Ngono, ulevi vinavyorudisha nyuma maisha ya wavuvi Ziwa Victoria

Wavuvi na wachuuzi wa dagaa na samaki katika Mwalo wa Mswahili jijini Mwanza wakiendelea na shughuli zao katika mwalo huo. Picha na Anania Kajuni

Muktasari:

  •  Kutokana na mazingira ya kazi ya wavuvi kuonekana magumu, wavuvi wengi hawana uwezo wa kutunza fedha kwa ajili ya maendeleo hivyo, wakipata wanazitumia kwa kufanya starehe.

Mwanza. “Wakipata mapato hutawaona wakiingia ziwani tena…wataenda kwenye baa, watakula hizo hela mpaka ziishe ndo warudi tena ziwani kuvua.”

Huyo ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wavuvi nchini (Tafu), Jephta Machandaro akielezea sababu kwa nini maisha ya baadhi ya wavuvi ni duni licha ya kujiingizia kipato cha uhakika kila wakipata samaki na mazao yake.

Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi Aprili 11, 2024, Machandaro amesema tabia ya baadhi ya wavuvi kupenda starehe hususan matumizi ya vilevi na ngono, si tu inawasababishia kutoendelea kiuchumi, bali pia ndio chanzo cha kupata magonjwa ya zinaa ukiwamo Ukimwi.

“Wale wenye zana za uvuvi hao angalau maisha yao yanakuwa ni nafuu. Lakini wale wavuvi wanaoingia ziwani kuvua, wakipata fedha wananunua chakula, wanawake na pombe basi, hiyo siku imeisha, anajua na kesho atapata nyingine,” amesema Machandaro.

Ameongeza; “Na wanatumia pombe kwa wingi na bangi….sasa watu kama hao huwezi kutegemea watabadilika hata kama utawapa hela nyingi watazitumia mpaka ziishe. Wakipata mapato leo, ukawalipa kama wewe ndio tajiri, hutowaona wakiingia tena ziwani, wataingia kwenye baa watazinywea hizo hela mpaka ziishe,” amesema.

Akiunga mkono hoja ya Machandaro, Katibu wa Umoja wa Wavuvi Magu, Busega na Bunda, Ndalahwa Mabula amesema kutokana na mazingira ya kazi ya wavuvi kuonekana magumu, wengi wao hawana uwezo wa kutunza fedha kwa ajili ya maendeleo, hivyo wakipata wanazitumia kufanya starehe.

“Kuna aina mbalimbali ya ufanyaji kazi ambayo huwa tunaitumia kwa maana ya kufanya malipo ya wavuvi, kuna wavuvi wanaovua kwa mkataba na wengine wanavua kwa zamu. Zamu ni kwamba, wanatega labda siku 20 za tajiri halafu wanatega siku tano za kwao. Mfano mimi natumia hiyo ya siku 25 na siku sita za kwao,” amesema Mabula ambaye pia ni mmiliki wa zana za uvuvi.

Amesema kwa hesabu za haraka, mvuvi anafaidika kwa kupata fedha nyingi kuanzia za chai anazolipwa kila siku, ambayo ni Sh1,000, anazolipwa kwa kila kilo moja ya samaki atakayovua, ila shida inaanzia pale anavyopanga matumizi yake.

“Kwa mfano hela anazolipwa kwa ajili ya chai, zile anazopata kwa kuingia ziwani na kuvua na akivua kila kilo moja inalipwa. Sasa akivua samaki kilo 10 ana hela kiasi gani hapo? Na bado tajiri huwa navua kwa siku 25 zinazobakia ni za kwao.

“Wakati mwingine siku hizo tano au sita wanazomalizia mwezi wanajikuta wanapata samaki wengi zaidi, kwa hiyo katika kilo kwa mfano mimi nawalipa Sh6, 000 kwenye zamu zao. Wakipata kilo 100 kwa hizo siku sita inamaanisha wana Sh600, 000. Ukikuta ni mtu wa kutunza kwa ajili ya kufanya maendeleo anafika mbali,” anasema.

Kwa nini wanakuwa walevi

Wakati hali ya maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) mkoani Mwanza ikipungua kutoka asilimia 7.2 mwaka 2016/17 hadi asilimia 4.7 mwaka 2021/22, ngono na ulevi vinatajwa kuwaponza wavuvi na kusababisha kuendelea kwa maambukizi ya VVU katika maeneo yenye shughuli za uvuvi.

Kwa mujibu wa Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya Ukimwi wa mwaka 2021/22, asilimia 4.7 ya wakazi wa Mwanza sawa na watu 151,214 kati ya milioni 3.2, wanaishi na VVU huku zaidi ya nusu wakiwa ni vijana, wenye umri kati ya miaka 15 hadi 40.

Hata hivyo, kutokana na mwingiliano mkubwa wa watu na fedha katika sehemu zenye shughuli za uvuvi, inadaiwa maambukizi huongezeka licha ya kutokuwapo takwimu za moja kwa moja.

