Panya wateketeza eka 30,000 za mahindi Chalinze

Muktasari:

  • Panya wanakula mpunga na wanafukua viazi mashambani.

Chalinze. Wimbi la panya wanaoharibu mazao mashambani limeibuka kwenye maeneo mbalimbali katika halmashauri ya Chalinze mkoani Pwani ambapo zaidi ya eka 30,000 za mahindi yameharibiwa kwa kuliwa na wanyama hao.

Baadhi ya kata zinazodaiwa kuvamiwa na panya hao ni Mandela, Bwewe, Lugoba na Kibindu na pia wanyama hao wanafukua na mazao jamii ya viazi.

Baraza la Madiwani wa Chalinze leo Mei 27, wamemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya eneo hilo, Edes Lukoa kuwasiliana mara moja na mamlaka husika ili kupata dawa ya kuua panya hao.

Diwani kata ya Kibindu, Ramadhani Mkufya amesema panya hao wameanza kuharibu mazao hayo tangu msimu wa vuli na sasa wameongezeka mno na wanaonekana si wale wa kawaida waliozoeleka kuonekana hata majumbani.

"Tumehamasisha wananchi walime mazao ya chakula msimu huu kweli wamelima sana lakini cha kusikitisha mwenyekiti limeibuka wimbi la panya wanakula mahindi na tayari zaidi ya eka 20,000 zimeliwa, mbaya zaidi hawa panya wanakula pia na mpunga na wanafukua viazi, hali si shwari mashambani," amesema Mkufya.