Onyo la mwisho la Rais Samia

Onyo la mwisho la Rais Samia

Muktasari:

Rais Samia Suluhu Hassan, juzi alitoa onyo la mwisho kwa Waziri wa Mifugo Mashimba Ndaki kwa kushindwa kutekeleza agizo lake la kuziendesha ranchi za Taifa kibiashara, kwa kuwatumia vijana waliohitimu taaluma za kilimo na ufugaji ili kuongeza uzalishaji wa nyama nchini.



Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan, juzi alitoa onyo la mwisho kwa Waziri wa Mifugo Mashimba Ndaki kwa kushindwa kutekeleza agizo lake la kuziendesha ranchi za Taifa kibiashara, kwa kuwatumia vijana waliohitimu taaluma za kilimo na ufugaji ili kuongeza uzalishaji wa nyama nchini.

Onyo hilo alilitoa wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya wakulima yaliyofanyika kitaifa jijini Mbeya. Pamoja na kuzungumzia masuala kadhaa ya kilimo, aligusia pia sekta ya ufugaji.

Rais Samia alisema kwa eneo la malisho ya mifugo ambayo Tanzania inalo, inapaswa kuongoza kwenye biashara ya mazao ya ufugaji barani Afrika.

Alisema Tanzania ina jumla ya ranchi 14 na kama zitatumika vizuri, zinaweza kuifanya nchi kuwa kinara wa biashara ya mazao ya mifugo barani Afrika, ila changamoto kubwa iliyopo ni kutotumika kwa rasilimali hizo.

“Kama ilivyo kwenye sekta ya kilimo, sekta ya mifugo ilipata fedha za Uviko- 19 na nilitegemea zingetumika kutengeneza mashamba ya mifugo kwenye ranchi tulizo nazo na tukaweka vijana humo washughulike na ufugaji.

“Kuna vijana wengi wamemaliza SUA (Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo) kwenye taaluma ya kilimo na ufugaji, lakini wanahangaika mitaani kutafuta ajira. Njia pekee ya kutoa ajira kubwa ni kuwatumia vijana hawa kwenye hivyo vitalu kwenye ranchi za Taifa na kuwasimamia vizuri, lakini hili halijafanyika, waziri nilishalisema hili mara mbili sitalirudia na nilisema mshirikiane na SUA sitarudia,’’ alisema Rais kwa msisitizo.


Anusa ufisadi

Rais Samia pia alionyesha kunusa harufu ya ufisadi katika kampuni ya ranchi za Taifa akieleza kubaini eneo kubwa la ranchi kukatwa vitalu na kukodishwa huku mapato kutokana na biashara hiyo yakiishia mifukoni mwa watu.

Alisema taarifa alizonazo, ranchi 14 zilizo chini ya Narco kuna mifugo 155,554, mifugo 22,842 pekee ndiyo mali ya kampuni hiyo huku iliyosalia ikiwa ni mali ya watu binafsi.

“Hii ni sawa na asilimia 15 ya mifugo yote iliyopo kwenye ranchi za Narco; kiukweli hali ni mbaya na ni wazi kampuni imeshindwa kutimiza malengo ya kuanzishwa kwake. Ranchi nyingi zimekatwa vitalu na kukodishwa, Serikali haipati manufaa na huo ukodishaji,” alisema Rais.

Kufuatia hilo, aliielekeza bodi ya wakurugenzi na uongozi wa Narco kufanya uchambuzi wa vitalu vyote vilivyokatwa na kukodishwa na kutoa takwimu za mapato kutokana na ukodishaji huo.

“Tunataka tuone ukodishaji ule umeingiza mapato kiasi gani serikalini au kwa hao Narco wenyewe. Naagiza pia kuangaliwa upya ukataji wa vitalu, ikibidi kufuta vitalu vyote na kupanga upya matumizi bora ya ranchi hizo kwa kufanya uwekezaji wa maana. Ranchi hizi zingeweza kujiendesha zina thamani kubwa sana zingeweza kutumika kama dhamana wakapata fedha benki wakaweza kujiendesha, hawafanyi hivyo wamejikita kwenye kukata vitalu kwa ajili ya maslahi yao binafsi,” alisema na kuongeza;

“Tunazunguka huko duniani tukisema tuna ranchi ambazo tuko tayari kuingia ubia na wawekezaji, lakini ukilishusha hilo chini hauoni hata ranchi moja ikiwa tayari kwa uwekezaji wa ubia. Hii ni kwa sababu ranchi zote zimekatwa vitalu na watu wanalinda maslahi yao,”.

