Nyumba 145 zazingirwa na maji Lindi, 35 zabomoka

Moja ya nyumba zilizoharibiwa na mvua mkoani Lindi.

Muktasari:

Mvua hizo zimesababisha uharibifu wa makazi ya watu zikiwemo nyumba 145 kujaa maji na 35 kubomoka kabisa na watu kukosa makazi katika kitongoji cha Makangaga kilichopo katika wilayani Kilwa mkoani Lindi.

Lindi. Zaidi ya nyumba 145 zimezingirwa na maji huku nyingine 35 zikibomoka na kuharibika,  kufuatia mvua kubwa iliyonyesha mkoani Lindi kwa siku tatu mfululizo na kuleta athari kubwa katika Wilaya ya Kilwa.

Mvua hizo zimesababisha uharibifu wa makazi ya watu zikiwemo nyumba 145 kujaa maji na 35 kubomoka kabisa na watu kukosa makazi katika kitongoji cha Makangaga kilichopo katika wilayani Kilwa mkoani Lindi.

Akizungumza na Mwananchi Digital kwa njia ya simu leo Mei 6, 2024, Mwenyekiti wa kijiji cha Makangaga, Selemani Mnonya, amekiri kutokea kwa mafuriko katika kitongoji cha Makangaga na kusababisha uharibifu wa nyumba na mashamba, ambayo wameshindwa kufanya tathimini kutokana na kushindwa kupitika kwa njia za kwenda mashambani.

Amesema hali si nzuri hadi sasa ambapo bado nyumba zimezingirwa na maji na hivyo wananchi kukosa mahitaji muhimu ya kibinadamu.

“Kuna mashamba ya mpunga na vyakula vingine vimeathirika, lakini tumeshindwa kufika huko kufanya tathimini kwa sababu hakupitiki. Tunasubiria maji yatakapokata ndiyo tuende tukafanye tathimini kwenye mashamba hayo,” amesema Mnonya.

“Maji hayo yamesababishwa na kujaa kwa Mto Kiimbwi ambao unamwaga maji Makangaga na kupeleka Mto Mbwemkuru. Hakuna athari yoyote ile kwa binadamu zaidi ya nyumba kubomoka na zile ambazo maji yameingia na kutoka tumehakikisha ziko salama ndipo tumewaruhusu watu waingie na waliokosa makazi, basi tunahifadhiana,” amesema Mnonya.

Naye Sharifa Jariko, mkazi wa Makangaga ambaye nyumba yake imebomoka kutokana na mvua hizo, amesema nyumba yake imeharibika kabisa, vyakula vimechukuliwa na maji yeye na familia yake wamepata msaada kwa jirani.

“Nyumba yangu imebomoka imekaa chini kabisa hapa nimepata hifadhi kwa jirani na hata jirani mwenyewe haeleweki hatuna chakula, hatuna pa kulala, tupo tu, niko na mume wangu na mwanagu maisha yameshakuwa magumu,” amesema Sharifa.

Kwa upande wake, Saidi Mchemi amesema yeye na familia yake, kwa sasa wamehifadhiwa kwa jirani baada ya nyumba yake kubomoka.

“Tumeharibikiwa, tuliamini kwa muda huu tungekuwa tunakula vyetu lakini Mungu si Athumani, vitu vyetu vimefunikwa na maji, nyumba zimebomoka, kiufupi maisha yetu ni magumu, amesema Mchemi.

Kwa upande wake, diwani wa kata ya Kilanjelanje, Abrehemani Simba amesema kwa hatua ya kwanza waliyoifanya ni kwenda kuwatoa watu waliopo kwenye mazingira hatarishi na kukusanya taarifa ili watume wilayani.

“Katika kata yangu yote kuanzia Milumba, Kiswele, Makangaga na Mbwemkuru, kumetokea uharibifu,  lakini watu wametoka salama. Kwa kata yote, ni jumla ya nyumba kama 80 zilizoharibika.

“Kitongoji kilichopata madhara zaidi ni Makanganga, tumechukua hatua ya kwenda kuwatoa waliopo kwenye mazingira hatarishi na kuendelea kufanya tathimini ili tupeleke taarifa wilayani ambapo barabara nazo pia hazipitiki, tunachoshukuru watu wako salama, ni nyumba ndizo zimebomoka,” amesema Simba.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mohamed Nyundo amesema bado kuna wananchi wako katika maeneo ambayo hayafikiki kwa urahisi wakati wa uokoaji.

“Shida kubwa ni wale wananchi waliokwama vijijini maeneo ya uokoaji, wengi wamenasa, vijiji vingine havifikiki kabisa. Ipo timu imeenda Mtopela, wanashindwa kwenda kuokoa watu na wengine wapo kwenye maeneo ambayo maji yana nguvu, wanashindwa kwenda kuokoa wananchi,” amesema.


(Imeandikwa na Frank Said na Florence Sanawa)