Nyadhifa alizopitia Dk Salim-3

Mbali na nyadhifa mbalimbali za kidiplomasia alizokuwa nazo, Dk Salim Ahmed Salim aliongoza wizara na idara kadhaa maarufu na za kimkakati nchini.

Aliwahi kuwa Waziri Mkuu, Waziri wa Mambo ya Nje na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Akiwa ubalozini India, mwaka 1968 aliitwa nchini kuja kuwa mkurugenzi wa kwanza wa idara mpya ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje kwa sababu ya uzoefu wake katika masuala ya kimataifa.

Aprili 1969 aliteuliwa kuwa balozi wa Tanzania nchini China na mwaka 1970 alikwenda New York, Marekani akiwa mkuu wa Ubalozi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa.

Akiwa mwakilishi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa kuanzia mwaka 1970 hadi 1980, Dk Salim alikuwa na mchango mkubwa katika kutetea haki za nchi zinazoendelea.

Ni wakati wa uongozi wa Salim katika Umoja wa Mataifa, huku Tanzania na Sri Lanka, ziliwasilisha azimio la kwanza katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (Unga) mwaka 1974 kuhusu shughuli za kijeshi katika Bahari ya Hindi.

Kutokana na rekodi bora ya Dk Salim ya utumishi katika Umoja wa Mataifa, watu wengi ndani na nje ya Tanzania walishauri kugombea nafasi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Akiwa rais wa Unga, Dk Salim alikuwa amefikia kiwango cha juu katika kazi yake katika Umoja wa Mataifa na alitamani kugombea nafasi ya katibu mkuu wa umoja huo.

Hata hivyo, Dk Salim aliamua kurejea nyumbani mwaka 1980. Kupitia madaraka yake ya urais, Mwalimu Julius Nyerere alimteua Salim kuwa mbunge na hatimaye kumteua kuwa Waziri wa Mambo ya Nje.

Tanzania ilikuwa ndiyo kwanza inapata nafuu baada ya kuingia vitani na Uganda iliyokuwa chini ya Idi Amin Dada (1978 hadi 1979).

Vita vya Kagera viliongeza msukosuko wa kiuchumi ambao Tanzania ilikabiliana nao.

Tangu mwaka 1979 nchi ilikuwa katika mvutano wa muda mrefu na Shirika la Fedha la Duniani (IMF) na Benki ya Dunia, lililoagiza Tanzania kupitisha na kutekeleza programu za marekebisho ya kimuundo.

Serikali ya Mwalimu Nyerere iliyakataa masharti hayo kwa kuwa yalikuwa tishio kwa kanuni za Azimio la Arusha na uhuru wa Tanzania.

Uamuzi huu ulizidisha hali kuwa mbaya zaidi.

Kutokana na hali hiyo, Dk Salim alijitahidi kuomba msaada kutoka Algeria, Libya, nchi za Skandinavia, Cuba, China na India na kutetea hoja za Tanzania dhidi ya masharti magumu ya Benki ya Dunia na IMF kwenye Umoja wa Mataifa na vikao vingine vya kimataifa.

Dk Salim alikuwa Waziri Mkuu wa Tanzania kuanzia Aprili 1984 hadi Novemba 1985, akimrithi Waziri Mkuu Edward Sokoine, aliyefariki dunia katika ajali ya gari barabarani.

Tanzania ilikuwa katika mtikisiko wa kiuchumi na changamoto nyingine za kijamii.

Jukumu lake moja akiwa Waziri Mkuu lilikuwa ni kuendelea na juhudi za kupambana na rushwa zilizoanzishwa na Sokoine muda mfupi kabla ya kifo chake.

Wengi walitilia shaka uwezo wake wa kukabiliana na changamoto hiyo kutokana na historia yake ya kidiplomasia. Baadhi ya watu walimpachika jina la ‘TX’, wakirejea utambulisho wa namba za gari ambazo kwa wakati huo zilikuwa zikitolewa tu kwa wageni.

Ahadi yake ya kwanza ilikuwa kutembelea mikoa na wilaya mbalimbali hasa katika maeneo ya Kigoma, Mtwara na Songea ambako athari za msukosuko wa uchumi zilionekana wazi.

