Ukarabati wa meli kuibua shida ya usafiri Mwanza-Kagera

Ukarabati wa meli kuibua shida ya usafiri Mwanza-Kagera

Muktasari:

  •  Usafiri wa abiria na mizigo kati ya Mkoa wa Mwanza na Kagera utadorora kwa siku 14 kutokana na meli ya Mv Victoria na Mv Butiama kufanyiwa ukarabati.


Mwanza. Usafiri wa abiria na mizigo kati ya Mkoa wa Mwanza na Kagera utadorora kwa siku 14 kutokana na meli ya Mv Victoria na Mv Butiama kufanyiwa ukarabati.

Mv Victoria ilianza kutoa huduma Agosti 16, 2020 na Mv Butiama yenyewe inatoa huduma zake kati ya Mwanza na Nansio- Ukerewe.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Septemba 21, 2021 kaimu ofisa mtendaji mkuu wa kampuni ya huduma za meli nchini (MSCL),   Abel Gwanafyo amesema ukarabati wa Mv Victoria  utafanyika kati ya Septemba 29 hadi Oktoba 8 , 2021 huku Mv Butiama ikisimama kutoa huduma kupisha ukarabati huo kuanzia Oktoba 11 hadi Oktoba 18,2021.

"Lengo la kusimama kwa meli hizi ni kutoa nafasi ili zifanyiwe ukarabati ambao hufanyika kwa kila meli inapotumika kwa mwaka mmoja, pia kutoa nafasi kwa Wakala wa usafirishaji majini (TASAC) kufanya ukaguzi na kutoa cheti cha ubora kwa meli hizi ili ziendelee kutoa huduma bora," amesema Gwanafyo.

Gwanafyo amesema kwa kipindi hicho huduma ya usafirishaji kati ya Mwanza na Kagera itasimama huku wateja na wafanyabiashara wanaosafirisha bidhaa kati ya maeneo hayo wakitakiwa kutumia njia mbadala kupata huduma hiyo kwa kipindi cha siku 14.

"Tunawaazima wenye malori wateja wetu kwa kipindi hicho lakini baada ya siku kumi na nne tunaamini wateja wetu watarejea kwa wingi kuendelea na huduma zetu," amesema Gwanafyo.

Ameongeza,  "kwa upande wa wasafiri wanaotumia MV Butiama, wao huduma itaendelea kama kawaida kwa sababu tuna meli yetu ambayo ilikuwa inafanyiwa ukarabati ya MV Clarius ambayo imeshafikia hatua ya kuanza kutoa huduma tena, kwa hiyo hawa wasihofu,"

Kwa upande wake meneja masoko na biashara wa MSCL, Anselm Namala amesema kusimama huko pia kunalenga kutoa nafasi kwao kumaliza changamoto zilizokuwa zikiwasilishwa na wateja.

"Kwenye meli ya New MV Victoria watu wamekuwa wakilalamika kuwepo na msanii mmoja wa muziki wa rhumba, itakapofanyiwa ukarabati  tutakuwa tumeongeza msanii mwingine pia kutakuwa na nafasi kwa wateja wetu kupanda jukwaani kuimba nyimbo mbalimbali, " amesema Namala.

Mfanyabiashara, Ibrahim Salum amesema kusimama kwa meli hizo kutaongeza gharama ya usafirishaji wa bidhaa na abiria kati ya Mkoa wa Mwanza na Kagera.


"Kwenye meli hii tulikuwa tunalipia Sh27,000 kwa tani moja ya mzigo na tiketi ya daraja la chini kwa abiria ilikuwa hadi Sh16,000 sasa sijui kwenye malori itakuwaje! Siku za nyuma tani moja walikuwa wanatufanyia hadi Sh60,000, tunaomba watusaidie kurekebisha meli hii haraka," amesema Salum.