Ofisa wa zamani JWTZ apigania haki miaka 30
Moshi. Mahakama Kuu ya Tanzania, masjala kuu Dar es Salaam, imekubali maombi ya kupata amri ya Mahakama ya kibali cha kuongezewa muda wa kufungua maombi ya mapitio ya uamuzi wa mwajiri kusitisha ajira, yaliyowasilishwa na askari wa zamani wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Omary Nyambu.
Mahakama Kuu imekubali ombi hilo ikiwa imepita miaka 29 tangu askari huyo afukuzwe kazi mwaka 1994.
Askari huyo wa zamani, amesota kwa miaka 17 akifuatilia jeshini ili tu wampe nyaraka zinazoonyesha sababu za kumfuta kazi bila mafanikio, hadi Mei 25, 2011 alipopata majibu rasmi akijulishwa kuwa hatapewa barua ya aina hiyo, labda kuwe na amri ya Mahakama.
Hata hivyo, akajulishwa kuwa kusitishwa kwa ajira yake baada ya kutumikia jeshi tangu 1977 ni kutokana na taarifa ya daktari iliyoonyesha kuwa alikuwa anaugua ugonjwa wa akili wa hadi asilimia 100, sababu ambazo hakukubaliana nazo.
Hivyo akaamua kufungua maombi Mahakama Kuu ya Tanzania ya kuongezewa muda (extension of time), ili aweze kufungua maombi ya kupatiwa kibali cha Mahakama ili afungue maombi ya kupitiwa upya kwa uamuzi wa kumfuta kazi.
Katika maombi yake namba 6/2023, aliwashtaki Mkuu wa Majeshi (CDF) kama mjibu maombi wa kwanza, Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, kama mjibu maombi wa pili na Mwanasheri Mkuu wa Serikali kama mjibu maombi wa tatu.
Kulingana na maelezo yaliyomo katika uamuzi huo, Nyambu alikuwa mwajiriwa wa JWTZ tangu mwaka 1977, lakini ajira yake ilisitishwa Aprili 13, 1994 alipopewa mafao yake bila kupewa nyaraka kueleza sababu za kusitishiwa ajira.
Baada ya kupita miaka 17 akipigania kupewa mawasiliano ya sababu za ajira yake kusitishwa, Mei 25, 2011 alipewa majibu rasmi kuwa hastahili kupewa barua yoyote au sababu za ajira yake kusitishwa, labda kuwe na amri ya Mahakama.
Hata hivyo, aliambiwa kuwa sababu ni kutokana na taarifa ya daktari iliyoonyesha kuwa alikuwa anaugua ugonjwa wa akili wa hadi asilimia 100, sababu ambazo hakukubaliana nazo. Hata hivyo jitihada za kupata sababu ambazo angeridhika nazo zimegonga mwamba.
Tangu apewe taarifa hizo, mwanajeshi huyo wa zamani anaeleza amekuwa katika viunga vya Mahakama akipigania haki yake kupitia kesi ya kikatiba aliyokuwa ameifungua, ambayo hata hivyo ilitupwa kutokana na dosari za kisheria.
Jaji Kagomba wakati anatoa uamuzi kuhusu suala hilo, alisema katika kesi hiyo ombi la mwombaji ni kupata amri ya Mahakama ya kibali cha kuongezewa muda wa kufungua maombi, akiomba mapitio ya uamuzi wa mwajiri kusitisha ajira yake.
Kulingana na Jaji Kagomba, muombaji kwa muda mrefu amekuwa akifuatilia kupata barua inayoeleza sababu za kusitishwa kwa ajira yake ili aweze kuomba mapitio, na pia anahoji namna mafao yake yalivyokokotolewa bila kushirikishwa.
“Ni dhahiri kupitia majibu ya kiapo cha wajibu maombi kuna upande mwingine wa hadithi. “Wakati wajibu maombi wanasema ajira yake ilisitishwa kwa sababu za kiafya, muombaji anakataa kuwahi kuwa na changamoto hiyo.
Jaji alisema muombaji amewasilisha hoja kuwa alinyimwa haki ya kusikilizwa wakati akijitetea kama sehemu ya haki alizonyimwa.
“Hoja ya kunyimwa haki ni sababu inayotosha kumpa amri ya kumuongezea muda,” alisema Jaji huyo.