Prime
Utoto wauzwa kwa Sh2,000 migodini Geita -1
Geita. Katika eneo la Kwa Emmanueli Lwamgasa mkoani Geita, mvulana mwenye miaka 14 (jina limehifadhiwa) hutumia siku za maisha yake kuvunja mawe chini ya jua kali ili kujikimu yeye na ndugu zake wawili wenye miaka 17 na 19.
Kutokana na hali ngumu ya maisha ya familia yenye kipato kisichotabirika, ndugu hao hutegemea kila shilingi wanayoipata ili kuendelea kuishi. Kuanzia alfajiri hadi jioni, mvulana huyo wa miaka 14 pamoja na kaka zake hupambana kila uchao kuhakikisha wanapata mahitaji ya msingi.
Mvulana huyo na kaka yake wa miaka 19 huvunja mawe mgodini kwa ujira wa kati ya Sh2,000 na Sh5,000 kwa siku.
Utoto wao umetwaliwa na kazi ngumu ili kupata chakula, mavazi na mahitaji mengine ya msingi. Kila siku ni mapambano ya kuzuia njaa.
“Mama alituacha, baba alivunjika mguu kisha akarudi kijijini kwao. Mimi na kaka yangu mkubwa tunasaga mawe, huku kaka yetu wa miaka 17 akifanya kazi katika duka la huduma za mtandao. Tunatafuta chakula na mavazi kwa sababu angalau tuna nyumba ya kuishi,” anasema.
Kaka yao wa miaka 17 anasema elimu ni ndoto ya mbali kwao kwa kuwa wazazi wao hawana kipato.
“Nafanya kazi katika duka la huduma za mtandao napata takribani Sh2,000 kwa siku ili kujikimu mimi na ndugu zangu,” anasema.
Kaka mkubwa ambaye hakuwapo wakati wa mahojiano hufanya kazi karibu na mgodi. Licha ya saa nyingi za kazi na malipo madogo, watoto hao wanaendelea kuvumilia ili kuishi huku elimu ikiendelea kuwa ndoto isiyofikika.
Maisha ya kila siku
Unapofika Lwamgasa kwa kutumia gari aina ya Toyota Noah kutoka Katoro, ambalo hubeba takribani abiria 11, jambo la kwanza unaloliona ni soko la dhahabu lililo upande wa kulia, jirani na eneo panapochezwa kamari lenye bango linalokataza watoto wenye umri chini ya miaka 18 kuingia.
Lwamgasa ni kitongoji chenye shughuli nyingi, kikiwa na maduka, migahawa na baa zilizojaa wanaume wanaokunywa tangu asubuhi hadi usiku.
Nyuma ya shughuli hizo kuna migodi ya dhahabu ya wachimbaji wadogo (Mwela wa Dhahabu) pamoja na maeneo ya kuchakata mawe ya madini, ambayo husagwa ili kupata dhahabu au kuuzwa kwa wanunuzi wanaoyapeleka kuyachakata sehemu nyingine.
Katika migodi hiyo, watoto wenye umri wa kati ya miaka mitatu hadi 10 huonekana wakizurura na kucheza bila usimamizi, huku wenye umri wa miaka 13 hadi 17 wakibeba mawe, kuyavunja au kuosha dhahabu.
Hali hiyo imechangiwa na usimamizi hafifu na utekelezaji dhaifu wa Kifungu cha 5(1) cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, Sura ya 366 (Toleo lililorekebishwa la 2023), jambo ambalo linachochea kuongezeka kwa ajira za watoto katika migodi ya Geita.
Watoto wenye umri wa miaka 10 hadi 15 wanaacha shule, hivyo kunyimwa haki yao ya elimu na maisha bora.
Tanzania ina mfumo imara wa kisheria wa kulinda haki za watoto, ukiwamo Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini pamoja na Sheria ya Mtoto (Sura ya 13, Toleo lililorekebishwa la 2023), ambazo zinakataza watoto chini ya miaka 18 kufanya kazi hatarishi kama uchimbaji madini.
Kifungu cha 6.2 cha Sera ya Madini ya mwaka 2009 pia kinaelekeza hatua za kulinda watoto. Tanzania pia imepitisha mikakati na mipango ya kitaifa ya kutokomeza aina mbaya zaidi za ajira za watoto hususani katika sekta za madini, kilimo, kazi za majumbani na uvuvi.
