Tamaa ya fedha inavyochangia ongezeko la talaka - 4

Amina Abdallah Ali

Muktasari:

  • Katika sehemu ya tatu ya simulizi hii, tumemsoma Salma Hamad, mkazi wa Koani, Unguja aliyezungumzia kadhia ya kuolewa na kuachika. Pi tulimsoma Saadia Mohamed Bakari,  aliyeeleza namna alivyoolewa mara kadhaa na kuachwa, ikiwamo kupewa talaka akiwa hospitali. Endelea...

Dar es Salaam.  “Talaka zina madhara, maana watoto wanahangaika, mimi najitafuta hakuna hata mtoto mmoja anayejuliwa hali na baba yake. Je, kwa wasiokuwa na uwezo wa kuhangaika wanaishije? Nikiona hali ngumu nakwenda kutafuta maisha nje ya nchi. Tofauti na hapo, watoto wangekuwa wanateseka,” anasema Saadia.

Anasema hata nyumba anayoishi sasa ameijenga kwa fedha za mikopo ya Blac na pia, alikuwa anakwenda Muscat (Oman), huku akiwaacha watoto kwa mama yake, akirudi anaungana nao tena.

“Hivi sasa nikishindwa maisha narudi tena kwa mama, ilimradi ananilea mimi na wanangu, hivyo tunaleana,” anasema Saadia.

Bianu Ally Khamisi, ameachwa mara tano na anasema; “Nina watoto sita, wakiwamo watatu wa kiume. Nalala nao chumba kimoja, watoto hawana sare za shule, viatu wala mahitaji mengine ya shule kwa kuwa hakuna anayenisaidia miongoni mwa baba zao.”

Akizungumzia maisha ya Bianu, jirani yake Amina Abdallah Ali anasema ni magumu, kwani ana watoto sita wanaiishi nao katika chumba kimoja na kwamba hawaendi shule.

“Kutokana na uzoefu wangu hapa Pemba, haya  yanasababishwa na talaka. Hata akiolewa na nani hawezi kukaa na wale watoto. Mwanamume anaona anamuongezea mzigo.

“Mabibi wa Kipemba hawaishi kulea. Unaolewa ukipewa mimba unarudi nyumbani. Anayekuoa hataki mtoto, bibi anabaki na mtoto. Mabibi zetu, mama zetu wanateseka na watoto hawaishi kuleta wajukuu...hizi talaka zinaleta shida kwa kweli,” anasema Amina.


Wanaume wafunguka

Yunus Kombo, anasema ni kweli visiwani si jambo la ajabu kwa mwanamke kumpa mwanaume fedha akamtolee mahari kwao, ili amuoe.

“Shida ninayoiona hapa, ndoa hizi hazidumu kwa sababu mwanaume anaweza akawa hana mapenzi na huyo mwanamke, lakini akilini mwake anaamini ameolewa. Kukiwa na pesa hiyo ndoa inaweza kudumu, zisipokuwepo mwanaume hatotaka kuulizwa chochote, si inajulikana hana pesa,” anasimulia mwanaume huyo.

Hata hivyo, anasema licha ya baadhi ya wanawake kuwapatia wanaume fedha ya mahali wakatoe nyumbani kwao ili wawaoe, bado mwanamke huyo atataka ampangie masharti ya namna ya kuishi.

“Atakupangia mpaka marafiki.  Niliwekwa mpaka ndani, kisa mwanamke kanipa mahari nimuoe. Ikawa tena sina raha, nilikwenda Amani kutazama mpira, nikimueleza hasikii, kiasi nikamfokea kwa hasira kilichonikuta niliishia kulala polisi na kesi juu ya kumtishia maisha. Ndoa ilikwisha kwa mashauriano nje ya Mahakama, lakini iliniendesha sana,” anasema Kombo.

Kombo anasema haoni ubaya mwanamke kumpa pesa mwanaume kama mahari ili amuoe, ila wanandoa wakubaliane baadhi ya vitu kabla hawajafunga ndoa. Tofauti na hapo wanaoana, ili waachane maana ndoa haitadumu.

Hafidhi Machano, mkazi wa eneo la Kuukuu lililopo Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba, anasema mtazamo wake ni tofauti. Mwanamke akikulipia mahari lazima atataka kukutawala.

“Huku huwa tunaishi kwenye nyumba za wake zetu, jamaa zao, lakini likija suala la mahari bora upambane ulipe mwenyewe, ukitaka hasa kuwa mume.

“Akikulipia jiandae kuwa chini yake, ndiyo maana wanandoa wa namna hiyo hata kuachana hawaoni shida kwa sababu ni kama hawakuwa wamedhamiria. Bora ulie hali upunguziwe mahari kuliko kulipiwa yote,” anasema Machano huku akicheka.


Tamaa zinavyozaa talaka

Tofauti na wengi wanavyodhani na baadhi ya wasichana kutaka kuolewa na yeyote ili wapate uhuru wa kutoka nyumbani,  Mwananchi imebaini kuwa baadhi wanalazimika kudai talaka kutokana na maisha wanayokutana nayo kwenye ndoa.

