NMB yaahidi kuinua wachimbaji wadogo

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde akipata maelezo kutoka katika banda la benki ya NMB kwenye kongamano na maonyesho ya madini yaliyofanyika mjini Musoma. Picha na Beldina Nyakeke
Muktasari:
- Katika kutambua umuhimu wa sekta hiyo, benki ya NMB iliamua kuanzisha klabu ya wachimbaji (Mining Club) kwa malengo ya kuboresha mnyororo wa thamani katika sekta hiyo.
Musoma. Benki ya NMB imeahidi kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuboresha na kuimarisha sekta ya madini nchini, hatua ambayo itasaidia kuifanya sekta hiyo kuwa sehemu muhimu na imara ya ukuaji wa uchumi wa nchi na wananchi wake.
Ahadi hiyo imetolewa leo Ijumaa, Juni 6, 2025, na Meneja wa NMB Kanda ya Ziwa Victoria, Faraja Ng’ingo, kwenye hitimisho la kongamano na maonyesho ya madini mkoani Mara yaliyofanyika kwa muda wa siku nne mjini Musoma.
Amesema katika kutambua umuhimu wa sekta hiyo, benki hiyo iliamua kuanzisha klabu ya wachimbaji (Mining Club) kwa malengo ya kuboresha mnyororo wa thamani katika sekta hiyo.
"Baada ya kuona umuhimu wa sekta hii na kuzitambua changamoto zake, tulianzisha klabu hii ambayo pamoja na mambo mengine inahusika na utoaji wa mikopo kwa wachimbaji kwa ajili ya mitaji na ununuzi wa vifaa na mitambo kwa ajili ya shughuli za uchimbaji," amesema.
Amefafanua kuwa benki hiyo imedhamiria kubadilisha sekta ya uchimbaji nchini, ambapo inalenga kuwainua wachimbaji wadogo kuwa wa kati na hatimaye kuwa wakubwa. Mbali na mikopo hiyo, benki hiyo kupitia klabu hiyo imekuwa ikitoa elimu juu ya uboreshaji wa sekta hiyo, ikiwemo suala la uchimbaji wa kisasa wa kisayansi.
Amesema kupitia klabu hiyo wachimbaji wamepokea mikopo iliyowawezesha kuboresha shughuli zao, huku akimtolea mfano mchimbaji mmoja aliyeanza kwa mkopo wa Sh5 milioni lakini hadi sasa ana mkopo wa zaidi ya Sh1 bilioni.
Ameongeza kuwa lengo la benki hiyo ni kutaka kuifanya sekta ya madini kuwa kinara katika kuchangia pato la taifa na pato la mtu mmoja mmoja, jambo ambalo linawezekana kwa kuwa sekta hiyo ina fursa nyingi.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, ameitaka NMB pamoja na taasisi nyingine za fedha kutoa elimu kwa wachimbaji na kuwaelekeza namna ya kunufaika na mikopo inayotolewa na taasisi hizo ili kuboresha shughuli zao.
Amesema maonyesho na kongamano hilo lililofanyika kwa mara ya kwanza mkoani humo ni moja ya mikakati ya kufanya mapinduzi katika sekta ya madini mkoani humo, kwani wachimbaji na wadau wameweza kupata elimu juu ya matumizi sahihi ya teknolojia na namna ya kufikia teknolojia hizo.
"Kwa sasa sekta hii inachangia asilimia 18 ya pato la mkoa, lakini tumejiwekea malengo kuwa miaka mitatu ijayo sekta hii itakuwa inachangia zaidi ya asilimia 40 kwenye pato la mkoa wetu, na hapa ndipo tunapozihitaji taasisi kama NMB," amesema.
Akizungumza katika kongamano hilo, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania (Femata), John Binna, amesema benki ya NMB imekuwa ni mkombozi mkubwa kwa wachimbaji wa madini kwa namna ambavyo imekuwa ikishirikiana nao katika kutatua changamoto zao, hususan ukosefu wa mitaji.
"Hii klabu iliyoanzishwa na NMB ni msaada mkubwa sana kwetu wachimbaji. Nakumbuka walitenga zaidi ya Sh160 bilioni kwa ajili yetu. Niiombe tu benki yetu iendelee kufanya utafiti ili kuja na majibu ya namna ya kutatua changamoto zinazowakabili wachimbaji nchini," amesema Binna.
Mwakilishi wa Ofisi ya Madini Mkoa wa Mara, Hamad Kalaye, amesema benki hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika kuboresha sekta ya madini ndani ya mkoa huo, hasa kwa kutoa mikopo inayowawezesha wachimbaji kufanya shughuli zao.
Amesema kulingana na mazingira ya utendaji ya wachimbaji, hasa wale wadogo, awali ilikuwa vigumu kwao kupata mikopo, lakini benki hiyo imeweka utaratibu mzuri ambao unawatambua wachimbaji wanaomiliki maduara badala ya utaratibu wa awali uliokuwa unawatambua wenye leseni pekee
"Wachimbaji wengi wana changamoto ya mitaji, na mwanzoni waliokuwa wanapata mikopo ni wale wenye leseni. Ila kwa sasa NMB imeweka utaratibu hata kwa wale wenye maduara tu, na mikopo hii inatolewa baada ya kushirikisha ofisi ya madini. Hili jambo linakwenda kubadilisha sana sekta ya madini," amesema.
Akihitimisha kongamano hilo, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, wakiwemo benki ya NMB, imeweka mipango na mikakati ya kuboresha sekta ya madini ili kuinua uchumi wa nchi na watu wake.
Amesema mipango hiyo, pamoja na mambo mengine, inalenga kuwawezesha wachimbaji wadogo kuchimba kisasa na kwa kutumia teknolojia ili uchimbaji wao uweze kuwa na tija.
Mavunde amesema katika kipindi cha miaka minne iliyopita Serikali imeboresha sekta ya madini na kupata mafanikio mengi, ikiwemo kupandisha mchango wa sekta hiyo katika pato la taifa kutoka Sh162 bilioni mwaka 2015/16 hadi kufikia Sh960 bilioni mwezi Mei mwaka huu.