Mipango hiyo inahusisha ushirikiano kati ya maofisa kazi, Serikali za mitaa, shule, polisi na maofisa ustawi wa jamii.
Katika maeneo ya migodi, Tume ya Madini na wakaguzi wa migodi hushiriki katika kusimamia marufuku ya ajira za watoto.
Waajiri wana wajibu wa kisheria kuthibitisha umri wa wafanyakazi, kuhakikisha mazingira salama ya kazi, kuepuka kuajiri watoto na kuzingatia sheria za kazi pamoja na ukaguzi.
Waziri mwenye dhamana ya kazi ndiye mamlaka kuu inayohusika na kufafanua kazi hatarishi, kutoa kanuni na kusimamia mifumo ya utekelezaji wa sheria za kazi.
Kwa sasa utekelezaji huo uko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu.)
Maofisa kazi wanawajibika kufanya ukaguzi wa maeneo ya kazi, kuchunguza kesi za ajira za watoto, kuwafikisha wahusika mahakamani na kuhakikisha waajiri wanazingatia sheria.
Akizungumzia suala hilo, Kamishna wa Madini, Dk AbdulRahman Mwanga, anasema Serikali inaongeza juhudi za kutokomeza ajira za watoto katika shughuli za uchimbaji madini kupitia ukaguzi mkali na hatua za kisheria.
“Tunafanya ukaguzi wa mara kwa mara na kuchukua hatua za kuzuia. Tunashirikiana kwa karibu na maofisa ustawi wa jamii, wakuu wa wilaya na Serikali za vijiji. Kama sekta, tayari tumeweka mifumo ya kuwaondoa watoto kila unapofanyika ukaguzi,” anasema.
Anasisitiza kuwa, watoto hawaruhusiwi kufanya kazi yoyote ya uchimbaji madini kwa mazingira yoyote.
“Hata kama shughuli imeanzishwa na wazazi wa mtoto, kuhusisha watoto katika shughuli za madini ni kinyume cha sheria. Mmiliki yeyote wa mgodi anayefanya kazi bila leseni anavunja sheria na mwenye leseni anafahamu kuwa akibainika kufanya hivyo leseni yake itasimamishwa mara moja,” anasema.
Kamishna huyo anasema wamiliki wa migodi wanapaswa kufanya mikataba na waendeshaji wenye leseni pekee, akionya kuwa yeyote atakayekiuka masharti hayo atanyang’anywa leseni kabisa.
“Tukimkamata mtu yeyote akivunja sheria hizi, tunafuta kabisa leseni yake,” anasema.
Njaa yawatoa watoto shuleni
Mwandishi wa The Citizen aliyetembelea eneo la Lwamgasa Machi 2026 alikuta watoto wengi walioacha shule, akiwamo mvulana mwingine wa miaka 14 (jina linahifadhiwa) aliyekutwa akicheza ‘pool’ baada ya kufanya kazi ya kuvunja na kuosha mawe.
Aliacha shule kutokana na njaa akieleza: “Niliacha shule kwa sababu hatukuwa na chakula. Nilikuwa naenda darasani nikiwa na njaa, nikashindwa kuelewa masomo na nikirudi nyumbani hakukuwa na chakula. Njaa ilipozidi sikuwa na chaguo zaidi ya kuacha shule. Hakuna msaada wa ada wala chakula shuleni. Niliacha nikiwa darasa la sita na sasa ningekuwa darasa la saba.”
Katika eneo la Mwaloni, mvulana mwingine wa miaka 15 husaga mawe ili kujipatia kipato.
“Ninasaga mawe na kuyaweka kwenye karai. Nikijaza gunia moja nalipwa Sh2,000 ambazo ninazitumia kununua chakula,” anasema.
Anasema aliacha shule akiwa darasa la nne na hawezi kusoma wala kuandika vizuri.
“Niliomba mama anirudishe shule nikiahidi sitakuwa mvivu, lakini alisema hawezi kurudia kosa lilelile,” anasema.
Mvulana mwingine mwenye miaka 14 hufanya kazi ya kusaga mawe muda wote.
Anasema: “Niliacha shule nikiwa darasa la tano, ningekuwa darasa la sita. Kwa sasa sina ndoto yoyote kuhusu maisha yangu ya baadaye, ni Mungu tu anayejua.”
Mvulana wa miaka 13 anaonekana akiwa amebeba mfuko wa salfeti (kiroba) wenye mawe machache kwa ajili ya kuuza.