Baadhi ya watu walikosa hata mavazi ya msingi. Dk Salim alijadili na Mwalimu Nyerere hali hiyo na njia ya kusonga mbele; baadaye akatafuta nguo kutoka nchi kama China na akahimiza kuchukua hatua za ukombozi ili kuondoa vikwazo vya kiuchumi visivyo vya lazima.

Ulipofanyika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 1985, muda wake wa Waziri Mkuu ukamalizika.

Kwa kutambua kazi zake katika ngazi ya kitaifa na kimataifa, Dk Salim alitunukiwa Nishani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 1985, Dk Salim alichaguliwa kuwa mbunge wa Mkoani katika Mkoa wa Kusini Pemba.

Rekodi zake kama mbunge zinaonyesha kuwa alikuwa mwakilishi madhubuti ambaye kila mara alilenga kuwatumikia watu wake.

Alipochaguliwa, hali ya kijamii na kiuchumi ya Wilaya ya Mkoani ilikuwa duni, huku huduma za afya na elimu zikiwa katika hali ya kusikitisha.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkoani District Development Fund, kulikuwa na barabara moja tu nzuri kutoka Chake Chake hadi Mkoani.

Hakukuwa na fedha za kutatua matatizo hayo na hali ya Wilaya ya Mkoani ilikuwa sawa na wilaya nyingine za Pemba.

Ili kusaidia kuboresha hali ya kijamii na kiuchumi ya watu wake, Dk Salim alichukua hatua mbalimbali za kutafuta fedha.

Alianzisha Mfuko wa Maendeleo wa Wilaya ya Mkoani, taasisi isiyo ya faida.

Dk Salim alikuwa mwenyekiti wa taasisi iliyolipia miradi mbalimbali ya maendeleo ya afya, elimu, maji na ujenzi wa barabara.

Pia, alishirikiana na Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco) ili kuhakikisha umeme unasambazwa kwa watu wengi iwezekanavyo.

Azma ya Dk Salim kuiendeleza Zanzibar haikuishia katika Wilaya ya Mkoani pekee, bali ilienea katika wilaya nyingine za Pemba.

Makatibu wa chama wa wilaya na mikoa walimtaka kutembelea maeneo yao na kujadili namna wanavyoweza kuanzisha miradi ya maendeleo.

Kuanzia mwak 1985 hadi 1989 Dk Salim alikuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa katika Serikali ya Ali Hassan Mwinyi.

Changamoto kubwa ambayo Tanzania ilikabiliana nayo ni uchumi na hatimaye Serikali mpya ikalazimika kutekeleza programu za marekebisho ya kimuundo mwaka 1986.

Akiwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Salim alihakikisha anazingatia sera ya Serikali ya Tanzania ya kutoa msaada wa kijeshi kwa Frente de Libertacao de Mocambique (FRELIMO) wa Msumbiji.

 Pia, aliendelea kufanya kazi karibu na vyama vingine vya ukombozi kama ANC na SWAPO, katika juhudi zao za kukomesha ubaguzi wa rangi na ukoloni katika nchi zao.

Kilikuwa kipindi kigumu kwa sababu uchumi wa Tanzania haukuwa mzuri na nchi nyingine za Afrika hazikuwa tayari kutoa msaada huo.

Kati ya taasisi zote alizofanya kazi, kwa mujibu wa kitabu ‘Salim Ahmed Salim: Son of Africa’ kilichohaririwa na Jakkie Cilliers, Dk Salim anakiri kufurahia zaidi kufanya kazi kama Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Alithamini weledi na nidhamu ya jeshi na anasisitiza utumishi wa Taifa ulichangia katika kuimarisha umoja, uzalendo na utangamano wa kitaifa wa Tanzania.

Anakumbuka jinsi alivyokuwa akikaa usiku katika kambi mbalimbali za jeshi, hasa Kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa ya Makutopora, mjini Dodoma alipokuwa akihudhuria mikutano ya chama na wabunge.

Alifurahia kuwasiliana na maofisa, askari wa vyeo na waajiri kutoka sehemu mbalimbali za nchi, kutoka bara na Zanzibar, wote wakifanya kazi kwa lengo moja.

Hakikisha hupitiwi na mfululizo wa simulizi hii kesho.