Ofisa Tabibu kortini Dar kwa kusafirisha dawa za kulevya

What you need to know:

  • Gema anadaiwa kukutwa na dawa hizo eneo la AREMAX Ocean road.

Dar es Salaam. Ofisa Tabibu, Gema Mmassy (37) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na shtaka la kusafirisha dawa za kulevya aina ya methamphetamine zenye uzito wa gramu 398.39.

Mshtakiwa anadaiwa kukutwa na dawa hizi eneo la AREMAX, Ocean Road Wilaya ya Ilala.

Wakili wa Serikali Neema Moshi ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa mshtakiwa anakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 10/2023.

Kabla ya kusomewa shtaka lake, Hakimu Mkazi Mkuu Amir Msumi alimwambia mshtakiwa hatakiwi kujibu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina uwezo kusikiliza kesi hiyo isipokuwa kwa kibali maalumu kutoka Kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini.

"Chini ya kifungu namba 29(3) cha Sheria ya Uhujumu uchumi, mshtakiwa hutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hii haina mamlaka ya kusikiliza shauri hili hadi Mahakama Kuu au kwa kibali Maalumu," amesema Hakimu Msumi.

Baada ya maelezo hayo, Wakili Moshi alimsomea shtaka lake mshtakiwa huyo ambapo alidia kuwa Gema anadaiwa kutenda kosa hilo Machi 22, 2023 katika eneo la AREMAX Ocean road.

Inadaiwa siku hiyo ya tukio mshtakiwa huyo alikutwa alikutwa akisafirisha dawa za kulevya aina ya methamphetamine zenye uzito wa gramu 398.39, wakati alijua kufanya hivyo ni kinyume cha Sheria.

Baada ya kusomea shtakiwa hilo, upande wa mashtaka umedai kuwa upelelezi wa shauri hilo haujakamilika hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Msumi ameahirisha kesi hiyo hadi Mei 11, 2023 itakapotajwa.

Mshtakiwa amerudishwa rumande kutokana na shtaka linalomkabili halina dhamana kwa mujibu wa sheria.