Nyeusi, nyeupe bajeti za utawala wa Rais Magufuli

Muktasari:

Kasi ya Rais John Magufuli kutaka ufanisi katika utumishi wa umma ilitosha kuwajengea matumaini wananchi kuwa masuala yaliyokuwa yakiahidiwa kwenye bajeti za kisekta mwaka 2016/17, yangetekelezwa.

Dar es Salaam.  Matarajio ya wengi katika bajeti ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Tano ilikuwa ni kuona ahadi zinazoahidiwa zinatekelezwa kikamilifu.

Kasi ya Rais John Magufuli kutaka ufanisi katika utumishi wa umma ilitosha kuwajengea matumaini wananchi kuwa masuala yaliyokuwa yakiahidiwa kwenye bajeti za kisekta mwaka 2016/17, yangetekelezwa.

Isingekuwa rahisi kuamini kuwa katika Serikali inayodhibiti ukwepaji kodi, inayobana matumizi, inayosisitiza ufanisi katika utendaji kwa ‘kutumbua’ wabadhirifu wa fedha za umma na wazembe, ingekuwa na matatizo ya utekelezaji wa bajeti husika.

Hata hivyo, mambo ni tofauti. Yapo yaliyotekelezwa na mengine yamebaki kama yalivyokuwa miaka iliyopita licha ya kubadilika kwa utawala.

Miongoni mwa mambo yaliyobaki kuwa mwiba katika utekelezaji wa bajeti ni utoaji wa fedha za maendeleo zilizoahidiwa ili kutimiza ahadi za kuwaletea wananchi maendeleo.

Mwaka jana, Watanzania kwa mara ya kwanza walishuhudia fedha za miradi ya maendeleo zikifikia asilimia 40 ya Bajeti Kuu ya Sh29.5 trilioni.

Hata hivyo, hadi Februari mwaka huu ni asilimia 34 tu ya fedha za miradi ya maendeleo zilizokuwa zimeshatolewa. Hali hii inaleta picha kuwa huenda miradi mingi isitekelezwe kwa wakati kama ilivyokuwa imeahidiwa.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango aliwaeleza wabunge wakati akisoma mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa kiwango na ukomo wa bajeti ya 2017/18, kuwa hali hiyo ilisababishwa na kuchelewa kwa misaada na mikopo kutokana majadiliano na washirika wa maendeleo kuchukua muda mrefu na kupaa kwa riba ya mikopo ya kibiashara katika soko la kimataifa.

Habari zaidi soma Gazeti la Mwananchi