Pangani watakiwa kuzingatia lishe bora

Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Galib Lingo akizungumza na wananchi wa wilaya hiyo katika kijiji cha masaika kuhusiana na umuhimu wa kuzingatia lishe bora.

Muktasari:

Wananchi wilayani Pangani wametakiwa kuhakikisha familia zao zinapata mlo kamili ikiwemo chakula bora ili kuwa na afya bora kwa ustawi wa jamii na uchumi wa Taifa.

Pangani. Wananchi wilayani Pangani wametakiwa kuhakikisha familia zao zinapata mlo kamili ikiwemo chakula bora ili kuwa na afya bora kwa ustawi wa jamii na uchumi wa Taifa.

Rai hiyo imetolewa leo Jumatatu Mei 30, 2022 na Mkuu wa Wilaya hiyo, Ghaibu Lingo katika viwanja vya Shule ya Msingi Masaika wilayani humo wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi itakayozinduliwa na Mwenge wa Uhuru katika Wilaya hiyo.

Amesema wakuu wa kaya wana wajibu kuhakikisha familia zao zinapata mlo wa mpangilio.

Lingo amesema lishe bora inasaidia kuondoa tatizo la udumavu kwa watoto na kuwafanya wakue vizuri wakiwa na afya bora.

"Ulaji hovyo wa vyakula visivyo sahihi vinasababisha madhara katika mwili wa binadamu hasa kwa watoto kwa sababu wanapata tatizo la udumavu." amesema.

Amesema jamii inatakiwa kujenga tabia ya kufanya mazoezi na kuzingatia mlo kamili ili kuweza kujiepusha na magonjwa na viriba tumbo.

Kwa upande wake kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa, Sahili Geraruma amesema wanaume wanatakiwa kushiriki katika kuhakikisha familia zao zinapata lishe bora.

"Suala la kuzingatia lishe bora si tu kina mama ndiyo wasimamie familia na kina baba pia tushiriki hasa mama anapokuwa mjamzito hakikisha kama ni mwenza wako unampeleka kituo cha afya ili aweze kupata elimu juu ya lishe bora," amesema Sahili.

Amesema suala la ushirikiano kuanzia ngazi ya familia pamoja na wataalamu wa afya litasaidia kutokomeza tatizo la udumavu kwa kula mlo kamili wenye lishe bora.

"Jamii inapaswa kula vyakula vyenye virutubisho ili iweze kuwa na afya bora pamoja na matumizi ya chumvi yenye madini joto hivyo nasisitiza suala hili si la mtu mmoja ni la familia nzima kwa kushirikiana na wataalamu wa afya," amesema.