NHIF yapewa miezi mitatu kumaliza usumbufu kwa wanachama

Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel akizungumza leo Ijumaa Novemba 10, 2023 bungeni jijini Dodoma.

Muktasari:

  • Baada ya Mbunge wa Geita Mjini (CCM), Constatine Kanyasu kuzuia ahoji matibabu ya baadhi ya wagonjwa wenye bima za afya wakiwa hospitali, Serikali yaeleza hatua inazochukua.

Dodoma. Serikali ameipa miezi mitatu menejimenti ya Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF ihakikishe inaboresha mifumo ya Tehama itakayoweza kuondoa usumbufu na pia kudhibiti udanganyifu pasipo kuwa kero kwa wanufaika wa mfuko.

Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel amesema hayo leo Ijumaa Novemba 10, 2023 wakati akijibu swali hiyo Mbunge wa Geita Mjini (CCM), Constatine Kanyasu.

Mbunge huyo amehoji kwa nini Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) inazuia matibabu ya baadhi ya wagonjwa wenye Bima za Afya wakiwa hospitali.

Akijibu swali hilo, Dk Mollel amesema ni kweli kulikuwa na zoezi la uhakiki wa uhalali wa wanufaika wa mfuko wa bima ya Afya, zoezi hilo lilileta usumbufu ambao ungeweza kuzuilika kama wahakiki hao wangetumika wataalamu wenye miiko ya taaluma ya tiba.

“Wizara ilipopata malalamiko hayo ilifuatilia mara moja na kufanya maboresho ambayo yaliyoondoa usumbufu kwa wateja,”amesema.

Ameagiza menejimenti ya mfuko huo katika kipindi cha miezi mitatu ihakikishe inaboresha mifumo ya Tehama itakayoweza kuondoa usumbufu na pia kudhibiti udanganyifu pasipo kuwa kero kwa wanufaika wa mfuko.

Katika swali la nyongeza Kanyasu alisema kuna baadhi ya wanufaika wa mfuko huo walilelewa na watu ambao siyo wazazi wao kwa kuzaliwa lakini wakafutiwa huduma.

Amehoji Serikali inampango gani wa haraka wa kuwatambua na kuwarejeshea huduma na hivyo.

Amesema pia kuna wagonjwa walinyang’anywa kadi zao wakiwa hospitali na kupelekwa polisi ambapo walifunguliwa mashtaka.

Kanyasu amehoji nini kimefanyika baada ya hilo kwa watumishi hao.

Akibu maswali hayo, Dk Mollel amesema kwa kuwa wamepitisha muswada wa Bima ya Afya kwa Wote hivi karibuni na wanakwenda kutengeneza kanuni wataangalia ni kwa jinsi gani suala hilo la waliolelewa na wazazi ambao si wa kuzaliwa halijitokezi tena.

Kuhusu walionyang’anywa kadi, Dk Mollel amesema suala hilo lina pande mbili kuna walionyang’anywa kweli walifanya udanganyifu hao watashughulikiwa kwa mujibu wa taratibu.

Amesema wapo baadhi walinyanganywa kutokana na makosa ya watumishi kutoa kadi zinazotofautiana na majina yaliyo kwenye vyeti vya kuzaliwa na kwamba hilo wataliangalia mfano huo kulitatua kwa mtu mmoja na nchi nzima.