Nusu kilo maini ya swala yampeleka jela miaka 20

Nusu kilo maini ya swala yampeleka jela miaka 20

Muktasari:

  • Familia ya Bakari Abdallah, 22, ambaye Novemba mwaka jana alifungwa jela miaka 20 kwa kukutwa na nusu kilo ya nyama ya swala aliyoinunua kwa Sh1,000 iko katika machungu na haiamini kilichompata ndugu yao.

Dar es Salaam. Familia ya Bakari Abdallah, 22, ambaye Novemba mwaka jana alifungwa jela miaka 20 kwa kukutwa na nusu kilo ya nyama ya swala aliyoinunua kwa Sh1,000 iko katika machungu na haiamini kilichompata ndugu yao.

Pamoja na kuuza shamba na kufanikiwa kumtoa kwa dhamana wakati kesi ya ndugu yao aliyekamatwa Novemba 15, 2018 katika Kijiji cha Nyarutanga, Wilaya ya Morogoro ikiendelea, ndugu hao wameshindwa kulipa faini ya Sh8.8 milioni aliyoamriwa kulipa na mahakama, hivyo akaanza kutumikia adhabu mbadala ya kifungo cha miaka 20.

“Nimeumia sana. Ndugu yangu alikuwa msaada mkubwa sana katika familia yetu ambapo tumezaliwa wawili. Siamini leo hii yuko jela kwa nyama ya Sh1,000. Laiti angejua kuwa haikuwa nyama ya ng’ombe naamini asingeinunua.

“Naiomba Serikali iangalie upya kesi yake apunguziwe adhabu, tunaumia sana jamani,” anasema dada yake Bakari, Hadija Abdallah, 32.


Bakari alivyokamatwa

Siku ya tukio Hadija na mama yake walidamka mapema kwenda shambani na kumwacha Bakari nyumbani akiendelea na shughuli zake za kutengeneza simu kijijini kwao ili kujipatia kipato.

Wakati akiendelea na shughuli zake alipita mtu amebeba tenga akitangaza kuwa alikuwa anauza nyama. Bakari alimuuliza ni nyama ya aina gani na kujibiwa ilikuwa nyama ya ng’ombe.

Bila kutia shaka, Bakari alinunua nusu kilo kwa Sh1,000. Muuzaji alimpatia vipande viwili vya maini na moyo nayeye akaviweka ndani akisubiri mama yake na dada yake warudi ili wapike mboga.

Saa mbili baada ya kununua nyama hiyo, askari polisi wapatao sita walifika katika nyumba hiyo wakidai kupokea taarifa kwamba kulikuwa na nyama ya swala imefichwa ndani ya nyumba hiyo.

Askari hao waliingia ndani kufanya upekuzi na kumwacha mkubwa wao nje. Walipotoka ndani walimweleza mkuu wao kuwa hawakuona kitu. Mkuu yule hakukubali akiwaeleza kuwa alipokea simu ya uhakika kwamba kulikuwa na nyama katika nyumba hiyo.

Baada ya kusikia hivyo, Bakari akawaeleza wale askari kuwa ni kweli alikuwa amenunua nyama ya ng’ombe muda si mrefu uliopita na kwamba alikuwa ameihifadhi ndani kwenye bakuli la plastiki. Askari waliingia ndani na kuichukua nyama ile na kuondoka na Bakari.

“Tuliporejea kutoka shamba hatukumkuta Bakari nyumbani na tulipowauliza majirani walitwambia kuwa amechukuliwa na polisi na kwenda naye Kituo cha Polisi Kisaki.

“Baada ya kupata taarifa hiyo, mimi na mama tulikwenda hadi kituoni ili kujua kosa lake kwa sababu Bakari hakuwahi kuwa na tabia ya utukutu, kwanza anaumwa na muda wote alitulia kwenye shughuli zake za ufundi simu,” anasema Hadija.

Alisema baada ya kufika kituoni hapo walambiwa kuwa Bakari amenunua nyama ya swala, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.

“Tulimuuliza Bakari ilikuwaje akatueleza alivyonunua nyama ile akidhani ya ng’ombe,” anasema Hadija.

Bakari alikaa mahabusu kwa siku saba kabla ya kufikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Morogoro kujibu mashtaka la kukutwa na nyara za Serikali.

“Tulihangaika kutafuta hela kwa ajili ya kumchukulia dhamana, tuliuza shamba na tukafanikiwa kumtoa ndugu yetu kwa dhamana wakati kesi ikiendelea.

