Ole Sendeka kuzungumza kushambuliwa kwake mchana huu

Msafara wa pikipiki na magari yakielekea mji mdogo wa Orkesumet wilayani Simanjiro mkoani Manyara, ambapo mbunge wa Simanjiro Christopher Ole Sendeka atazungumza na wakazi wa eneo hilo. Picha na Joseph Lyimo

Muktasari:

  • Ole Sendeka na dereva wake Machi 29, 2024 gari lao lilishambuliwa kwa risasi walipofika eneo la Ndaleta wilayani Kiteto akielekea jimboni kwake.

Simanjiro. Mbunge wa Simanjiro mkoani Manyara, Christopher Ole Sendeka muda mfupi ujao anatarajiwa kuzungumza na wakazi wa jimbo hilo juu ya tukio la kushambuliwa risasi akiwa ndani ya gari lake.

Ole Sendeka anazungumza na wakazi wa jimbo lake leo Jumatatu Aprili mosi, 2024 siku tatu baada ya kunusurika na kifo kutokana na shambulio la risasi yeye na dereva wake Hassan, wakiwa na gari Ijumaa Machi 29, 2024.


Wakazi wa mji mdogo wa Orkesumet wilayani Simanjiro mkoani Manyara, wakiwa kwenye uwanja utakaotumiwa na mbunge wa Simanjiro Christopher Ole Sendeka kuzungumza juu ya tukio la kushambiliwa kwa risasi. Picha na Joseph Lyimo


Wawili hao wanadaiwa kushambuliwa walipofika eneo la Ndaleta wilayani Kiteto.

Akizungumza na Mwananchi Digital Machi 30, Ole Sendeka alisema anamshukuru Mungu kwa kumnusuru na tukio hilo kwa sababu risasi zilizopigwa kwenye gari hazikuwapata.

"Zilipigwa risasi za kutosha ila tunamshukuru Mungu tumenusurika hazikutupata," alisema Ole Sendeka.

Leo asubuhi akizungumza na waandishi wa habari amesema atazungumza na wakazi wa mji mdogo wa Orkesumet na maeneo mbalimbali ya Simanjiro.

Amesema pamoja na mambo mengine, ataelezea mkasa mzima wa tukio la kushambuliwa kwake.

"Alasiri ya leo nitazungumza na hadhira ya Simanjiro juu ya tukio lililonitokea ambalo japokuwa lilichukua muda mfupi wa dakika mbili, ila ilikuwa vita kubwa mno," amesema Ole Sendeka.

Msemaji wa Polisi, David Misime siku moja baada ya kutokea kwa tukio hilo, alisema timu ya watalaamu wa uchunguzi inayohusisha matumizi ya risasi kutoka makao makuu ya Polisi Dodoma,  ilitumwa kushirikiana na timu ya mkoa wa Manyara kuchunguza kwa kina tukio hilo.

Walaani tukio hilo

Akizungumza baada ya kuripotiwa kwa shambulio hilo, Mgombea ubunge wa Chadema mwaka 2020, aliyegombea na Ole Sendeka uchaguzi mkuu wa mwaka huo, Emmanuel Ole Landey alitoe pole kwa mbunge huyo na dereva wake kwa tukio baya na la kukemewa lililowapata.

"Mbegu tuliyoipanda ya wasiojulikana inapaswa kung'olewa sasa na kuiangamiza, kwani matunda yake ni sumu kwa Taifa na hayakubariki kwa namna yoyote ile," alisema Ole Landey.

Diwani wa Terrat, Jackson Ole Materi alitoa pole kwa mbunge huyo kwani ni habari mbaya kwa wana Simanjiro huku Diwani wa Emboreet, Yohana Shinini naye akitoa pole kwa tukio hilo.

Mkazi wa kata ya Naberera, Aloyce Loishiye alilaani vikali kitendo hicho na kuomba vyombo husika kuwachukulia hatua kali wote waliofanya tukio hilo.