Nyuma ya pazia muungano wa Tanganyika, Zanzibar

Mengi yamesemwa kuhusu sababu za kufanyika kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa Tanzania. Lakini ziko sababu tano zilizofanya jambo hilo litokee. Tatu ni za muda mrefu na mbili ni za muda mfupi.

Sababu za muda mrefu ni pamoja na historia na tamaduni za watu wake, muungano na uhusiano uliokuwapo kati ya Chama cha Afro Shiraz (ASP) na Tanganyika African National Union (TANU). Sababu za muda mfupi ni mambo ya usalama na kujihusisha kwa Marekani kwenye mpango huo.

Kwa muda mrefu imejulikana kuwa wananchi wa Tanganyika na Zanzibar wana historia na utamaduni unaoshabihiana. Kwa nyakati mbalimbali watu wa Zanzibar na wale wote waishio katika mwambao wa Bahari ya Hindi kwa upande wa Tanganyika walikuwa wakitawaliwa na watawala walewale. Tangu karne ya nane hadi ya 15 walitawaliwa na Washirazi. Wakati huo miji ya mwambao ilianzishwa kutokana na kushamiri kwa biashara ya dhahabu na bidhaa nyingine.

Baadhi ya miji iliyoanzishwa kwa mtindo huo ni pamoja na Kilwa, Mombasa, Mogadishu, Lamu na Zanzibar. Lugha ya Kiswahili ilipata maendeleo ya haraka kama lugha ya biashara. Mbali na kukua kwa utamaduni wa Kiswahili, utamaduni wa Kiislamu nao ulikua kutokana na kuenea kwa Uislamu wakati huo.

Kufuatia ushindi wa watawala wa Kishirazi na Zanzibar, walirithiwa na watawala wa Kireno kuanzia karne ya 16 na 17.

Utawala wa Wareno ulijipanua katika mwambao wa Afrika ya Mashariki kuanzia Msumbji hadi kwenye pembe ya Afrika, Mombasa ikiwa ni makao makuu yake. Mwishoni mwa karne ya 17 Waarabu wa Oman, wakisaidiwa na Waswahili, waliwafukuza Wareno katika mwambao wa Afrika ya Mashariki Kaskazini mwa Mto Ruvuma.

Kwa mara nyingine utawala wa Sultan wa Oman ulijitanua katika mwambao wa Afrika ya Mashariki na Zanzibar huku ukiifanya Zanzibar kuwa makao makuu yake.

Katika karne za 18 na 19, utawala wa Sultan wa Oman, kwa kutumia biashara, ulipanuka hadi mikoani ambako vituo kadhaa vilianzishwa, ambavyo ni pamoja na Mpwapwa, Tabora, Ujiji na Katanga nchini Zaire sasa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC). Kutokana na kutanuka huko, Kiswahili nacho kilienea katika maeneo yote hayo.

Uhusiano wa historia unaofanana kati ya Tanganyika na Zanzibar uliendelea kukua hata wakati wa utawala wa kikoloni wa Uingereza. Mwaka 1890 Zanzibar iliwekwa chini ya uangalizi wa Uingereza, na miaka 28 baadaye, mwaka 1918, Tanganyika ikawa koloni la Uingereza.

Kabla ya hapo Tanganyika ilikuwa koloni la Ujerumani pamoja na Rwanda na Burundi, zote kwa pamoja zikiitwa ‘Afrika ya Mashariki ya Ujerumani’ (German East Africa).

Ilikuwa ni wakati wa utawala wa Uingereza, raia wengi wa Tanganyika walianza kuishi Zanzibar kwa sababu walikuwa wakienda huko wakati wa msimu wa kuvuna karafuu. Yote hayo yaliongeza uhusiano wa kitamaduni na kiuchumi kwa Watanganyika na Wazanzibar.

Hotuba zilizotolewa na Mwalimu Julius Nyerere, Rais wa Tanganyika na Rashidi Mfaume Kawawa, Makamu wa Rais, Aprili 25, 1964 katika Bunge la Tanganyika, zote zilisisitiza juu ya ukweli kwamba Watanganyika na Wazanzibari walikuwa na uhusiano wa karibu wa kihistoria.

Sababu nyingine ya muda mrefu iliyochochea Muungano huu ni jitihada za wakati huo za kuziunganisha nchi za Bara la Afrika. Kati ya mwaka 1950 na 1960 juhudi hizo zilikwenda sambamba na harakati za kudai uhuru na ujenzi wa Taifa.

Kuliibuka mikakati ya muungano wa bara la Afrika na kuanzishwa kwa mashirikisho ya kanda. Uhusiano kati ya ASP kama chama cha kupigania uhuru cha Zanzibar na TANU kama chama cha kupigania uhuru cha Tanganyika ulikuwa wa karibu wakati wote wa harakati za kutafuta uhuru.

Hii ilitokana na sababu mbili kubwa. Moja ni kwamba vyama vyote viwili ni matunda ya asasi za kiraia ambazo zenyewe zilikuwa na uhusiano wa kihistoria.

Wakati TANU ilizaliwa kutoka kwa Tanganyika African Association (TAA), Afro-Shirazi Party kilizaliwa kutokana na Zanzibar African Association (ZAA) ambacho kilikuwa tawi la TAA.

