Nyarandu ampa tano Rais samia, ni kuhusu afya
Waziri wa zamani wa Maliasili na Utali, Lazaro Nyalandu
Muktasari:
- Waziri wa zamani wa Maliasili na Utali, Lazaro Nyalandu amesema maelekezo na miongozo ya Rais Samia Suluhu Hassan katika sekta ya afya yamesaidia kuboresha na kusogeza huduma za matibabu katika maeneo mbalimbali hasa vijijini.
Dar es Salaam. Waziri wa zamani wa Maliasili na Utali, Lazaro Nyalandu amesema maelekezo na miongozo ya Rais Samia Suluhu Hassan katika sekta ya afya yamesaidia kuboresha na kusogeza huduma za matibabu katika maeneo mbalimbali hasa vijijini.
Amesema Rais Samia ameonyesha kwa vitendo namna ya kukabiliana adui wa maradhi ndani ya Taifa.
Amefafanua kuwa kiongozi huyo mkuu wa nchi amekuwa mstari wa mbele kupigania sekta afya ndio maana wasaidizi wake wamekuwa wakitafsiri vema maelekezo na miongozo anayoitoa.
Nyalandu ambaye ni mbunge wa zamani wa Singida Kaskazini, amesema kambi ya huduma ya afya katika kijiji cha Pohama mkoani Singida iliyofanyika kwa siku (5) imekuwa msaada mkubwa kwa wananchi. Shughuli ilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel.Kambi ilihitimishwa jana Juni 19, 2023.
Mwanasiasa huyo amesema kambi hiyo imeongozwa na madaktari kutoka hospitali za Rufaa ya Singida, Mount Meru na Arusha walioshirikiana na timu ya madaktari kutoka Marekani waliokuja kupitia shirika la Stemm.
Nyalandu aliyewahi kuwa waziri katika serikali ya awamu ya nne, amesema jumla ya madaktari wazawa 16 walishiriki kutoa huduma kwa wananchi na 15 walitoka Marekani wakiwa na vifaa vya kisasa na dawa za kutosha kwa ajili ya matibabu ya wakazi waliojitokeza.
“Zaidi ya watu 2,000 wa mikoa ya Singida na Manyara walitibiwa na kupewa dawa na huduma za kitabibu bure bila malipo. Chini ya uongozi wa Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, Mganga mkuu wa mkoa na wilaya, na mkuu wa wilaya wamefanya kazi nzuri, asante sana Mama (Rais Samia),” amesema Nyalandu ambaye alikuwa mratibu wa kambi hiyo na kuongeza;
“Madaktari hawa waliokuwa wabobezi kwa kila sekta ikiwemo macho au meno na magonjwa mengine yanayowakabili wananchi. Jumla ya wagonjwa 60 walipata rufaa kwenda hospitali ya mkoa kwa matibabu Zaidi.”
Amesema lengo la kuweka kambi hiyo katika halmashauri ya wilaya Singida ni kuunga mkono jitihada za Serikali za kuwasogezea huduma wananchi kama ambavyo Rais Samia amekuwa akihimiza kwa nyakati tofauti kuhusu uboreshaji wa huduma za afya.
“Sikupata shida ya ushirikiano katika jambo hili kuanzia ngazi ya mkoa hadi kijiji, ndio maana nasema Rais Samia amegusa sekta ya afya kwa sababu maelekezo yake kwa viongozi wa chini yanatekelezwa vema namshukuru kwa maono haya,” amesema Nyalandu.
Kwa mujibu wa Nyalandu, yupo mbioni kukamilisha ujenzi wa hospitali ya kisasa ya misheni anayoijenga katika kijiji cha Pohama, akisema ikikamilika itakuwa mkombozi sio kwa wananchi wa kijiji bali hadi vijiji vya jirani.
Naibu Waziri wa Afya, Dk Mollel amewashuruku madaktari kutoka Marekani na wale wazawa kwa kuendesha kambi hiyo, akisema ni azma ya Rais Samia ya kuhakikisha huduma za afya zinafika vijijini na kuhudumia makundi yote.