Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Operesheni kali kuondoa ajira za watoto migodini-3

Muktasari:

  • Mamlaka za ukaguzi zinatarajiwa kuanza operesheni katika maeneo ya uchimbaji madini yasiyosajiliwa, ambako watoto mara nyingi hukutwa wakifanya kazi hatarishi.



Dar es Salaam. Serikali imeongeza juhudi za kuzuia watoto kufanya kazi katika maeneo ya migodi kwa kutangaza operesheni mpya dhidi ya shughuli za uchimbaji madini zisizo rasmi, ambako ajira hizo zimekuwa zikijitokeza kwa kiwango kikubwa.

Hatua hiyo inakuja wakati mamlaka zikiongeza juhudi za kuhakikisha kila mtoto anakuwa shuleni.

Mamlaka za ukaguzi zinatarajiwa kuanza operesheni katika maeneo ya uchimbaji madini yasiyosajiliwa, ambako watoto mara nyingi hukutwa wakifanya kazi hatarishi.

Hatua hiyo inafuatia msimamo wa Serikali kwamba hakuna mtoto anayepaswa kufanya kazi migodini kwa mazingira yoyote.

Naibu Waziri wa Madini, Dk Steven Kiruswa anasema shughuli zote za uchimbaji madini zinapaswa kusajiliwa na kufuatiliwa kupitia mifumo ya Serikali, ikiwamo mashimo binafsi ya uchimbaji.

Anasema waendeshaji waliosajiliwa hukaguliwa mara kwa mara ili kuhakikisha wanazingatia sheria za kazi na usalama.

“Watoto hawaruhusiwi kufanya kazi migodini. Pale ambapo ukiukwaji wa sheria unagundulika, hatua kali huchukuliwa,” anasema.

Dk Kiruswa anasema matukio mengi ya ajira za watoto yanahusishwa na shughuli za uchimbaji madini zisizosajiliwa.

Anasema mamlaka zitafuta leseni za waendeshaji waliosajiliwa watakaobainika kukiuka sheria, huku waendeshaji haramu wakiondolewa na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Wakati huohuo, maofisa elimu katika Mkoa wa Geita wanaongeza juhudi za kuhakikisha watoto wote wanaingizwa katika mfumo wa elimu, wakieleza kuwa hiyo ni hatua muhimu katika kupambana na ajira za watoto.

Usimamizi hafifu pamoja na utekelezaji dhaifu wa Kifungu cha 5(1) cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, Sura ya 366 (Toleo lililorekebishwa la 2023), unachangia kuongezeka kwa ajira za watoto katika migodi ikiwamo ya mkoani Geita.

Watoto wenye umri wa miaka 10 hadi 15 wanaacha shule na kunyimwa haki yao ya elimu pamoja na maisha bora.

Tanzania ina mfumo imara wa kisheria wa kulinda haki za watoto ukiwamo Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, Sura ya 366, na Sheria ya Mtoto, Sura ya 13 (Toleo lililorekebishwa la 2023), ambazo zote zinakataza watoto walio chini ya miaka 18 kufanya kazi hatarishi kama uchimbaji madini.

Mbali na hayo, Kifungu cha 6.2 cha Sera ya Madini ya mwaka 2009 kinaelekeza Serikali kusimamia kanuni kali dhidi ya ajira za watoto ili kulinda ustawi wao na kuzuia watoto kuingia katika maeneo ya uzalishaji wa madini.


Nini kinafanyika

Ofisa Elimu Mkoa wa Geita, Antony Mtweve, anasema Serikali za mitaa na vijiji zimeelekezwa kuwabaini na kuwaandikisha watoto wote wenye umri wa kwenda shule, akisisitiza kuwa elimu bila ada imeondoa vikwazo vikubwa vya upatikanaji wa elimu.

“Hii ni fursa ya kipekee. Serikali tayari imepunguza mzigo wa kifedha kwa familia kwa kuondoa ada za shule. Kinachohitajika sasa ni ufuatiliaji wa karibu kuhakikisha kila mtoto anayeanza shule anamaliza elimu yake,” anasema.

Mtweve anasema ujenzi wa mabweni katika shule za msingi na sekondari ni muhimu ili kusaidia wanafunzi kuendelea na masomo, hasa wale wanaotoka katika mazingira magumu.

Takwimu za mkoa zinaonesha maendeleo tofauti katika uandikishaji wa elimu ya awali.

Wilaya ya Nyang’wale inaongoza kwa asilimia 96 ya uandikishaji, huku halmashauri nyingine zikiwamo Bukombe, Chato na Manispaa ya Geita zikiwa kati ya asilimia 70 na 75.

