Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Polisi aliyetoweka bado hajapatikana siku 68

Polisi aliyetoweka bado hajapatikana siku 68

Muktasari:

  • Baada ya Emanuel Govela kutoonekana kwa zaidi ya miezi miwili sasa, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene amesema anazo taarifa hizo na ameagiza uchunguzi wa kina ufanyike.

Dodoma. Baada ya Emanuel Govela kutoonekana kwa zaidi ya miezi miwili sasa, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene amesema anazo taarifa hizo na ameagiza uchunguzi wa kina ufanyike.

Leo zinatimia siku ya 68 tangu Govela atoweke nyumbani kwake Nkuhungu jijini hapa alikokuwa anaishi. Si ndugu zake tu wanaomtafuta, bali kituo chake cha kazi cha Mji wa Kiserikali jijini Dodoma, hajaonekana kwa muda wote huo.

Govela (39) alipoteza mawasiliano na ndugu zake tangu Juni 26 na tangu wakati huo hajaonekana. Kwa kipindi hicho chote ndugu wamekuwa wakimtafuta bila mafanikio na hadi jana hawajapata taarifa zozote zenye matumaini ya kumpata akiwa hai au vinginevyo.

“Taarifa hizo ninazo, polisi wanafanya kazi kubwa usiku na mchana kumtafuta ofisa huyo, hata ndugu zake nao wanamtafuta lakini hatujafanikiwa ila hatujakata tamaa,” alisema Waziri Simbachawene.

Waziri alisema siku chache baada ya kutoonekana kwake, mkuu wa polisi nchini alimpa taarifa na wamekuwa wakimweleza hatua zinazoendelea katika jitihada za kumtafuta ingawa bado hajapatikana.

Simbachawene alisema ugumu wa kupatikana kwake ni kwa sababu alitoweka bila kuchukua kielelezo cha kusaidia kupatikana kwake, ikiwamo simu ambazo aliziacha ndani ya nyumba alimokuwa anaishi.

Alisema bado wanamtafuta ofisa huyo lakini muda ukifika watasema juu ya kinachoendelea ili umma utambue na akatoa wito kwa yeyote mwenye taarifa za aina yoyote zinazoweza kusaidia kupatikana kwa Govela azitoe kituo chochote cha polisi.

Jana mdogo wa Emanuel, Athuman Govela alisema familia inaendelea kumtafuta kwa kushirikiana kwa karibu na Jeshi la Polisi.

Katika mahojiano aliyofanya na gazeti hili nyumbani kwake Mtera, mama mzazi wa Emanuel, Monika Maluli alisema matamanio yake ni “kumpata mwanangu akiwa hai lakini hata akiwa amekufa natamani wamtupe nje ya nyumba yangu ili nimzike.”

Awali, ndugu walisema juhudi za polisi kumtafuta kachero huyo zilikuwa ndogo, ingawa baadaye walikiri kujiridhisha kwamba polisi wanafanya kazi usiku na mchana na maeneo wanakopita wanaambiwa polisi walikwenda.