Niwemugizi:Rais Samia usikubali kulinganishwa na Mungu

Muktasari:

  • Askofu wa Jimbo Katoliki  la Rulenge-Ngara, Severine Niwemugizi amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kutokubali kulinganishwa na Mungu kwa namna yoyote ile.

Askofu wa Jimbo Katoliki  la Rulenge-Ngara, Severine Niwemugizi amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kutokubali kulinganishwa na Mungu kwa namna yoyote ile.

Amesema hayo leo Jumanne Februari 22, 2022 katika sherehe za Jubilee ya miaka yake 25 inayofanyika wilayani Ngara mkoani Kagera.

“Nikikuombea uwe na afya njema na uwe mnyenyekevu lakini pamoja na madaraka hayo makubwa uliyonayo usikubali kamwe kulinganishwa na Mungu kwa namna yoyote ile  usikubali."

"Ninakumbuka sana Hayati Benjamini Mkapa najua huko mlikuwa mmezoea mtukufu rais, mtukufu rais alifika mahali akawa mkali kabisa mtukufu ni Mungu tu naomba hilo liwe neno kwako, " amesema Askofu Niwemuguzi.

Huku akiwa makini amesisitiza,"basi nakuombea Mungu akusaidie kukuza upendo kati ya Watanzania unaotuongoza,  ukuze haki nayo haki izae amani na utulivu na kukuza demokrasia katika nchi yetu."

“Ukuze upendo na mshikamo wa Watanzania ili hatimaye utumishi wako utukuke na kuacha alama itakayoonwa kwa vizazi vingi.

Mungu akujalie hekima na uvumilivu wa kusikiliza hata yale yanayokela masikio yako,  unajua sisi watoto wako tuko wakorofi, Mungu akujalie tu hekima na uvumulivu hasa pale unapokuwa ni ushauri wenye nia njema ya kulijenga Taifa letu liendelee kuheshimika ndani na nje."