Ole Sendeka alipuka bungeni akitaka ‘shingo ya mtu’

Muktasari:

  • Mbunge ametaka mawaziri ambao mashirika na taasisi zao zimetajwa wawajibike wenyewe kabla ya kuwajibishwa.

Dodoma. Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka amewataka mawaziri ambao wizara na taasisi zilizo chini yao zimetajwa katika ubadhirifu, wawajibike wenyewe.

Ole Sendeka amesema kama hawatawajibika basi bunge liondoke na kile alichokiita “shingo” ya yule ambaye wana mamlaka naye huku akiongezea kusema “wanatuchezea sana.”

Mbunge huyo ametoa kauli hiyo bunge leo Alhamisi Novemba 2, 2023 alipokuwa akichangia kwenye taarifa za Kamati za bunge kuhusu ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Mkongwe huyo ametoa kauli hiyo alipoomba kutoa taarifa wakati mbunge wa Igalula Venant Protas alipokuwa akichangia.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa taarifa mzungumzaji ambaye anachangia vizuri sana, napendekeza kuwa, mawaziri wote ambao taasisi zilizo chini yao zimetajwa, wawajibike haraka lakini wasipowajibika twendeni na shingo ya yule ambaye tuna mamlaka naye, wasituchezee,” amesema Olesendeka.

Katika mchango wake Protas amemuomba Naibu Waziri Mkuu kwenda na kalandinga (gari la polisi) akabebe watumishi wote wa kampuni ya Tan Oil isipokuwa mhudumu pekee ndiye anastahili kubaki.

Protas kwenye mchango wake amesema kuna mashaka hata katika ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambayo nayo ameomba ifanyiwe ukaguzi maalumu.

Kwa mujibu wa mbunge huyo, kwenye kesi ya Escrow kampuni ya IPTL ilichukua mabilioni ya fedha lakini Mwanasheria alisimama hadharani na kusema kuwa fedha hizo hazikuwa za Serikali lakini inashangaza muda mfupi imekuja taarifa kuwa Serikali inadaiwa.

“Hii nchi kila mtu ni mpiga dili, tumechoka kuibiwa na ofisi ya Mwanasheria Mkuu nayo ichunguzwe lakini Takukuru imekuwa ni kichaka kingine na kuchelewesha mambo,” amesema Protas.