Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wafanyakazi wa majumbani 700 wapewa mafunzo Veta

Muktasari:

  • Mtalaa huu umeanzishwa ili kuwasaidia wafanyakazi wa majumbani kupata ujuzi stahiki ikiwamo namna ya kupika, kuishi vizuri na wazee, watoto sambamba na stadi za maisha.

Dar es Salaam. Zaidi ya wafanyakazi wa majumbani 700 wamepatiwa mafunzo ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi kupitia mtalaa mpya ulioanzishwa na Mamlaka ya Ufundi Stadi (Veta).

Mtaala huo ulioanza Aprili mwaka jana unatekelezwa na Veta kwa kushirikiana na Shirika la CVM ukilenga kuboresha utendaji kazi wa wasaidizi hao na kuondoa malalamiko yaliyokiwapo awali kutoka kwa waajiri.

Hayo yamesemwa leo Julai 2, 2025 na mtaalamu wa masuala ya jinsia kutika Veta, Maria Shimba wakati akizungumza na Mwananchi katika Maonyesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu Sabasaba yanayoendelea Dar es Salaam.

Shimba amesema wafanyakazi hao wamesoma  masomo mbalimbali ikiwamo namna ya kuandaa chakula kwa ajali ya watoto na wazee.

Katika mtalaa huo, mambo mengine wanayosoma ni ujuzi wa kimaisha, usalama jikoni, usafi, uvumilivu, huduma kwa wateja pamoja na haki za kazi.

“Hao ni waliosoma, lakini tunaamini wapo wengi, hivyo kupitia maonyesho haya tuko kwa ajili ya kuhamasisha  kuhusu mtalaa huu kwa Watanzania ili kujua kuwa zipo kozi mbalimbali  zinazotolewa kwa wafanyakazi wa majumbani,” amesema.

Amesema kozi hizo hutolewa kwa vipindi tofauti ikiwamo ya mwezi mmoja, mitatu hadi sita.

Shimba amesema mafunzo hayo kwa sasa yanatolewa katika vyuo sita vya Veta vya Tanzania Bara na Zanzibar ikiwemo Chang'ombe (Dar es Salaam), Dodoma, Lindi, Tanga, Iringa na Mikumi.

“Kwa upande wa Zanzibar mafunzo yanatolewa katika chuo cha Veta cha Mkokotoni, Makindudi na Daya Pemba na mwanafunzi akihitimu anapewa cheti cha ubobezi wa kazi za majumbani,” amesema.

Maria amesema wanatumia maonyesho ya Sabasaba kuelezea kutangaza mtalaa huo kwa kuwa ni msaada wa kupunguza shida kwa wafanyakazi wa majumbani pamoja na kupokea  ujuzi.

Mtalaa huu unakuja wakati ambao kumekuwapo kwa malalamiko kutoka kwa watu mbalimbali juu ya baadhi ya wasaidizi wa ndani kushindwa kujua namna ya kufanya shughuli zao kwa ufanisi ikiwamo ulezi wa watoto.

Pia, linafanyika wakati ambao baadhi ya watu bado wameendelea kuwakimbia watu ambao wamepitia katika fani hiyo kwa kuogopa kuwalipa mishahara mikubwa.

“Tatizo watu wanataka watu ambao watawalipa fedha kidogo bila kujali wingi wa kazi atakazofanya huyo mtu huko nyumbani. Wakati mwingine malipo kidogo yanaweza kuwa chanzo cha mtu kufanya vitu vyake bila kujali athari zinazoweza kutokea kwa familia,” amesema Hawa Balali mkazi wa Kinondoni.

Maneno yake yaliungwa mkono na Salma Sulle mkazi wa Kinondoni B ambaye amesema kama mtalaa huo umeanzishwa ni wakati sasa wa kuangalia namna ya kuwarasimisha watumishi wote.

“Isijekuwa ni chaguo, mtu akitaka kusoma asome au aache, ni vyema kuhakikisha watu wote wanakuwa na ujuzi unaotakiwa kama inavyostahili. Hii itasaidia kupunguza ukatili majumbani hasa kwa watoto na wazee,” amesema Salma.