Mvuvi wa mwalo wa Kayenze Ndogo Manispaa ya IIemela, Butuli Emmanuel anasema wengi wao wanaendekeza ulevi kwa sababu ya mambo  ya ajabu wanayoyashuhudia ziwani.

“Bila kujiboosti kidogo mambo hayaendi. Tunakutana na mambo mengi, kwa hiyo tukifika salama nchi kavu lazima tujipongeze, maana maisha yetu wavuvi ni mafupi mno,” anasema Emmanuel.

Naye Magreth John, mchuuzi wa samaki na dagaa katika Mwalo wa Mswahili amesema ukosefu wa elimu ya nidhamu ya fedha na namna ya kukabiliana na maambukizi ya Ukimwi, ni chanzo cha wavuvi hao kutumia fedha kwa wanawake bila kuwa na hofu ya kupata maambikizi ya VVU na magonjwa mengine ya zinaa.

"Kila mmoja anayefanya kazi ya kujiuza huwa anakuwa na kakazi ka kujishikiza mwaloni, anaweza kuwa mchuuzi wa dagaa au samaki au mamantilie, pale si kwamba anafanya ile biashara kweli, ila anakuwa anatega muda ambao wavuvi wamemaliza kuuza samaki wana ‘maokoto’ yao wanaelewana na kuondoka kwenda kufanya ngono. Sio kwamba hapa kuna madanguro, hapana ila wavuvi wenyewe wanawajua wanawake wanaojiuza, kwa hiyo wanaondoka nao moja kwa moja," anasema Magreth.

Mvuvi wa mwalo wa Butuja katika Manispaa ya Ilemela, Ramadhani Hassan amesema unywaji pombe uliokithiri kwa baadhi ya wavuvi baada ya kutoka ziwani, huchangia wao kufanya ngono zembe.

Mvuvi wa mwalo wa Mswahili uliopo Wilaya ya Nyamagana, Baraka Kabadua akizungumzia hilo, amesema mbali na ulevi, mwingiliano mkubwa wa watu, hasa wanawake katika maeneo hayo kunasababisha wawe na tamaa ya kujiingiza kwenye mapenzi.

"Maeneo yoyote yenye shughuli za uvuvi ni hatari kwa maambukizi, kwa sababu watu walioko hapo wa fedha nyingi na matumizi ya kwanza ni kwenye ngono na pombe, na wanawake nao wamelijua hilo wanakuja kila siku wa kila aina,” anasema Kabadua.

Kwa upande wake Chota Simba mkazi wa Sabasaba anayejishughulisha na uvuvi anasema kukosekana kwa elimu ya namna ya kukabiliana na maambukizi ya VVU na uwepo wa biashara ya ngono katika maeneo wanayofanya kazi za uvuvi, kunachochea wengi kujikuta wakitumia vibaya vipato vyao vya kila siku.

"Maeneo kama haya kuna tabia zinazoibuka za vijana, mfano watoto wa kike wengi kuanzia miaka 17 na kuendelea, wanakuja kufanya biashara ya kujiuza kwa sababu kuna hela na wanaipata ndani ya muda mfupi, hawazisotei. Na kutokana na ulimbukeni wa wanaume ambao ndio wavuvi na baadhi yao hata elimu hawana kuhusiana na magonjwa hatarishi, hujikuta wanatumbukia kwenye matatizo,” anasema Simba.


Nini kifanyike kuwainua wavuvi?

Pamoja na kushauri elimu ya fedha kwa wavuvi, Katibu wa Tafu, Jephta Machandaro amesema ni wakati sasa Serikali ifanye sensa kwenye maeneo ya uvuvi kuwaondoa watu wasiohusiana na kazi hiyo wakiwemo wanawake wanaojiuza.

“Serikali ifanye sensa ya tathmini ya visiwa ambavyo vinastahili kwa shughuli za uvuvi na vikae kweli kwa ajili ya uvuvi na kuwe na mipaka ya watu ambao wanaweza kuishi mle kwa ajili ya makambi yao,”amesema


Kupunguza maambukizi ya VVU

Mratibu Udhibiti Ukimwi, Magonjwa ya Zinaa na Homa ya Inni kutoka Halmashauri ya Buchosa, Dk Christian Chacha amesema elimu sahihi kuhusu maambukizi ya VVU na njia za uzazi wa mpango zinapaswa kufikishwa kwa wavuvi ili wawe na uelewa wa kutosha kuhusu maambukizi hayo.

"Endapo elimu sahihi itafikishwa, watapata  uelewa wa kutosha, lakini pia matumizi sahihi ya vidonge vya kuzuia kama Prep yakizingatiwa, tutaweza kupunguza maambukizi kwa kiwango kikubwa. Mbali na hivyo, matumizi ya kondom pia yanapaswa kusisitizwa kwao, itasaidia,” amesema Dk Chacha.