Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Uchimbaji madini kichocheo kwa wanafunzi kuacha shule -2

Muktasari:

  • Baadhi ya watoto wenye miaka 12 hadi 15 hubeba magunia ya mawe yaliyosagwa kutoka eneo moja kwenda jingine kwa malipo ya Sh5,000



Geita. Katika Kijiji cha Lwamgasa, mkoani Geita, takribani watoto 60 waliokuwa wanatarajiwa kuanza kidato cha kwanza mwaka huu hawajulikani walipo, hali inayozua hofu kwa walimu na viongozi wa eneo hilo.

Licha ya kuwapo kwa hatua kali za kuhakikisha wanafunzi wanahudhuria masomo, mvuto wa shughuli za uchimbaji madini zilizo karibu unaonekana kuwa mkubwa kuliko wito wa kwenda shule, jambo linalotishia mustakabali wa wanafunzi hao na juhudi za jamii za kuhakikisha watoto wanapata elimu.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Lwamgasa, Amos Mwita anasema ingawa watoto wengi walioandikishwa mwaka huu wameripoti shuleni, bado wanafunzi takribani 60 hawajulikani walipo na juhudi za kuwatafuta zinaendelea.

“Watoto wote waliotarajiwa kuanza kidato cha kwanza mwaka huu wameripoti shuleni isipokuwa takribani 60 ambao hatujui walipo. Tunaendelea kuwafuatilia ili kujua waliko,” anasema.

Mwita anatoa wito kwa wananchi kusaidia kuwabaini watoto wanaopaswa kuwa shuleni lakini wanaonekana wakizurura kijijini.

“Kama ukimkuta mtoto mitaani, mtoe taarifa kwa kiongozi wa kijiji ili hatua zichukuliwe kubaini anatoka wapi na alipaswa kuwa shule gani,” anasema.

Anasema viongozi wa kijiji wameweka hatua kali za kuhakikisha watoto wanahudhuria shule.

“Mzazi ambaye mtoto wake haendi shule anaweza kuchukuliwa hatua za kinidhamu ikiwamo kulipa mfuko mmoja wa saruji. Tunatoza mfuko mmoja wa saruji kama adhabu ili kuwepo hofu ya kuchukuliwa hatua. Saruji hiyo hutumika katika miradi ya maendeleo ya kijiji,” anasema.

Mwita anasema viongozi wa eneo hilo pia huingilia kati pale walezi kama wazee wanaposhindwa kuhakikisha watoto wanakwenda shule.

“Kama babu au bibi analea wajukuu na wazazi wako mbali, na mzee huyo hawezi kuwapeleka shule, sisi tunaingilia kati. Wakati mwingine mtoto mwenyewe anakataa kwenda shule; tukibaini hali hiyo tunachukua hatua,” anasema.


Shuhuda za watoto

Kauli ya Mwita inatokana na watoto kadhaa kuonekana katika maeneo ya Lwamgasa wakifanya kazi katika sehemu za kusaga na kuosha mawe ya dhahabu kutoka migodini.

Miongoni mwao ni mvulana mwenye umri wa miaka 14 aliyekutwa akicheza ‘pool’ na marafiki zake baada ya kufanya kazi ya kuvunja na kuosha mawe ili kujikimu.

Anasema aliacha shule kutokana na njaa, “niliacha shule kwa sababu hatukuwa na chakula. Nilikuwa naenda darasani nikiwa na njaa, nikashindwa kuelewa vizuri masomo na nikirudi nyumbani hakukuwa na chakula. Njaa ilipozidi sikuwa na chaguo zaidi ya kuacha shule. Kwa sasa hakuna msaada wa ada wala chakula. Niliacha shule nikiwa darasa la sita na sasa ningekuwa la saba.”

Katika eneo la Mwaloni, mvulana mwingine wa miaka 15 anasema husaga mawe ili kujipatia kipato.

“Ninasaga mawe na kuyaweka kwenye karai. Nikijaza kiroba kimoja nalipwa Sh2,000 ambazo nazitumia kununua chakula,” anasema na kuongeza kuwa, aliacha shule akiwa darasa la nne na kwa sasa angekuwa la saba.