“Leo tu ndiyo siku ambayo sikuenda shule. Nikimpata mnunuzi nalipwa Sh1,000. Nahitaji fedha hizo ili kununua kaptura ya shule,” anasema akiongeza kuwa baba yake anafanya kazi buchani lakini hagharamii mahitaji ya shule.
Wakati huohuo, Adventina Bundala, anasema alilazimika kumtoa binti yake wa miaka 11 shuleni baada ya kujifungua watoto pacha ambao sasa wana miaka mitatu. Pia ana mtoto mwingine wa miaka mitano.
“Nilipojifungua pacha sikuwa na msaada wowote. Mume wangu alikuwa amekimbia, hivyo nikawa mtafutaji wa familia. Naenda migodini kutafuta mawe ya kuuza kwa wanunuzi wa dhahabu,” anasema.
Binti yake aliacha shule akiwa na miaka tisa ili kuwalea pacha hao.
“Tunatarajia wakikua tutajua namna ya kumrudisha shule,” anasema.
Baadhi ya wazazi wanasema mapambano ya kila siku ya kutafuta mahitaji ya msingi yamewaacha watoto wengi bila chaguo lingine isipokuwa kuacha shule.
Mzazi mmoja anaeleza kuwa alipoondoka kijijini kwenda kutafuta fedha, aliporejea alimkuta mtoto wake wa miaka 13 ameacha shule kutokana na ukosefu wa chakula nyumbani.
Anasema watoto hao kila uchao hujishughulisha na kazi ya kusaga na kuosha mawe yenye madini ya dhahabu ili kujikimu kimaisha.
“Hali hii inawanyang’anya watoto hawa utoto wao pamoja na haki yao ya kupata elimu,” anasema.
Kwa upande wake, kijana mwenye umri wa miaka 17, ambaye hakuendelea na masomo baada ya kumaliza darasa la saba, anasema kwa sasa anajishughulisha na kazi ya kusaga mawe akijipatia ujira wa Sh20,000 kwa siku, huku akiweka akiba kwa ajili ya kutimiza ndoto yake ya kusomea ufundi wa umeme katika chuo cha Veta.
Anaeleza hulipwa Sh5,000 kwa kila viroba saba vya mawe anayosaga kwa kutumia mashine, hivyo hulazimika kusaga viroba 28 kwa siku ili kufikia kiwango cha mapato anachokusudia.
“Sehemu ya fedha ninayopata huwasaidia wazazi wangu na kiasi kinachobaki ninaweka akiba ili kutimiza ndoto yangu ya kuwa fundi umeme,” anasema.
Mvulana mwingine wa miaka 14 aliyebaki nyumbani kuwatunza wadogo zake wakati wazazi wake wakiwa safarini hupata Sh2,000 kwa kila kiroba anachohamisha kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
Anasema aliwahi kutumia zebaki kuchenjua dhahabu lakini aliacha baada ya kuathiriwa na fangasi kwenye vidole.
Jirani na eneo hilo, wanawake pia wanaonekana wakisaga mawe katika mazingira yenye vumbi, huku watoto wa miezi mitatu hadi miaka mitano wakiwa karibu nao.
Upondaji mawe kugharimia matibabu
Akizungumza na The Citizen, Joyce Malomo akiwa amembeba mtoto wake wa miezi mitatu aliyezaliwa na ulemavu wa miguu, anasema baba wa mtoto amemkimbia hivyo analazimika kuvunja mawe ili kupata fedha za kujikimu na kugharimia matibabu.
“Namtibu mwanangu. Huduma hospitalini ni bure lakini vifaa vya matibabu vinagharimu Sh200,000. Ninalazimika kuja naye hapa kwa sababu sina mtu wa kumuacha naye,” anasema.
Katika mgodi wa dhahabu wa Miembeni, mvulana aliyekuwa amevaa helmeti na buti alikataa kutaja umri wake.
Hata hivyo, anasema alianza kazi mgodini hapo mwaka jana baada ya kufeli mtihani wa darasa la saba. Alipoulizwa umri wake aliondoka.
