Ofisa wa Polisi kortini akidaiwa kumiliki bastola, risasi bila leseni
Mshtakiwa Fredrick Malekela ambaye ni Mkaguzi Wa Polisi (aliyevaa tisheti) akiwa chini ya ulinzi wa askari kanzu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kusomewa mashtaka yanayomkabili.
Muktasari:
- Ofisa huyo amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa mara ya pili akikabiliwa na mashtaka manane, yakiwemo ya kumiliki bastola tatu na risasi 26 bila kuwa na kibali.
Dar es Salaam. Mkaguzi wa Polisi namba PF 19931, Fredrick Malekela (45) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka manane, yakiwemo ya kumiliki bastola tatu na risasi 26 bila kuwa na leseni.
Malekela kutoka Kambi ya Polisi Kilwa Road, alifikishwa mahakama hapo Julai 31, 2025 na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali, Frank Rimoy mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini.
Hii ni mara ya pili kwa Malekela kufikishwa mahakamani hapo, Julai 28, 2025 pamoja na wenzake saba wakiwamo maofisa watano wa jeshi hilo walifikishwa mahakamani hapo na kusomewa mashtaka 16 ya kughushi vibali vya kumiliki silaha.
Wakili Rimoy alidai Malekela anakabiliwa na kesi ya Jinai namba 18577 ya mwaka 2025.
Katika kesi ya pili, Malekela ameshtakiwa peke yake.
Kati ya mashtaka hayo manane yanayomkabili Malekela, matatu ni ya kughushi, matatu ya kuwasilisha nyaraka za uongom moja la kukutwa akimiliki silaha tatu na lingine ni la kumiliki risasi bila kuwa na leseni.
Akimsomea mashtaka, Rimoy alidai katika shtaka la kughushi, mshtakiwa anadaiwa Juni 20, 2025 eneo lisilojulikana ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa nia ya kudanganya alitengeneza nyaraka ya uongo ambayo ni kibali cha kumiliki silaha chenye jina la Marwan Harbetsh akionyesha kuwa ni kibali halali, wakati akijua ni uongo.
Shtaka la pili na la tatu, anadaiwa Oktoba 30, 2024 ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa nia ya kudanganya alitengeneza kibali cha kumiliki silaha chenye jina la Ahmed Sandruddin na Muntaser Harbetsh, akionyesha ni kibali halali, wakati akijua kuwa ni uongo.
Shtaka la nne, la tano na la sita anadaiwa kuwasilisha nyaraka za uongo. Anadaiwa Julai 11, 2025 sehemu isiyofahamika ndani ya Jiji la Dar es Salaam, aliwasilisha nyaraka za uongo zenye majina ya Marwan Harbeth, Muntaser Harbetsh na Ahmed Sandruddin kwa kuonyesha kuwa ni kibali halali wakati akijua ni uongo.
Inadaiwa katika shtaka la saba kuwa, Juni 4, 2025 katika Kambi ya Polisi Kurasini, mshtakiwa alikutwa akiwa na silaha tatu aina ya bastola, bila kuwa na leseni.
Silaha hizo ni bastola aina ya CZP yenye namba D108054, aina ya Glock 26 yenye namba XSL 7694 na aina ya Glock 17 yenye namba LXE088.
Shtaka la nane anadaiwa Juni 4, 2025 eneo hilo la Kambi ya Polisi Kurasini, alikutwa akimilili risasi 26 za bastola bila kuwa na leseni.
Baada ya kusomewa mashtaka mshtakiwa alikana na upande wa mashtaka ulidai upelelezi wa kesi bado haujakamilika. Mshtakiwa alirudishwa polisi kwa ajili ya kukamilisha taratibu za kipolisi.
Hakimu Mhini aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 12, 2025 kwa ajili ya kutajwa.