muktasari:

  • Kati ya taka zote zinazozalishwa nchini, asilimia 40 hadi 50 hutoka katika miji mikubwa, ikiwemo Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Dodoma, Mbeya na Tanga, hali inayoonesha shinikizo kubwa la kiikolojia na kiuchumi katika maeneo ya mijini.

Dar es Salaam. Tanzania huzalisha zaidi ya tani milioni 14 za taka kila mwaka, ambazo, kwa mujibu wa wataalamu wa mazingira, zinaendelea kuthibitishwa kuwa ni rasilimali muhimu inayoweza kuchochea mapato, ajira na ukuaji wa uchumi wa kijani endapo zitadhibitiwa na kurejelewa kikamilifu.

Hayo yameelezwa jana, Mei 15, 2026 jijini Dar es Salaam katika kikao cha kitaifa cha wadau wa mazingira kilichoandaliwa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), kikilenga kujadili mustakabali wa usimamizi wa taka na kukuza sekta ya urejelezaji nchini.

Katika kikao hicho, wadau wameelezwa kuwa kati ya taka zote zinazozalishwa nchini, asilimia 40 hadi 50 hutoka katika miji mikubwa, ikiwemo Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Dodoma, Mbeya na Tanga, hali inayoonesha shinikizo kubwa la kiikolojia na kiuchumi katika maeneo ya mijini.

Akizungumza katika kikao hicho, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Balozi Baraka Luvanda, amesema dunia inaelekea katika mfumo wa uchumi wa kijani, hivyo usimamizi wa taka na urejelezaji haupaswi kuonekana kama suala la usafi pekee, bali kama fursa kubwa ya kiuchumi.

“Kadri dunia inavyoelekea katika uchumi wa kijani na maendeleo endelevu, usimamizi wa taka na urejelezaji si tu suala la mazingira, bali pia ni fursa ya kiuchumi,” amesema Balozi Luvanda.

Ameongeza kuwa ni wajibu wa Serikali, kwa kushirikiana na wadau binafsi, kuhakikisha kunajengwa mfumo jumuishi wa usimamizi wa taka unaotambua mchango wa kila mhusika, kuanzia ngazi ya ukusanyaji hadi uchakataji, ili kuongeza tija katika sekta hiyo inayokua kwa kasi.

Katika kikao hicho kilichowakutanisha pia waokota taka rejeshi kutoka Mkoa wa Dar es Salaam, ilielezwa kuwa kundi hilo bado linakabiliwa na changamoto ya kipato kidogo, licha ya mchango wake mkubwa katika kupunguza taka zinazokwenda dampo na kuongeza viwango vya urejelezaji nchini.

Balozi Luvanda amebainisha kuwa waokota taka na waokota chuma chakavu ni sehemu muhimu ya mfumo wa usimamizi wa taka nchini, akisema:

“Ninyi ni sehemu ya mfumo wa usimamizi wa taka ambao kwa muda mrefu umechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza taka zinazopelekwa dampo, kuongeza viwango vya urejelezaji, kutoa ajira na kipato kwa maelfu ya wananchi, na kuchangia katika kupunguza uzalishaji wa taka.”

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk Immaculate Seme, amesema mazingira ni nguzo muhimu ya afya ya jamii, ustawi wa kiakili na maendeleo ya kiuchumi ya taifa, akisisitiza kuwa taasisi hiyo imepewa dhamana ya kusimamia usalama wa mazingira nchini kote.

“Leo hii, wadau wa urejelezaji, wawekezaji wa teknolojia za mazingira, waokota taka na wabunifu wa suluhisho za kijani wana mchango mkubwa katika kupunguza uchafuzi wa mazingira, kuongeza ajira za kijani na kuchochea uchumi endelevu wa taifa,” amesema Dk Seme.

Aidha, mmoja wa wadau wa taka rejeshi, Paul Mwihanga, ameelezea changamoto wanazokutana nazo, ikiwemo bei ndogo ya mauzo ya taka za plastiki na mtazamo hasi wa jamii dhidi ya kazi yao.

“Wengi wanasema sisi mateja. Huu unaouona si mwili wangu, lakini nimekuwa mwembamba kwa sababu ya kazi ninayofanya. Angalau sasa hivi tunauza kilo moja ya taka za plastiki kwa shilingi 300, zamani ilikuwa shilingi 200,” amesema Mwihanga.

Ameongeza kuwa iwapo Serikali itawatambua rasmi na kuwawekea mazingira bora ya kazi, sekta ya urejelezaji itaweza kuongeza tija na kupunguza uwepo wa taka barabarani na maeneo ya makazi.

Katika mjadala huo, wataalamu walibainisha kuwa ongezeko la taka nchini lina athari kubwa, ikiwemo kuziba kwa mifereji ya maji, mafuriko ya mara kwa mara, kuongezeka kwa magonjwa ya mlipuko, uchafuzi wa mazingira, kuongezeka kwa gharama za usafi wa miji, pamoja na upotevu wa rasilimali ambazo zingeweza kurejelezwa na kuingizwa tena kwenye mzunguko wa uchumi.