Ofisa ununuzi wa Tanesco, kortin kwa wizi wa Sh821milioni.

Muktasari:

  • Ofisa Ununuzi kutoka Shirika la Umeme nchini( Tanesco) Clemence Mlay(41) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashtaka mawili likiwemo la wizi wa Sh 821milioni akiwa mtumishi wa Tanesco.

Dar Es Salaam. Ofisa Ununuzi kutoka Shirika la Umeme nchini( Tanesco) Clemence Mlay(41) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashtaka mawili likiwemo la wizi wa Sh 821milioni akiwa mtumishi wa Tanesco.
Mlay, ambaye ni mkazi wa Yerusalem- Pangani, wiayani Kibaha Mkoa wa Pwani, alisomewa mashtaka yake leo Februari 22 na Wakili wa Serikali, Marterus Marandu, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Rashid Chaungu.
Kabla ya kusomwa kwa kesi hiyo,  Hakimu Chaungu alisema mshtakiwa hatakiwi kujibu chochote mahakamani hapo kwa kuwa kesi inayomkabili ni ya uhujumu Uchumi.
Wakili Marandu amedai kuwa mshtakiwa anakabiliwa na kesi ya Uhujumu Uchumi, namba 12/2021, ambapo kati ya Julai 2018 na Juni 2019, katika eneo la kupokea, kutunza na kutoa vifaa vya umeme lililopo  katika bohari ya Kurasini Tanesco, mshtakiwa anadaiwa kuhusika katika wizi na upotevu wa vifaa vya umeme, vikiwemo nyaya na nati, zenye thamani ya zaidi ya Sh 821.38 milioni Mali ya Tanesco.
Katika shtaka la pili, siku na maeneo hayo, mshtakiwa akiwa mtumishi wa Shirika hilo, aliisababishia hasara Tanesco ya Sh Sh 821milioni.
Upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo, haujakamilika na kwamba wanaomba  tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hakimu Chaungu aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 8, 2021 itakapotajwa na mshtakiwa amerudishwa rumande kutokana na mahakama ya Kisutu haina uwezo wa kutoa dhamana isipokuwa Mahakama Kuu pekee.