Ongezeko la talaka linayumbisha muhimili wa familia– 5
Muktasari:
- Hata hivyo talaka imeruhusiwa katika imani ya dini ya Kiislamu kwa mlango wa dharura, pale ambapo utulivu, mapenzi na huruma ambayo ndiyo misingi mikuu ya ndoa inapokosekana na kusababisha madhara kwa wanandoa. Tofauti na hapo inamchukiza Mwenyezi Mungu.
Dar es Salaam. Kama ambavyo simulizi hii imeonyesha namna ambavyo wanawake wanalalamika kuachwa au kutelekezwa ili wadai talaka. Aina ya talaka iitwayo kwa dini ya Kiislamu Khului, ambayo mwanamke anarudisha gharama zilizolipwa na mwanaume wakati wanaoana ili apewe talaka (ajigomboe) zimeongezeka.
Kwa mujibu wa idadi ya talaka zilizotolewa kwenye maadhimisho ya wiki ya sheria visiwani Zanzibar kwa miaka mitatu zinaonyesha mwaka 2020, talaka zilizotolewa zilikuwa 122 na zote ziliamuliwa mahakamani.
Pia, mwaka 2021, mashauri ya talaka yaliyorekodiwa yalikuwa 86 na kati ya hayo, ndoa zilizotenguliwa zilikuwa nne, Khului (talaka ya kujigomboa kwa kulipa mahari) zilikuwa 15, waliorejeshwa kwa waume zao walikuwa tisa na ndoa zilizofutwa zilikuwa 58.
Mwaka 2022 inaonyesha mashauri ya talaka yalikuwa 96 na kati ya hayo, 85 yalishaamuliwa huku 11 yakiendelea.
Ndoa zilizotenguliwa zilikuwa 10, Khului zilikuwa 23 na zilizofutwa zilikuwa 52.
Wakati Zanzibar hali ikionyesha hivyo, mkoani Mtwara takwimu zinaonyesha mashauri ya ndoa yaliyotolewa na Mahakama ya Mwanzo Mikindani hadi kufikia mwanzoni mwa Machi 2024, yalikuwa saba.
Mwaka 2023 yaliripotiwa mashauri 42 ya ndoa, mwaka 2022 kulikuwa na mashauri 47, mwaka 2021 yalikuwa 24 na mwaka 2020 yalikuwa 27.
Akizungumza na Mwananchi kuhusiana na hilo, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Mtwara Mjini, Baro Nyaki anasema wanapokea kesi hizo kila wakati.
Nyaki anasema mwaka 2023 walipokea mashauri ya ndoa 31, mwaka 2022 yalikuwa 37 na 2021 yalikuwa 40.
Hata hivyo, anasema idadi hiyo inaweza isiakisi uhalisia wa talaka zinazotolewa mkoani humo kwa sababu ndoa nyingi huvunjwa au kuvunjika na wahusika kupeana talaka bila kufika mahakamani.
“Ipo wazi kwa Waislamu sheria yao inaruhusu talaka na wengi hawana uelewa wa kuona umuhimu wa kuzisajili mahakamani,” anasema Nyaki.
Lakini anasema hata mashauri ya talaka yaliyowasilishwa mahakamani hapo, yalikuwa na sababu kuu mbili.
Anasema ya kwanza ni kutaka mgawanyo wa mali zilizochumwa ndani ya ndoa na malezi kwa maana ya huduma kwa watoto.
“Kukiwa na changamoto za namna hii ndiyo wanandoa huja mahakamani kuleta shauri lao na mwisho wa siku huishia kupeana talaka,” anasema Nyaki.
Anasema ili kuwajengea uelewa wananchi wa kuwasilisha talaka zao mahakamani kila siku asubuhi, kabla hawajaanza shughuli za kusikiliza kesi, hutoa elimu kwa wananchi waliofika mahakamani hapo.
“Pia tuna vipindi mara mbili kwa wiki kwenye redio za Ahmadia na Jamii za hapa mkoani Mtwara, huko nako huwa tunatoa elimu ya masuala ya talaka na haki za kila upande,” anasema Hakimu Nyaki.