Umury Ali Jumbe, anasema aliachana na mumewe aliyezaa naye watoto watano kwa sababu aliingia kwenye tamaa ya kuoa wake walioachwa na waume zao ili warudiwe.

“Nimeishi naye miaka tisa, tumejenga kibanda chetu, nikifanya biashara naye vibarua vya hapa na pale, lakini miaka miwili hii ya karibuni tabia yake imebadilika sana,” anasimulia Umury.

Anasema mumewe alikuwa hachelewi kurudi nyumbani, akaanza kuchelewa, mara harudi kabisa hata siku mbili, akimuuliza majibu yake hayana mashiko.

“Nikawa navumilia kwa sababu nina watoto watano, wawili wadogo niliwazaa kwa kupishana miezi 11, hivyo sikuwa na nyendo, lakini nikapata taarifa kuwa ameoa. Sikuitilia maanani. Kuna wakati akawa kama zamani, ikawa hiyo hali inajirudia, mara anabadilika, mara anakuwa sawa.

“Taarifa za kuoa zikawa zinakuja kila mara. Nikiambiwa ameoa sehemu tofauti nikawa najiuliza inakuwaje anaoa huku na huko na wake wameshazidi wanne tangu nimeanza kusikia. Nikaamua kufuatilia,  ukiwa ni mwaka wa pili tangu aanze hizo tabia zake,” anasema.

Hata hivyo, anasema alichokuja kukigundua na baadaye kuthibitishiwa na mumewe huyo, kwamba amekuwa msitiri wa wanaume walioacha wake zao na kutaka kuwarudia.

 “Yaani mume wangu anapewa fedha za mahari na mwanamke, anakwenda kutoa kwa huyo mwanamke aliyeachika, anamuoa kwa muda kisha anamuacha, ili arudiane na mumewe wa awali kwa mujibu wa dini.

“Kwa hiyo hapo anapewa pesa mara mbili. Hapa ina maana anapewa mahari ya kwenda kuoa, ananunuliwa nguo na shengesha nyingine, kisha analipwa pesa ya ujira kwa kuoa kisha kuacha,” anasema mama huyo.

Anasema alipombana, alikiri ni kweli na huu ulikuwa mwaka wa pili anafanya hivyo, lakini huwa anabadilika kwa sababu kuna anaowapenda na kuwaacha inakuwa ngumu kwake, hivyo huwa analazimika kulala hukohuko walipo.

Anasema madhara ya hiyo hali alikuwa anaswali akaacha na akaanza kunywa pombe. “Nilipomuuliza akasema kuna wanawake anawaoa ili apate pesa, hivyo ili awe nao kutimiza ada ya ndoa inabidi awe amekunywa maana moyo wake unakuwa hautaki.

“Akikuhadithia unaweza kucheka huku unalia maana ameamua kuwa mtumwa. Katika kuhangaika kuna ambaye amempa mimba ambayo mpaka sasa inamletea shida, baada ya kumuacha na kuolewa na mume aliyemuacha mwanzo na kubainika ana mimba.”

Kukomolewa kwenye fidia ya talaka

Umury anasema alidai talaka baada ya kuona anamuweka hatarini kupata maradhi, kwani ndani ya miaka miwili amepata hilo analoliita dili mara saba.

“Niliachika kwa kumlipa mahari aliyoniolea, licha ya kuishi na kuzaa naye watoto...mwanaume akikuchoka anakufanyia visa, ukishindwa utadai talaka. Atakuzungusha mpaka utakwenda kwa kadhi kuidai kisheria. Huko ndiko atakapokubana umlipe, kwani sheria inaeleza hivyo. Nilimlipa na nikamalizana naye,” anasema.

Hilo linaungwa mkono na Hanifa Hamad Hafidh, anayesema aliyekuwa mumewe alimkomoa kwa kudai fidia kubwa baada ya kudai talaka.

“Kweli sheria inasema nimlipe kulingana na tulivyokubaliana, lakini alinioa kwa mahari ya Sh300,000, kitanda na godoro. Nilipodai talaka baada ya kutelekezwa bila huduma na watoto wawili, alidai nimlipe Sh700,000 kama ninataka talaka na kitanda na godoro jipya. Ilhali lile aliloninunulia tulilalia sote, jamaa zangu kwa sababu ya mateso niliyokuwa nikipitia walichanga wakampa ili aniache,” anasema.

Anasema ni kama wanaume wameingiwa na shetani, kwani aliolewa tena na akaishi kwenye ndoa  miaka mitatu, akamuacha bila kosa.

“Aliamka tu kama mlevi akasema sikutaki na ninakuacha uende kwenu. Akanisindikiza akaniacha nje ya nyumba, akaondoka zake. Kesho yake nikaletewa talaka,” anasimulia Hanifaa.


Makala haya yameandikwa kwa ufadhili wa Bill & Melinda Gates Foundation.

Itaendelea kesho