NMB yagawa madawati kwa shule tatu za jamii ya wafugaji

Muktasari:

  • Shule hizo ziko wilayani Monduli na zimegawiwa jumla ya madawati 130 yanayokwenda kutumiwa na wanafunzi 390.

Arusha. Shule tatu za msingi zilizoko kwenye jamii ya kifugaji wilayani Monduli mkaoni hapa,  zimepata jumla ya madawati 130 yanayokwenda kutumiwa na wanafunzi 390.

Madawati hayo yenye thamani ya Sh15 milioni yametolewa leo Jumatatu Aprili 15, 2024 na Benki ya NMB kwa Shule za Msingi za Sokoine na Ngarash kila moja ikipewa madawati 50 huku Orarash wakipewa madawati 30.

Akizungumza wakati wa kukabidhi madawati hayo, Meneja wa NMB Kanda ya Kaskazini, Baraka Ladislaus amesema msaada huo ni sehemu ya faida wanayoipata na sasa wanairudisha kwa jamii.

Amesema Benki ya NMB imejiwekea vipaumbele vyake katika sekta nne katika kurudisha faida kwa jamii ambazo ni pamoja na  afya, elimu, mazingira na kusaidia kurejesha au kutoa mkono wa pole kwa majanga mbalimbali yanayotokea nchini.

“Kwenye sekta ya elimu tulipokea maombi ya madawati kwa shule hizi za kifugaji tukaguswa na watoto hawa na leo tumekuja kugawa madawati haya 130 kwa shule tatu ikiwa na gharama ya zaidi ya Sh15 milioni,” amesema.

Ametoa rai kwa uongozi wa shule na wanafunzi kuyatunze madawati hayo ili yalete manufaa na wanafunzi.

“Sisi lengo letu ni kusaidia jamii na  Serikali kutimiza malengo yake kwenye sekta ya elimu kwa kupunguza baadhi ya changamoto ndogondogo zinazokwamisha ufaulu shuleni,” amesema meneja huyo.

Diwani wa Meserani, Lotha Tarakwa akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Monduli, amesema wilaya hiyo ilikuwa na upungufu wa madawati 1,214, kwa msaada huo wa NMB wa madawati 130, sasa wanaomba wadau wengine wajitokeze kusaidia kumalizia upungufu wa madawati 1,084 yaliyobakia.

Akizungumza kwa niaba ya walimu wakuu wa shule zilizopokea msaada huo, Mkuu wa Shule ya Sokoine, Abdallah Hoza amesema shule hiyo yenye wanafunzi 570 walikuwa na madawati 120 pekee na upungufu ulikuwa madawati 70, hivyo msaada huo umesaidia wanafunzi wengi kupata sehemu ya kukaa na utaongeza ufaulu kwa asilimia 60.

Amesema changamoto kubwa wanayokumbana nayo kwa sasa ni baadhi ya wazazi kushindwa kuchangia chakula cha wanafunzi, lakini pia kukataa kuwalipia nauli ya usafiri kwa wale wanaotoka mbali na kuhatarisha maisha yao kwa wanyama wakali, lakini pia mafuriko hasa kipindi hiki cha mvua.

“Mbali na hayo pia tuna changamoto kubwa ya ubovu wa barabara ya mita 600 inayoingia shuleni ambayo imejaa matope na mashimo, lakini pia tuna shida ya maji hapa shuleni, hivyo tunaomba tuvutiwe maji,” amesema Hoza.

Kwa upande wake Mbunge wa Monduli, Fredrick Lowassa ameishukuru NMB kwa msaada huo.

Hata hivyo, amesema amesikia changamoto zilizopo kama alivyoeleka Mwalimu Hoza huku akiahidi kuzifanyia kazi.

“Changamoto nimezisikia na naenda kuyafanyia kazi hasa barabara hii mbovu nimeiona lakini kwa sasa nitatoa matanki mawili ya lita 5000 kila moja, kwa ajili ya kutunza maji ya mvua mnayovuna,” amesema Lowassa.

Akipokea msaada huo, Ofisa  wa Wilaya ya Monduli, Anaeli Mbise amesema Serikali imepokea madawati ambayo yanakwenda kuwasaidia wanafunzi kujifunza kwa uhuru.