“Tukapangiwa tarehe nyingine ambapo siku hiyo Bwana Pori pia alikuwepo na akaeleza ‘ndugu yenu nimemkamata na nyama ya swala na tulipomhoji akasema hana utaalamu wa kutofautisha nyama ya swala na ile ya ng’ombe na swala ni mali ya Serikali, hivyo anatakiwa alipe faini Sh845,000,” anasema Hadija.

Anasema baada ya kutajiwa kiasi hicho cha fedha ndugu walikaa kuona namna gani wanaweza kulipa fedha hizo ikiwemo kuuza tena shamba lao. Baada ya kuhangaika huku na kule walifanikiwa kupata kiasi hicho cha fedha kilichotamkwa na Bwana Pori.

Hata hivyo, matumaini ya ndugu wa Baraka kumwona ndugu yao akiwa huru yalitoweka pale walipofika mahakamani kwa ajili ya kusikiliza hukumu huku wakiwa wamejianda kulipa faini ya Sh845,000, ndipo alipohukumiwa kulipa faini ya Sh8.8 milioni au kifungo cha miaka 20 jela.

“Kwa kweli baada ya kusikia hivyo familia ilihuzunika sana kwa kuwa hatuna uwezo wa kulipa kiasi hicho cha fedha. Wakati tunajiuliza nini cha kufanya tulishuhudia ndugu yetu aliyekuwa nje kwa dhamana akikamatwa na kupelekwa katika Gereza la Morogoro ambapo yupo huko hadi leo,” anasema Hadija.

Kwa mujibu wa Hadija, katika familia yao walizaliwa yeye na Bakari na sasa hivi anaishi yeye na mama yao baada ya baba yao kufariki.

Yaliyoendelea mahakamani

Bakari, maarufu kwa jina la Liuti Pinde alishtakiwa na kosa la kukutwa na nyara za Serikali kinyume na kifungu cha 86 (1) (2) (c) (iii) na cha (3) cha Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori ya mwaka 2009.

Sheria hiyo inatamka kuwa ni kosa la jinai kumiliki, kununua au kuuza nyara za Serikali. Swala ameainishwa kuwa nyara ya Serikali katika sheria hiyo endapo mtu ataipata bila kibali cha afisa wanyamapori.

Bakari alikana mashtaka hayo na upande wa Jamhuri uliita mashahidi watano kuthibitisha mashtaka dhidi yake. Upande wa mashtaka pia ulitoa mahakamani hapo hati ya ukamataji, taarifa ya onyo ya mshtakiwa, orodha ya vidhibiti na fomu ya uthamini wa nyama iliyokamatwa.

Ofisa wanyamapori Ramadhani Mgaya ambaye ndiye aliyekamata nyama hiyo alidai kuwa aliitambua kuwa nyama ile ilikuwa ya swala kwa kuwa yeye ni mtaalamu aliyesomea katika Chuo cha Wanyamapori Mweka.

Afisa mwingine Lamaratu Makoki aliimbia mahakama kuwa ndiye aliandaa hati ya uthamini wa nyara iliyokamatwa na kwamba nyama hiyo ilikuwa na thamani ya dola za Marekani 390 sawa na Sh845,520.

Bakari alivyojitetea

Katika utetezi wake, Bakari alidai kuwa yeye alimwona mtu akiuza nyama na kumwita na kumuuliza alikuwa akiuza nyama gani na kujibiwa kuwa ilikuwa ya ng’ombe.

Alidai kuwa alipewa vipande viwili vya maini na moyo na baadaye askari alikwenda akamkamata. Wakati akihojiwa na wakili wa Serikali, Baraka alikiri kuwa nyama ile ilikutwa ndani ya nyumba yake.

Baada ya kutiwa hatiani, Bakari aliomba apunguziwe adhabu kwa kuwa hakuwa na baba na kwamba mama yake alikuwa mzee.

Hakimu E Ushacky aliyesikiliza kesi hiyo aliridhika na ushahidi wa upande wa mashtaka akisema wamethibitisha kosa dhidi ya Bakari bila kuacha shaka na hivyo kumhukumu kulipa faini ya Sh8,845,000 au kwenda jela miaka 20. Bakati alishindwa kulipa faini hivyo akaanza kutumikia kifungo hicho.

“Mahakama hii inahitimisha kuwa mshtakiwa alikutwa na nyara za serikali na wataalamu wa wanyamapori wamethibitisha nyama ile ilikuwa ya Swala. Nimezingatia kwamba mshitakiwa ni mkosaji wa mara ya kwanza, ,” alisema hakimu Ushacky.

Imeandikwa na Asna Kaniki, Mwananchi
[email protected]