Ongea na Aunt Bettie: Mapenzi, pesa na elimu vinakaribia kuivunja ndoa yangu

Ninafanya kazi nzuri na nina elimu ya juu kidogo tofauti na mume wangu. Elimu hii nimekuwa nikiiongeza kidogo kidogo kupitia programu ya ninakofanya kazi hadi kufikia ngazi ya meneja. Ila imekuwa shida kwa mume wangu, hata akifanya jambo lisilo sawa hataki niulize wala niliweke sawa, kisa nimesoma na nina pesa.

Mara zote mume wangu anaamini nina uhusiano nje ya ndoa yetu, kwa madai kuwa siwezi kukosa rafiki wa daraja langu huko nje kwa sababu siwezi kujadiliana naye mambo ya kisomi. Jambo ninalolipinga kwa nguvu zangu zote. Sijawahi si tu kutoka nje ya ndoa, bali hata kufikiria hilo. Nifanyeje?


Pole sana, nashindwa kujua mumeo akili hiyo ameitoa wapi ilihali alibariki kusoma kwako kwa nini baada ya kuhitimu amebadilika.

Hujasema kama amekuwa akikushutumu kubadilika tabia, hivyo naona kama anajitisha mwenyewe na kinyago alichokichonga. Mweleze ukweli kuwa huna baya unalolifanya zaidi ya kazi, kisha mbali an kazi hakikisha unakuwa karibu naye huku ukitimiza majukumu yako ya msingi kama mke.

Ukipata nafasi ya kuwa karibu na familia yako fanya hivyo kwa asilimia 100, usitumie muda mwingi kwa kazi za ofisini ukaisahau familia.

Mumeo anaonekana anaogopa au anawaza ipo siku utamuacha kwa sababu umeongeza daraja kazini anahisi utaungana na mabosi wenzako. Umesema hufikirii kufanya jambo baya kama mumeo anavyosema, muonyeshe hilo kwa vitendo kwa kuwa naye kila hatua ya maisha yenu.

Waswahili wanasema wasiwasi ndiyo akili, mumeo anajaribu kuwaza kwa kutanua goli, inawezekana wapo wanawake waliwaacha waume zao baada ya kupata kazi nzuri au kusoma, ndiyo maana anatumia njia ya kulaumu kukumbusha usije kumfanyia hayo. Hongera pia kwa kuwa na dhamira ya kuwa mke bora hata baada ya kuwa na nafasi nzuri kimaisha.


Ananishitakia kila jambo linalomkera


Nina uhusiano na mwanamke mrembo kwa miaka mitatu sasa, ila ana shida moja ambayo natamani unifahamishe ni kawaida au kuichoka ni kujipunja.

Anashtaki kila linalomkera au analokerwa na marafiki, jamaa na familia. Kiasi naanza kuchoka na kuna wakati anataka nichukue hatua, ikiwamo kuwauliza au kuwakanya wahusika.

Je, hii ni kawaida au mwanamke wangu amezidi, maana anachosha!

Haahahaa, usinifurahishe bwana, nakujuza leo miongoni mwa vitu wanawake wanapenda ni pamoja na kuwa na mwanamume mwenye maamuzi na anayejiamini. Ndiyo maana wanawake wengi huwapenda waigizaji mahiri wa kwenye filamu hata kama ni maadui kwa sababu ya maamuzi na ulinzi wanaoimarisha.

Sasa kukushtakia ni pamoja na kutaka kupata uhakika wa usalama wake anapokuwa pembeni yako, mjibu kwa ujanja huku ukionyesha hao wanaomkwaza ipo siku utawakabili.

Pia hakikisha unamkataza kuwa karibu nao, ataamini unamhurumia na hutaki apate changamoto yoyote, pia kama ukichunguza ukabaini kweli kuna mtu anamuonea na kuna ushahidi wa wazi wa hilo, usisite kuliweka sawa kwa utulivu na busara nyingi. Usidharau mashtaka yake inawezekana yanampa nafuu fulani. Kamwe usithubutu kumwambia apambane nao, awajibu, hakikisha unamtuliza huku ukimuahidi ipo siku utamaliza utata husika na hufurahishwi na tabia za wabaya wake. Zingatia pia katika majibu yako kuwe na nafasi ya kumkumbusha kusamehe na kusahau, mengine hayapaswi kuwekwa kifuani, yakipita yapite kwelikweli.