“Sikuwa najua kusoma wala kuandika vizuri, hivyo nikaamua kuacha shule. Nilipomwomba mama anirudishe niliahidi sitakuwa mvivu tena, lakini alisema hawezi kurudia kosa lilelile,” anasema.


Mtazamo wa walimu

Kutokana na hali hiyo, walimu wanasema utoro shuleni bado ni changamoto kubwa, hususani katika maeneo yanayozungukwa na shughuli za uchimbaji madini.

Walimu wa eneo hilo wanasema hali hiyo inaonesha changamoto zinazozikabili familia za jamii za wachimbaji madini ambazo watoto huvutwa kuingia katika shughuli za kiuchumi zinazokatiza masomo yao.

Mwalimu mmoja wa Lwamgasa ambaye hakutaka kutajwa jina kwa kuwa si msemaji rasmi anasema watoto chini ya miaka 18 hawaruhusiwi kufanya kazi migodini, lakini baadhi yao bado wanajihusisha na shughuli za madini.

“Kijiji cha Lwamgasa kina shule nyingi, lakini utoro ni tatizo kubwa. Mtoto anaweza kuandikishwa darasa la kwanza, akaingia shule kwa miezi michache na baadaye akapotea,” anasema.

Anasema uongozi wa shule unapowatafuta wanafunzi waliopotea mara nyingi hugundua familia zimehamia maeneo mengine yenye shughuli za uchimbaji madini.

“Wakati mwingine tunagundua wamehamia vijiji jirani kama Tembo ambako shughuli za uchimbaji madini zinaendelea,” anasema.

Kwa mujibu wa kumbukumbu za shule, mwanafunzi akikaa nje ya shule kwa siku 90 huondolewa kwenye orodha ya wanafunzi wanaohudhuria masomo na kuhesabiwa kuwa ametoweka.

Anasema uhamaji unaochochewa na uchimbaji mdogo wa madini ni moja ya sababu kuu za tatizo hilo.

Katika baadhi ya matukio, wazazi huwasajili watoto shule huku wakiwahusisha pia katika shughuli za utafutaji wa dhahabu.

“Watoto wanaweza kuhudhuria shule kwa muda mfupi, lakini dhahabu ikipungua huhama pamoja na familia zao kwenda eneo jingine la uchimbaji,” anasema mwalimu huyo.

Anaeleza baadhi ya watoto hutoka maeneo ya mbali kama vile mkoani Singida wakifuatana na familia zao kutafuta dhahabu.

Mwalimu huyo anatoa mfano wa tukio la hivi karibuni la kuwakuta wanafunzi wawili wakizurura mitaani bila sare za shule.

“Mmoja alikuwa darasa la sita na mwingine la saba. Nilikutana nao nje ya shule wakidai wanaenda nyumbani kuomba fedha za mahitaji ya shule, lakini maelezo yao hayakuwa ya kuaminika. Niliwapeleka kituo cha polisi karibu na makao makuu ya halmashauri na wazazi wao waliitwa kutoa maelezo,” anasema.

Anasema utoro wa wanafunzi huathiri madarasa mbalimbali akieleza: “Katika darasa moja la wanafunzi wa darasa la saba, wanafunzi wanane kati ya 165 walioandikishwa hawakufanya mtihani kwa sababu walikuwa watoro.”

Anasema mwaka 2025 pekee, jumla ya watoto 61 kutoka darasa la kwanza hadi la saba waliondoka shule kutokana na uhamaji na ajira zinazohusiana na shughuli za uchimbaji madini.

Takwimu za kitaifa zinaonesha kuwa tatizo la utoro na kuacha shule ni kubwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Hali hiyo inachangiwa na usimamizi hafifu na utekelezaji dhaifu wa Kifungu cha 5(1) cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, Sura ya 366 (Toleo lililorekebishwa la 2023), hali ambayo imechangia kuongezeka kwa ajira za watoto katika migodi kama iliyopo  Geita na kusababisha watoto wenye umri wa miaka 10 hadi 15 kuacha shule na kunyimwa haki yao ya elimu pamoja na maisha bora.

