NEMC yaonya matumizi mifuko ya plastiki

What you need to know:

  • NEMC yateketeza kilo 600 za mifuko ya plastiki na tani 500 za mbolea za korosho zilizoisha muda wa matumizi yake, katika maadhimisho ya wiki ya mazingira huku ikiendelea kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plasitiki isiyooza.

Mtwara. Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Kusini limepiga marafuku matumizi ya mifuko ya plastiki isiyooza ambayo imekutwa ikitumika katika masoko mbalimbali mkoani hapa.

Baraza hilo limetekekeza zaidi ya kilo 600 za mifuko yenye Sh4 milioni sambamba na kuteketeza mbolea za korosho tani 500, iliyoisha muda wake wa matumizi.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha wiki ya mazingira Meneja wa NEMC kanda hiyo Mhandisi Boniphace Guni amesema kuwa serikali ilishapiga marufuku matumizi ya mifuko hiyo ambapo wao wanatekeleza sheria kwa kuiteketeza.

“Lakini pia serikali inaendela kupiga marufuku katazo la mifuko ya plastiki almaafuru vifungashio vinavyotumika kama mifuko ya plastiki, oparesheni itaendelea na kuwachukulia hatua wote watakao husika kukiuka maelekezo ya selikali,” amebainisha.

Nae Afisa Mazingira wa NEMC Khalid Mwakoba amesema kuwa mifuko mbadala ni ile inayooza yenye rangi tofauti tofauti inauzwa katika masoko mbalimbali na inatambuliwa na NEMC.

“Mifuko isiyoruhusiwa tunaikamata na kuitekeeleza ni muhimu wafanyabishara wafuate sheria kwa kuweka bidhaa katika vifungashio na kisha kubebea katika mifuko mbadala yenye rangi,” amesema

Nae Afisa Mazingira wa Kiwanda cha Saruji Dangote Mohamed Bakari alisema kuwa kiwanda hicho kina kichomeo chenye uwezo wa kutekekeza tani tano za taka kwa saa moja.

“Tunashirikiana na serikali kwa vibali maalum kwa kuteketeza takataka ambapo tunakichomeo cha taka chenye uwezo wa kupoteza kabisa taka hizo. Kwa kutumia joto kali, mtambo huo unapoteza hali ya kuwepo kwa karbondiaxide, na tunakibali cha kuteketeza hadi taka za plastic mataili na oili chafu,” amesema.

Nae Mkaguzi wa Kemikali kutoka ofisi ya Mkemia Mkuu Kanda ya Kusini Shaidu Shafiru amesema kuwa kemikali zikipitisha muda wake zinakuwa taka hivyo kwa mujibu wa sheria zinatakiwa kuteketezwa chini ya mkemia, NEMC na taasisi zingine.

Nae Meneja wa kampuni ya G20 ambao wadau wa uteketezaji wa taka hatarishi Andrew Kaluwa ambaye ni mhandisi kitaaluma, amesema kuwa wanakusanya na kutelekeza taka hatarishi kwa mujibu wa sheria.

“Taka tunazoteketeza mara nyingi huwa ni kemikali zilizoisha muda, plastiki, madawa, vifaa tiba na taka ambazo zimeainishwa kwenye sheria ya mazingira ambazo zinaweza kuwa hatarishi kwa jamii na viumbe hai,” amesema mhandisi huyo.