“Watu wa Narco na wizara, nitaanza kuwashughulikia halafu nyinyi mshughulikie vitalu nataka vifutwe tuanze ufugaji wa kibiashara, vijana waingie kwenye biashara hiyo maana kuna masoko ya kutosha ya kupeleka nyama lakini hatuwezi kukidhi mahitaji ya soko kwa kuwa hatuna rasilimali,”.


Azindua mpango wa ruzuku ya mbolea

Katika maadhimisho hayo Rais Samia alizindua Mpango wa Ruzuku ya Mbolea inayowawezesha wakulima kupata nafuu ya bei za mbolea katika msimu wa kilimo 2022/2023.

Akizungumzia mpango huo aliwataka wakulima kuitumia fursa hiyo kufanya kilimo chenye tija ili kupata mazao mengi ambayo yatatumika kwa chakula na biashara.

“Wakati Serikali inatenga fedha kwa ajili ya kutoa ruzuku niwaombe mlime kibiashara tupate chakula cha kutosha na cha kuuza nje, ili fedha itakayopatikana tuitumie kuanzisha mfuko wa maendeleo ya kilimo ili kuweza kusaidia pale inapotokea bei za mbolea na pembejeo kupanda.

“Msisahau pia kulipa tozo zinazotakiwa kulipwa ili tuweze kuunda mfuko huu, si kila mwaka tutatoa fedha za ruzuku hili limefanyika mwaka huu kukabiliana na changamoto ambazo zimejitokeza na kusababisha bei ya mbolea kupanda huko duniani,”.

Alitumia fursa hiyo kuwataka viongozi wa mikoa, wilaya, kata na vijiji kusimamia kwa ukamilifu usajili wa wakulima ili waweze kutambuliwa na mfumo huo wa ruzuku huku akieleza wizara kuratibu kwa ufanisi mchakato huo.

“Hii kazi ya ruzuku iweze kwenda vizuri naelekeza mifuko yote ya mbolea iwe na alama ya utambuzi, kuhakikisha kila kampuni iliyosajiliwa kusambaza mbolea ya ruzuku ina tangaza mawakala wake kila mkoa na wilaya.

Wizara ya kilimo na wizara ya fedha zihakikishe fedha za ruzuku zinatolewa kwa wakati, ili wakulima wapate pembejeo kuendena na misimu. Pia viongozi wa mikoa, wilaya, kata, vijiji wasimamie kwa ukamilifu usajili wa wakulima watakaopata,”

Waziri wa Kilimo Hussen Bashe alisema mpango huo unalenga kuwaondolea mzigo wakulima ambao wamekuwa wakikutana nao kwa muda mrefu kutokana na changamoto za bei za mbolea.

Mpango huo wa rukuzu unafanya bei ya mbolea ya DAP kuuzwa Sh70,000 kutoka Sh 131,000 ya awali huku mbOlea ya Urea ikiuzwa Sh70,000 kutoka Sh124,734.

Kupitia mpango huo mbolea zote za kupandia zinazofahamika kama NPK zilizokuwa zikiuzwa kwa Sh122,695 zitauzwa kwa Sh70000 huku ruzuku ya Serikali ikiwa Sh 52,695.

Katika kilele hicho Rais Samia alishuhudia utiaji saini wa mikataba 21 ya utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji, ambayo lengo lake ni kuchangamsha kilimo cha umwagiliaji ili kiwe na tija na kuwaondoa wakulima kwenye utegemezi wa mvua.


Kauli ya CCM, mawaziri

Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo aliipongeza Serikali kwa kufungua mfumo wa ruzuku ya pembejeo za kilimo hasa mbolea, akidai utaenda kumpunguzia mkulima gharama.

Alisema kutokana na mfumo huo, wakulima watalima bila kuwa na mzigo mkubwa wa gharama ya pembejeo za kilimo ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2000/2025 inayotaka ifikapo mwaka 2030, kilimo kichangie uchumi wa nchi kwa asilimia 10.

Chongolo aliyasema hayo jana wakati akizungumza katika Sherehe za Nanenane zilizofanyika katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.

“Umepokea nchi na muda huo tukaingia kwenye changamoto ya vita ya Ukrainna Urusi, lakini kukawa na changamoto ya corona, lakini wewe hukulala ukajikita kutafuta suluhisho badala ya kuhangaika kuhuzunika alisema Chongolo na kuongeza:

“Zaidi ya Sh150 bilioni za Kitanzania na Dola milioni 77 za Marekani umezipeleka kuhakikisha zinachangia kupunguza mzigo wa pembejeo hasa mbolea.’’