Tanzania ina mfumo imara wa kisheria wa kulinda haki za watoto ukiwamo Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, Sura ya 366 (Toleo lililorekebishwa la 2023) na Sheria ya Mtoto, Sura ya 13 (Toleo lililorekebishwa la 2023), ambazo zote zinakataza watoto chini ya miaka 18 kushiriki katika kazi hatarishi kama uchimbaji madini.

Vilevile, Kifungu cha 6.2 cha Sera ya Madini ya mwaka 2009 kinaelekeza Serikali kuweka na kusimamia kanuni kali dhidi ya ajira za watoto ili kulinda ustawi wao, huku mamlaka husika zikitakiwa kuzuia watoto kuingia katika maeneo ya uzalishaji wa madini.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, ripoti ya balehena vijana, iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), asilimia 25.7 ya watoto wenye umri wa miaka 10 hadi 13 walioacha shule nchini walifanya hivyo kutokana na utoro au kukataa kwenda shule.

Taarifa ya Takwimu za Elimu ya Msingi ya mwaka 2023 (BEST) kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Ofisi ya Rais-Tamisemi inaonesha kuwa, mwaka 2022 Mkoa wa Geita ulikuwa na wanafunzi 21,596 wa shule za msingi na wanafunzi 9,008 wa shule za sekondari walioacha shule, idadi kubwa zaidi Tanzania Bara.


Kauli za viongozi

Katika shina la CCM namba nane, Gombani, viongozi wa jamii wanaeleza wasiwasi kuhusu watoto wanaoacha shule na kujihusisha na kazi ngumu.

Balozi Sylvester Omolo anasema mzazi anaweza kufikishwa mahakamani iwapo mtoto wake hatahudhuria shule.

“Tumekuwa tukielimisha wazazi kuhakikisha watoto wanakwenda shule, lakini wengi wanakabiliwa na shinikizo la hali ngumu ya maisha,” anasema akieleza maeneo ya migodi ni hatari zaidi kwa watoto.

“Watoto wa miaka 12 hadi 15 hubeba magunia ya mawe yaliyosagwa kutoka eneo moja kwenda jingine kwa malipo ya Sh5,000. Katika shughuli za uchakataji wa dhahabu, kuosha mawe bila kutumia zebaki hulipwa Sh5,000,” anasema.

Anaeleza kuwa, matumizi ya zebaki yamepigwa marufuku ingawa watoto wanaotoka katika mazingira magumu sana bado hujihusisha nayo.

“Migodi imezungushiwa uzio ili kuzuia watoto kuingia,” anasema na kubainisha kuwa, baadhi ya watoto ni yatima au hawapati msaada wa wazazi wao, hali inayowalazimu kufanya kazi ili kuishi.

Licha ya madai kuwa wanafunzi huenda shule wakiwa na njaa, Omolo anasema wazazi huchangia chakula, huku shule zikitoa uji wa mchana ili kuhakikisha watoto hawaachi masomo.

“Shule zimekubaliana kuchangia chakula; shule za sekondari hupokea kilo 25 za maharagwe na kilo 20 za mahindi, huku shule za msingi zikipokea kilo tano,” anasema.

Baadhi ya viongozi wa Kijiji cha Lwamgasa, wanasema wataendelea kuwafuatilia wanafunzi watoro na kusimamia sheria za mahudhurio ili kuhakikisha watoto wanarudi shuleni.

Alipotafutwa kwa simu, Mratibu wa Elimu wa Kata ya Lwamgasa, Peter Wambura, alikataa kuzungumzia suala hilo akisema hana mamlaka ya kufanya hivyo bila ruhusa kutoka kwa msimamizi wake.

“Mimi ni mtumishi wa Serikali na siwezi kuzungumzia masuala kama haya bila kupata kibali kutoka kwa msimamizi wangu,” anasema.


Itaendelea kesho