Sababu ya pili ni vyama vyote viwili—ASP na TANU—vilikuwa na matarajio au dhamira sawa za kuwakomboa Watanganyika na Wazanzibari kutokana na uonevu.

Haishangazi kuona kuwa Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964 yalipofanikiwa, usiku huo huo Abeid Amani Karume alikwenda Dar es Salaam ambako alionana na Mwalimu Nyerere na Kawawa saa 9 mchana kuwaambia mambo mawili:

Moja ilikuwa ni kuwaambia Nyerere na Kawawa kuwa Mapinduzi yamefanikiwa. Pili ilikuwa kuiomba Serikali ya Tanganyika iitambue Serikali mpya ya Mapinduzi mara moja .

Hali ya usalama ya Zanzibar na kwa kiwango fulani Tanganyika, zimekuwa mojawapo ya sababu za muda mfupi zilizochangia kuanzisha kwa Muungano.

Mapinduzi yalimwondoa Sultani na Serikali yake na kukimbilia Oman. Kulikuwa na hofu kwamba Sultan angeweza akakusanya majeshi na kurudi kuipindua Serikali ya Mapinduzi. Hofu hiyo iliweka usalama wa Zanzibar shakani.

Kwa Tanganyika vumbi la maasi ya jeshi katika kambi ya Colito (sasa Lugalo) lilikuwa halijatulia. Maasi ya askari ambao yalitokea miezi michache kabla ya Muungano yalileta hali ya hofu pia kwa Tanganyika. Hii ilifanya usalama wa nchi zote mbili—Tanganyika na Zanziba—kuwa katika hali yenye kutia shaka.

Kujihusisha kwa mataifa makubwa hasa Marekani, Uingereza na Ujerumani ni sababu nyingine iliyozifanya nchi hizo kuungana.

Mapinduzi hayo yalisaidiwa na Urusi, Ujerumani Mashariki (wakati huo) na China. Kwa kuzingatia vita baridi vya wakati huo, nchi za Magharibi ziliogopa kuwa Zanzibar ingeweza kuwa kituo cha nchi za Kikomunisti na hivyo, kufanya ukomunisti uenee Afrika ya Mashariki.

Ilihofiwa pia kuwa Zanzibar ingeweza kugeuzwa kuwa Cuba ya Afrika Mashariki katika Bahari ya Hindi. Kufuatia hali hiyo, inasemekana nchi za Magharibi zilikuwa na ushawishi katika mapinduzi hayo.

Hata hivyo, maelezo kuhusu kuhusika kwa nchi za Magharibi katika muungano yanasisitizwa na wale wanaodai kuwa muungano huo una baraka za mataifa mengine ya nje. Hakuna ushahidi thabiti unaoonesha ni lini na kwa namna gani nchi hizo zilishinikiza kuungana kwa Tanganyika na Zanzibar au wametumia mbinu gani kufanikisha muungano huo.

Kwa mujibu wa kitabu ‘Mwalimu: The Influence of Nyerere’ cha mwaka 1995, katika mahojiano hayo, Carlucci alisema: “Nyerere alilazimika kufanya jambo fulani kuhusiana na Zanzibar. Sijui kwa hakika kama wazo (la Muungano) lilikuwa lake mwenyewe, au kama ni sisi (Wamarekani) .

“Kama kitendo chetu cha kumsukuma afanye lolote kuhusu Zanzibar kilisababisha matokeo yoyote kwake … Natambua kuwa hali ya kisiasa ya Zanzibar ilikuwa ikizidi kuzorota. Kama Tanganyika haingefanya lolote, sehemu hiyo (Zanzibar) ingedhibitiwa moja kwa moja na Wakomunisti.”

Nyerere alidai kuwa yeye ndiye aliyetoa wazo la Muungano kwa Abeid Karume wakati alipomtembelea Dar es Salaam kuzungumza suala la kummaliza Okello kisiasa. Kulingana na maneno ya Nyerere mwenyewe, Karume alikubaliana naye mara moja kisha akapendekeza Nyerere awe Rais wa Jamhuri ya Muungano.

Ingawa Mwalimu Nyerere alisema yeye ndiye aliyempa Karume wazo la Muungano, hakusema alilipata wapi na kwa nani kabla hajakutana na Karume, wala hakusema kama alimwita Karume aje Dar es Salaam ili ampe wazo hilo au hali hiyo ilitokea tu katika mazungumzo walipokutana.

Katika salamu zake za Mwaka Mpya kwa Watanganyika/Watanzania alizotoa Januari 2, 1965, Nyerere alidokeza kuwa hata kama ASP ingeingia madarakani kwa njia ya kikatiba na wala si kwa njia mapinduzi, bado Muungano wa Tanganyika-Zanzibar ungefanyika.

Hata hivyo, “utafiti wa hivi karibuni umeonesha kwamba kulikuwa na shinikizo kubwa la nchi za Magharibi, hususan Marekani,” kwa muungano kufanyika kwa hofu kwamba ingesababisha hofu ya ukomunisti katika Afrika Mashariki.

Je, nadharia ya kwamba Muungano ulikuwa ni sehemu ya mkakati wa kufanikisha ukombozi barani Afrika na kuundwa kwa dola moja lenye nguvu ni ya kweli? Itaendelea kesho. Mfululizo wa makala haya ni sehemu ya maadhimisho ya Miaka 60 ya Muungano ambayo kilele chake kitakuwa Aprili 26, 2024.