Nida yatoa ruksa kubadilisha kitambulisho kwa kulipia

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Geoffrey Tengeneza

Mwanza. Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) imesema ni ruksa kwa yeyote anayetaka kubadilisha kitambulisho chake cha Taifa kwa kulipia gharama ya Sh20,000.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Geoffrey Tengeneza ameyasema hayo Jumatano Februari 22, 2023 wakati wa mjadala ulioandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited kupitia mtandao wa kijamii ya Twitter (Mwananchi Twitter Space) kujadili uamuzi wa kuondoa ukomo wa muda kwenye vitambulisho vya Taifa.

“Mwananchi yeyote anaweza kwa hiari yake kuomba kitambulisho kipya kisicho na ukomo wa muda; lakini anayeamua kufanya hivyo awe tayari kulipia gharama ya Sh20, 000,” amesema Tengeneza.

Amesema mwenye nia hiyo atalazimika kufika kwenye ofisi yoyote ya Nida iliyo jirani kukamilisha taratibu ikiwemo kuongeza taarifa mpya zisizokuwepo kwenye kitambulisho chake cha awali.

Wakijadili mada inayosema “Vitambulisho vya Taifa kuondolewa ukomo kuna athari gani?” Wadau wamegawanyika katika makundi mawili, moja likunga mkono mpango huo wa Serikali na lingine likipinga.

Wanaounga mkono akiwemo mbunge wa zamani, Suzan Lyimo, wanasema mpango huo utawaondolea wananchi adha ya kulazimika kutafuta vitambulisho vipya kila ukomo wa muda unapofika huku wakitumia muda mrefu kutafuta vitambulisho badala ya kushiriki shughuli za uzalishaji.

“Hakukuwa na sababu za kuweka ukomo kwenye vitambulisho vya Taifa kwa sababu uraia ni suala lisilo na ukomo wa muda,” amesema Suzan Lyimo, mbunge wa zamani wa Viti Maalum (Chadema) ambaye kwa sasa anatambulishwa na chama chake kama Spika wa Bunge la Wananchi.

Akichokoza mada wakati wa mjadala huo, William Shao amesema uamuzi huo una faida chanya na hasi kwa wananchi na Serikali yenyewe huku akitaja faida kuwa ni fursa ya kuingiza taarifa mpya kulingana na anuani ya makazi, umri, picha na mabadiliko ya teknolojia.

Amesema japo yapo mataifa mengi duniani yakiwemo ya Kiafrika kama Kenya, Botswana na Ghana vinatoa vitambulisho vya kudumu vya Taifa, suala la kuisha vitambulisho ni muhimu ili kuingiza taarifa mpya kuanzia mabadiliko ya imani za kidini, ndoa, kiwango cha elimu, mabadiliko ya makazi na uraia.