Mita chache kutoka mgodini hapo, wasichana ambao hawakufahamika majina walionekana wakifanya kazi katika migahawa, huku mikokoteni kadhaa iliyovutwa na punda ikibeba mawe makubwa kutoka mgodini kuelekea Gombani ikiwa imewabeba wavulana watatu kila mmoja. Walikataa kuzungumza na waandishi wa habari, wazazi kadhaa walisema umaskini na mahitaji ya kila siku ndiyo sababu kuu zinazowafanya watoto wao kukosa shule na badala yake kufanya kazi ya kusaga mawe migodini.
“Mume wangu aliondoka na kuniacha na watoto watano wa kuwahudumia,” anasema Rehema Maneno.
“Watoto wanapoenda shule wakiwa na njaa hawawezi kuwa makini darasani. Angalau wanaposaidia kusaga mawe tunapata kiasi kidogo cha fedha za kununua chakula.”
Mzazi mwingine aliyejitambulisha kwa jina moja la John anasema gharama za elimu bado ni kikwazo licha ya kuwapo kwa elimu bila ada. “Bado tunahitaji sare za shule, madaftari ya mazoezi na nauli ya usafiri. Siwezi kumudu gharama hizo zote, hivyo wavulana wangu wawili huongozana nami hadi eneo la kazi na kusaidia kusaga mawe,” anasema.
Maria Omari, anayewalea wajukuu zake, anasema ugumu wa maisha unawalazimu kufanya uamuzi mgumu akieleza.
“Tunafahamu elimu ni muhimu, lakini njaa ni tatizo kubwa zaidi. Watoto hufanya kazi ya kusaga mawe kwa saa chache ili familia iweze kujikimu. Hali ya maisha ikiwa bora nitawarejesha shule.”
Usalama migodini
Katika mgodi wa dhahabu wa Mpandachalo, uliopo Lwamgasa, Mkaguzi mkuu wa migodi, January Mwendo anasema mgodi huo unazingatia kikamilifu kanuni za Tume ya Madini na kuweka usalama wa wafanyakazi mbele.
“Mgodi umezungushiwa uzio, una lango la ulinzi na wasimamizi wanahakikisha hakuna mtu mwenye umri chini ya miaka 18 anayeajiriwa,” anasema.
Mmiliki wa mgodi huo, Hamisi Mbaga anasema walinzi kutoka JKT wamewekwa kuzuia watu wasiokuwa na ruhusa kuingia, wakiwamo walevi.
“Wasimamizi wanathibitisha kuwa kila mfanyakazi ni Mtanzania na ametimiza umri wa miaka 18,” anasema.
Mlinzi katika mgodi wa Miembeni, Revocatus John kutoka Kigoma, anasema amebaini watoto wengi wakizurura mitaani bila usimamizi.
“Haturuhusu watoto kuingia migodini, lakini nimeona hasa wavulana wakibeba mchanga kutoka eneo moja kwenda jingine,” anasema.
Anaishauri Serikali ichukue hatua kali kuhakikisha watoto wote wanakwenda shule.
Mtazamo wa jamii
Katika shina la CCM namba nane, Gombani, viongozi wa jamii wameeleza wasiwasi kuhusu ongezeko la watoto wanaoacha shule na kuingia katika kazi ngumu.
Balozi wa shina hilo, Sylvester Omolo anasema: “Mtoto yeyote asiyekwenda shule anaweza kusababisha baba yake kufikishwa mahakamani. Tumekuwa tukielimisha wazazi lakini wengi wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha.”
Anasema maeneo ya migodi ni hatari zaidi kwa watoto.
“Watoto wa miaka 12 hadi 15 hubeba viroba vya mawe yaliyosagwa kwa malipo ya Sh5,000. Kuosha mawe bila kutumia zebaki pia hulipwa kiasi hicho,” anasema.
Anaeleza matumizi ya zebaki yamepigwa marufuku, ingawa watoto walio katika mazingira magumu sana bado hujihusisha nayo.
“Migodi imewekewa uzio ili kuzuia watu wasiokuwa na ruhusa kuingia,” anasema.
Anaeleza kuwa, baadhi ya watoto ni yatima au hawapati msaada kutoka kwa wazazi wao jambo linalowalazimu kufanya kazi.
Omolo anasema shule zimeanzisha utoaji wa uji wa mchana ili kupunguza utoro.
Vilevile, shule za msingi hutoa kilo tano za maharage na kilo tano za mahindi, huku shule za sekondari zikipokea kilo 25 za maharage na kilo 20 za mahindi kwa ajili ya chakula cha watoto shuleni.
Itaendelea kesho