New MV Victoria kuanza safari leo

New MV Victoria kuanza safari leo

Muktasari:

  • Kaimu Mhandisi Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli nchini (MSCL), Abel Gwanafyo amesema ukarabati na ukaguzi wa meli ya New MV Victoria umekamilika.

Mwanza. Kaimu Mhandisi Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli nchini (MSCL), Abel Gwanafyo amesema ukarabati na ukaguzi wa meli ya New MV Victoria umekamilika.

Ukarabati huo umetumia Sh9 milioni, na kuanza kutoa huduma ya usafiri leo Alhamisi Oktoba 14, 2021.

Meli hiyo ilisitisha kutoa huduma Septemba 22 mwaka huu ili kupisha ukarabati na ukaguzi wa kawaida unaofanyika kila baada ya mwaka mmoja.

Amesema meli hiyo itaanza safari zake leo kutokea jijini Mwanza kuelekea Bukoba mkoani Kagera, wakati Tanzania ikitimiza miaka 22 tangu kifo cha Baba wa Taifa Julius Nyerere.

"Ukarabati na ukaguzi uliyofanyika ni pamoja na ukaguzi wa wafanyakazi wa ndani ya meli, uwekaji na ukaguzi wa vifaa vya kuzima moto, kujaribu boti za dharura na maboya," amesema Gwanafyo

Akizungumzia uboreshaji wa huduma katika meli hiyo Ofisa Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma, Abdullahman Salim amesema ukarabati huo umeambatana na uboreshaji wa huduma za chakula na vinywaji ndani ya meli hiyo.

Amesema kampuni hiyo imeongeza aina za vyakula ndani ya meli hiyo huku bei yake ikianzia Sh1,500 tofauti na awali ambapo bei ya chakula ilianzia Sh5,000.

"Pia tumeongeza mwanamuziki wa kike atakayeshirikiana na yule wa kiume ili kuongeza burudani kwa abiria wanaosafiri kati ya Mwanza na Kagera," amesema Salim.

Ameongeza kwamba ili kuvutia abiria katika meli, kampuni itatoa tiketi 22 za bure kwa mfumo wa bahati nasibu kwa abiria wa meli hiyo.

"Watu 11 wanaotoka Mwanza watajishindia tiketi ya kusafiri kwa meli hii bure kwa njia ya bahati nasibu na 11 wengine kutoka Bukoba mkoani Kagera kurejea Mwanza pia watapatiwa tiketi hizo," amesema Salim.