Nida yapongezwa kumaliza kero ya vitambulisho

Muktasari:
- Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania, Jumanne Sagini amesema Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) inaandaa mkakati wa kuongeza uhakiki wa kutumia alama ya mboni za macho na sura ili kuwezesha utambuzi na uhakiki kwa watu wasiokuwa na alama za vidole.
Dar es Salaam. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama imeipongeza Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) kwa juhudi inazofanya za kuchapisha vitambulisho vingi vya Taifa na kuvisambaza kwa wananchi.
Imesema hatua hiyo inalenga kumaliza kero sugu ya upatikanaji wa Vitambulisho vya Taifa kwa wananchi.
Pongezi hizo zilitolewa jana Ijumaa, Machi 15, 2024 na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Vita Kawawa wakati kamati hiyo ilipofanya ziara Nida, kwenye kituo kikuu cha kuchakata na kutunza taarifa za watu na kukagua mradi wa vitambulisho vya Taifa.
"Kamati tumefurahishwa sana na jitihada za mkurugenzi mkuu, menejimenti na watumishi wote wa Nida katika kuhakikisha mnafikisha malengo ya kuzalisha vitambulisho vya Taifa kwa wananchi waliokuwa wamesalia zaidi ya milioni kumi. Hakika mmefanya kazi nzuri na mnastahili pongezi za dhati," amesema Kawawa
Amesema tatizo la kutopatikana kwa vitambulisho ilikuwa ni kilio cha wananchi kila kona, “lakini sasa mmezalisha vitambulisho vingi sana na kuvipeleka kwa wananchi katika mitaa, vijiji na vitongoji vyao na hivyo kilio hicho hakipo tena.”
Awali, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Jumanne Sagini katika taarifa yake, iliyowasilishwa kwa niaba yake na Mkurugenzi Mkuu wa Nida, Ismail Rumatila, amesema hadi kufikia Februari 2024, Nida imechapisha vitambulisho 20,548,067 na kusambaza 19,743,367.
Amesema kasi ya uzalishaji na usambazaji imeongezeka kutokana na Serikali kutoa fedha za ununuzi wa kadighafi 13,514,251 ambazo zinatumika kuzalisha vitambulisho vya watu wote waliokwishasajiliwa na kupata Namba za Utambulisho wa Taifa (NIN).
Kuhusu kuboresha na kuongeza njia za uhakiki na utambuzi, Sagini amesema Nida inaandaa mkakati kwa kuongeza uhakiki wa kutumia alama ya mboni za macho na sura ili kuwezesha utambuzi na uhakiki kwa watu wasiokuwa na alama za vidole.
Amesema mamlaka hiyo itaboresha usimamizi wa taarifa na kuboresha uwezo wa kuthibitisha utambulisho wa mtu kipekee.
Amedokeza katika mwaka huu wa fedha, Nida imeweka lengo la kukusanya maduhuli ya Sh24 milioni na hadi kufikia Februari 2024, imekusanya Sh19.1 milioni sawa na asilimia 79.6 ya lengo la mwaka huu wa fedha.
“Makusanyo hayo yametokana na tozo za huduma ya ushirikishanaji wa taarifa na huduma za usajili na utambuzi kwa wananchi na wageni wakaazi. Fedha hizi zimewasilishwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina,” amesema Sagini.