Nzi wafichua mwili wa aliyefia ndani kwa siku tatu

Muktasari:

  • Mwili wa Omary Mohammed (30) aliyekuwa fundi pikipiki jijini Arusha uligundulika baada ya majirani kusikia harufu kali huku nzi wakiingia na kutoka katika upenyo wa chini wa mlango wa chumba chake.

Arusha. Mwili wa mtu mmoja mkazi wa Kata ya Sokoni One, jijini Arusha aliyefia ndani umegundulika baada ya siku tatu baada ya inzi wengi kuzingira mlango wake.

Mwili wa mtu huyo aliyefahamika kwa jina la Omary Mohammed (30), fundi pikipiki Mtaa wa Long'dong uligundulika Jumapili Novemba 19, 2023 baada ya majirani wa eneo la hilo kusikia harufu kali huku nzi wakiingia na kutoka katika upenyo wa chini wa mlango wa chumba chake.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo leo Novemba 20, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, ACP Salvas Makweli amesema kifo hicho baada ya uchunguzi umebainika ni cha kawaida.

"Askari wangu walifika eneo la tukio na kuuchukua mwili, na baada ya uchunguzi tumebaini ni kifo cha kawaida na sasa umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika hospital ya mkoa Mount Meru kwa taratibu za maziko kutoka kwa ndugu zake," amesema.

Akizungumzia kifo hicho, balozi wa shina namba 93, Bilal Bushihiri amesema mtu huyo hakuoneka kwa siku tatu lakini hakuna aliyetilia shaka hadi moja ya jirani zake walipoona inzi kutoka mlangoni kwake ndio wakapata mashaka.

"Mtu huyu ambaye alikuwa anaishi na mke na mtoto, lakini baadaye walishindwana wakaachana, huwa anaishi peke yake.

“Tangu Alhamisi hakuonekana lakini hakuna aliyepata shaka hata harufu iliyokuwa inasikika na majirani hawakushtuka wakidhani labda ni taka taka zilizonyeeshewa.

"Mshtuko zaidi ilikuja baada ya jana inzi kuonekana wakiingia na kutoka chini ya mlango wake hivyo watu kuanza kuulizana alipo na baadhi ya marafiki zake kuja na kusukuma mlango wake ambao hata hivyo haunaga kitasa na kumkuta sakafuni amefariki," amesema.

Naye Mwenyekiti wa Mtaa huo, Abraham Mkurunzi, amesema mtu huyo aliyekuwa mnywaji wa pombe kali amekutwa na mkasa huo na ilikuwa vigumu kutambulika kwa sababu alikuwa akiishi peke yake.