Mwananchi lilizungumza na viongozi wa dini kutaka kujua ni kipi kifanyike ili kuweza kuiokoa jamii na janga hili la talaka.
Mratibu wa Ofisi ya Kadhi Pemba, Sheikh Said Ahmad Mohammed, anafafanua kuwa talaka inaruhusiwa katika sheria ya Kiislamu kama njia ya dharura.
Anasema, "tunapozungumza mlango wa dharura ni pahala ambapo pindi isipotoka talaka kuna madhara zaidi yanayopatikana kuliko faida katika ndoa."
Sheikh Said anaeleza kuwa talaka inaruhusiwa pale ambapo utulivu, mapenzi na huruma ambayo ndiyo misingi mikuu ya ndoa inapokosekana na kusababisha madhara kwa wanandoa.
Kwa mujibu wa Sheria ya Kiislamu, mume amepewa mamlaka ya kutoa talaka kutokana na maumbile yake ya kiasili.
Hata hivyo, mwanamke pia anaweza kujikomboa kutoka katika ndoa kupitia mfumo wa 'khului', ambapo anajikomboa kwa kutoa malipo maalumu yaliyokubaliwa na mume.
Lakini pia Sheikh Said anasema talaka inaruhusiwa lakini ni jambo ambalo halipendezi kwa Mwenyezi Mungu na linapaswa kufanywa kwa sababu za msingi pekee.
Hivyo, anasema kwa hali ya sasa, zipo sababu kadhaa za ongezeko la talaka katika jamii huku akisema moja wapo ni ukosefu wa elimu ya ndoa.
Kiongozi huyo anasema hivi sasa watu wengi huingia katika ndoa bila maarifa ya kutosha kuhusu haki na wajibu wa ndoa.
“Sababu nyingine ni ukosefu wa subira na uvumilivu, wanandoa wanashindwa kuvumiliana kutokana na tofauti zao za kijamii na kiutamaduni,” anasema Sheikh Said.
Aidha, mchango wa wazazi katika kuunga mkono au kuingilia ndoa pia unachangia migogoro ya ndoa.
Lakini pia anasema wakati mwingine wazazi hushindwa kuwa wasuluhishi wa haki na badala yake wanachukua upande wa mtoto wao, hali inayozidisha migogoro.
“Sababu nyingine ni changamoto za kiuchumi, zinaweza kusababisha migogoro katika ndoa kwa sababu matarajio ya kuboresha hali ya kiuchumi mara nyingi hayakutani na hali halisi baada ya ndoa,” anasema.
Sheikh huyo pia anagusia suala la ndoa za wake wengi, akisema ingawa Sheria ya Kiislamu inaruhusu, ni muhimu kuzingatia uadilifu na haki.
Anaonya kuwa kuoa mke zaidi ya mmoja bila kutimiza wajibu kwa mke wa awali ni kumuasi Mwenyezi Mungu.
Naye Mchungaji Samweli Maganga wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), anasema Mungu aliumba ndoa ili mwanamume na mwanamke waishi pamoja kwa upendo na amani.
Hivyo, anasema kutengana hadi kufikia hatua ya kupeana talaka, inachangia mmomonyoko wa maadili katika jamii na kusababisha watoto kukosa mapenzi na malezi ya wazazi wote.
Kutokana na hilo, Mchungaji Maganga anasisitizia umuhimu wa elimu, uvumilivu na uadilifu katika ndoa ili kupunguza ongezeko la talaka na kuimarisha misingi ya ndoa yenye furaha na amani.
Suluhisho
Mchungaji Maganga anasema familia, jamii irudi kwenye maadili na hofu ya Mungu ili kuipa heshima ndoa na kuamini ikiungwa ni mpaka kifo.
Katika hilo, Sheikh Said Ahmad Mohammed anasema kila mmoja atambue ana jukumu la kuilinda ndoa yake kwani ni mchunga na Mwenyezi Mungu amesisitiza kuliuliza hilo iwapo kuna mahali patakuwa na dosari. “Elimu ya ndoa kabla ya kuingia kwenye makubaliano hayo ya hiari ni muhimu sana.”