Hata hivyo, uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la kwanza umefikia asilimia 99, watoto 112,372 kati ya 114,021 waliostahili kuandikishwa tayari wameandikishwa.

Licha ya mafanikio hayo, anasema changamoto bado zipo, akieleza kuwa sababu za watoto kuacha shule ni nyingi, ikiwamo mazingira yasiyo tulivu ya kifamilia, ukosefu wa chakula shuleni na uhamaji unaotokana na shughuli za kiuchumi kama vile uchimbaji madini na uvuvi.

Anasema katika matukio mengi wazazi huhama kutafuta kipato na kuwaacha watoto bila usimamizi wa kutosha.

“Kuna watoto wanaoishi peke yao au katika mazingira magumu. Tunawabaini na kuwapeleka katika shule za bweni pale inapowezekana,” anasema Mtweve.

Anaeleza kuwa, programu za chakula shuleni zinaendelezwa ili kupunguza utoro, huku jamii zikielimishwa kuhusu umuhimu wa elimu.

Ajira za watoto katika shughuli za uchimbaji madini kama kubeba mawe na maji zimepigwa marufuku kitaifa na kimataifa, ikiwamo na Shirika la Kazi Duniani (ILO).

Hata hivyo, utekelezaji wa sheria bado ni changamoto kwa kuwa baadhi ya shughuli hizo hufanyika kwa siri.

“Mchana unaweza usiwaone, lakini jioni wanaenda kufanya kazi,” anasema Mtweve akieleza ugumu wa kubaini matukio hayo.

Anasisitiza kuwa jukumu la wazazi ni muhimu katika kutatua tatizo hilo.

“Iwapo wazazi hawatachukua wajibu wao, watoto huachwa wajitafutie maisha wenyewe. Umaskini pekee hauwezi kuwa sababu ya hali hii; maeneo mengi yanakabiliwa na changamoto kama hizi lakini watoto bado wanahudhuria shule,” anasema.

Diwani wa Lwamgasa, Daniel Mabala, anasema jamii zinapaswa kubadili mtazamo unaohalalisha ajira za watoto.

Anasema baadhi ya mila na mitazamo bado huwachukulia vijana walio nje ya mfumo wa elimu kama watu wazima wanaopaswa kujitafutia kipato.

“Watoto hawaruhusiwi kushiriki katika shughuli za kujipatia kipato. Lazima tuendelee kuielimisha jamii ili kuelewa kuwa elimu ni muhimu kwa maisha na ustawi wa mtoto,” anasema.

Wadau mbalimbali wa maendeleo wanaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kusaidia miundombinu ya shule, vifaa vya kujifunzia, baiskeli na sare za shule, hususani kwa watoto walio katika mazingira magumu na wenye mahitaji maalumu.

Anasema ushirikiano endelevu kati ya Serikali, jamii na wadau mbalimbali utakuwa muhimu katika kutokomeza ajira za watoto na kuhakikisha kila mtoto si tu anaandikishwa shule bali pia anamaliza elimu yake.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Lwamgasa, Amos Mwita anasema ingawa watoto wengi walioandikishwa mwaka huu wameripoti shuleni, bado wanafunzi takribani 60 hawajulikani walipo na juhudi za kuwatafuta zinaendelea.

“Watoto wote waliotarajiwa kuanza kidato cha kwanza mwaka huu wameripoti shuleni isipokuwa takribani 60 ambao hatujui walipo. Tunaendelea kuwafuatilia ili kujua waliko,” anasema.

Anawataka wananchi kusaidia kuwabaini watoto wanaopaswa kuwa shuleni lakini wanaonekana wakizurura mitaani.

“Kama ukimkuta mtoto mitaani, mtoe taarifa kwa kiongozi wa kijiji ili hatua zichukuliwe kubaini anatoka wapi na alipaswa kuwa shule gani,” anasema.

Mwita anasema viongozi wa kijiji wameweka hatua kali za kuhakikisha wanafunzi wanahudhuria masomo.

“Mzazi ambaye mtoto wake haendi shule anaweza kuchukuliwa hatua za kinidhamu ikiwamo kulipa mfuko wa saruji. Tunatoza mfuko wa saruji kama adhabu ili kuwepo hofu ya adhabu. Saruji hiyo hutumika katika miradi ya maendeleo ya kijiji,” anasema.

Anasema viongozi wa eneo hilo huingilia kati pale walezi, hususani wazee wanaolea wajukuu, wanaposhindwa kuhakikisha watoto wanakwenda shule.

“Kama babu au bibi analea wajukuu na wazazi wako mbali, na mzee huyo hawezi kuwapeleka shule, sisi tunaingilia kati. Wakati mwingine mtoto mwenyewe anakataa kwenda shule; tukibaini hali hiyo tunachukua hatua,” anasema.