Ombi la Somalia kujiunga EAC lasogezwa

Rais wa Rwanda Paul Kagame(kushoto) akipongezwa na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni baada ya kumkabidhi uenyekiti wa wakati wa mkutano wa 20 wa Wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), uliofanyika Arusha juzi. Kulia ni Rais John Magufuli. Picha na Filbert Rweyemamu

Muktasari:

Kuhusu mchakato wa kuanzishwa kwa shirikisho la kisiasa la nchi hizo, wakuu hao walimteua mshauri mwelekezi akayeandaa rasimu ya katiba ya shirikisho na kumtaka aikamilishe ndani ya miezi saba.

Arusha. Wakuu wa nchi za Afrika ya Mashariki (EAC), juzi walisogeza mbele hadi kikao kijacho mchakato wa Somalia kukubaliwa kujiunga na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC) kwa mara nyingine.

Somalia iliomba kujiunga na jumuiya hiyo mwaka 2013, lakini mjadala wa ombi hilo umekuwa ukisogezwa mbele kusubiri taarifa ya watalaamu ambao watakwenda Somalia kuhakiki utayari wa nchi hiyo.

Wakuu wa nchi wananchama wa EAC walioshiriki mkutano huo ni pamoja na mwenyeji wao, Rais John Magufuli, Yoweri Museveni wa Uganda, Uhuru Kenyatta wa Kenya na Paul Kagame wa Rwanda ambaye alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa jumuiya hiyo akichukua nafasi ya Museveni.

Rais wa Burundi, Pierre Nkurunzinza aliwakilishwa na Makamu wa Pili wa Rais wa nchi hiyo, Gaston Sindimwo na Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir aliwakilishwa na waziri wake wa biashara na masuala ya Afrika ya Mashariki, Paul Mayom Akec.

Akisoma maazimio ya mkutano wa 20 wa wakuu hao uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC), Katibu Mkuu wa EAC, Balozi Libérat Mfumukeko alisema wakuu hao pia wamelitaka Baraza la Mawaziri kukamilisha mchakato wa Sudan Kusini kushiriki katika masuala ya EAC.

Kuhusu mchakato wa kuanzishwa kwa shirikisho la kisiasa la nchi hizo, wakuu hao walimteua mshauri mwelekezi akayeandaa rasimu ya katiba ya shirikisho na kumtaka aikamilishe ndani ya miezi saba.

Mfumukeko alisema wakuu hao wa nchi wamelitaka Baraza la Mawaziri la EAC kuhakikisha siala hilo linafanyiwa kazi haraka na Rais Museveni atasaidia kutoa mwongozo.

Alisema imeamuliwa kwamba taarifa ya hatua zilizofikiwa katika mchakato wa kuanzishwa kwake itatolewa katika kikao kijacho cha 21 cha wakuu wa nchi hizo.

Katibu mkuu huyo alisema wakuu pia, wameipokea na kuikubali taarifa ya utekelezaji wa miradi ya Baraza la Mawaziri kuanzia Februari 23 hadi Januari 31.

Alisema wamelitaka baraza hilo kuendelea na utekelezaji wa kazi na miradi ya Jumuiya. Wakuu hao pia, wamepokea na kuridhia kwa kusaini itifaki kadhaa za Jumuiya na zile ambazo hazijafikiwa makubaliano, zitawasilishwa katika kikao kijacho.

“Marais hawa wameridhia Kenya kuwa mgombea katika Baraza la Usalama wa Umoja wa Mataifa katika nafasi ya wasio wanachama wa kudumu kati ya mwaka 2021 - 2022,” alisema katibu mkuu huyo.