Alisema hayo ndiyo mapinduzi ya kweli ya kilimo yenye dhamira ya kulitoa Taifa lilipo na kwenda mbele ili kufikia ajenda ya 10/30.

Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba, alisema ruzuku ziliwahi kutolewa miaka ya nyuma, lakini zilikuwa na ‘upigaji’ mwingi kwa watu kusainishana huku fedha zikienda kwa wachache.

“Mnaona bei inashuka kutoka kiasi gani Serikali imeweka na kiasi gani fedha hiyo ananufaika anayelima; haya yote Watanzania lazima tumuunge mkono Rais kwa vitendo,” alisema.

Alisema ilishatokea shughuli za uzalishaji kuwa kama ngoma za asili zikichezwa na wastaafu, akimaanisha waliokuwa wanafanya kilimo ni wazee huku vijana wakisubiri ajira.

“Niwaambie nchi zote zilizoendelea na zote ambazo pato la mtu mmoja mmoja limeongezeka na ni kubwa, ni zile ambazo vijana ni nguvu kazi iliyo kazini,” alisema.

Alisema bajeti peke yake haiwezi kufanya kazi na kuleta matunda kwenye Taifa kama wananchi hawataamua kufanya kazi.

Naye, Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Innocent Bashungwa, alisema ofisi yake ipo tayari kushirikiana na Wizara ya Kilimo katika kuhakikisha wanafanikisha ajenda ya kilimo ya 10/30.

“Tutajipanga vyema na wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya, kusimamia vyema mabilioni haya ambayo Rais ameyatua kwa wakulima kuwapunguzia gharama za maisha ili wafanye uzalishaji mkubwa,” alisema.

Waziri huyo alisema wataenda kusimamia vyema mfuko wa ruzuku wa pembejeo ili uende kufanya kazi iliyokusudiwa.

Aliwaelekeza wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa halmashauri, kuhakikisha pikipiki na vipima udongo vinatumika kama ilivyokusudiwa.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki alisema japo mifugo na uvuvi ni miongoni na sekta muhimu katika kuondoa umaskini, bado mchango wake katika kukuza uchumi ni mdogo.

Alisema kutokana na hali hiyo Serikali imefanikiwa kuongeza bajeti kwenye wizara hiyo ili isaidie kukuza pato la nchi.Alisema moja ya mambo ambayo wataendelea kufanya ili sekta hiyo iwe na mchango mkubwa kwenye pato la Taifa ni kujenga majosho, kununua dawa za kuogoshea mifugo, kujenga miundombinu ya mialo na masoko. “Tutaendelea kufanya mambo mengi ambayo yanatoa ajira kwa vijana wetu,” alisema.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Dk Christine Ishengoma, alisema wakulima walikuwa wanateseka kutokana na bei ya mbolea kuwa kubwa.

Alisema bei ya mbolea ilikuwa juu kiasi kwamba wakulima walikuwa wanashindwa kufanya kilimo chenye tija.


Vodacom yafungua fursa

Mkurugenzi mtendaji wa huduma za kidijitali na ziada za kampuni ya Vodacom Tanzania, Mbugu Kamando, alisema wamefungua fursa ya teknolojia mpya kwa wakulima kutumia simu za mkononi kujua hali ya hewa na masoko katika misimu ya kilimo kupitia huduma iitwayo M- Mkulima .

Kamando alisema licha ya huduma hizo pia wanawaunganisha wakulima na mfumo wa afya kiganjani, lengo likiwa ni kuunga mkono sekta ya kilimo

“Ilikumbwe kuwa hivi karibuni tulizindua huduma ya Farm clinic kwa kushirikiana na Kampuni ya Mwananchi Communications (Ltd), lengo ni kuiongoza Tanzania kwa vijana kwenda kwenye ulimwengu wa kidijital katika sekta ya kilimo na upatikanaji wa masoko,” alisema.

Alisema katika kutoa huduma ya M - Mkulima wamewafikia wakulima zaidi ya 165,000 na kuhakikisha wanapata ruzuku na dondoo za afya wakiwa shambani.

‘’Leo mmeshuhudia Rais Samia akizindua mfumo wa upatikanaji wa pembejeo za kilimo kwa wakulima kwa mfumo maalum. Sisi kama taasisi ya kifedha tunawakopesha wakulima kupitia Vodacom M pesa au Songesha,” alisema.

Kamando alisema Vodacom wakiwa wadau muhimu, wanaendelea kubadilisha maisha ya Watanzania kwenye ulimwengu wa kidijitali, ndio maana wanashirikiana na Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL), kwa lengo la kufikia ajenda ya 10/30 katika sekta ya kilimo.

Nyongeza na Hawa Mathias