Polisi Arusha yawanasa wanaodaiwa kutengeneza konyagi feki

Muktasari:

  • Miongoni mwa watuhumiwa yumo mmiliki wa baa maarufu jijini Arusha ya Kipong

Arusha. Polisi mkoani Arusha linawashikilia watu kadhaa akiwemo mmiliki wa baa maarufu jijini Arusha ya Kipong kwa kosa la kutengeneza na kuuza kinywaji bandia aina ya Konyagi kinyume cha sheria.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo ameiambia Mwananchi Digital jana Machi 25, 2024 kuwa wanawashikilia watu hao kwa kosa la kuendesha kiwanda bubu cha utengenezaji wa pombe kali aina ya Konyagi.

“Siwezi kusema ni watu gani na wangapi tumewakamata hadi sasa, cha kujua ni kweli awali tulikamata watu wawili na kuna ambao leo wamekamatwa ila sijajua wangapi maana nilikuwa nje ya ofisi, na operesheni inaendelea, subirini tukikamilisha tutatoa taarifa kamili,” amesema.

Katika tukio hilo, miongoni mwa watu waliokamatwa ni mmiliki wa baa ya Kipong, John Shayo na mwanamke anayedaiwa kuwa mwendesha mitambo ya utengenezaji wa kilevi hicho.

Akizungumzia tukio, Sia, mke wa Shayo amesema  mume wake alikamatwa Machi 23, 2024 usiku wa manane na maofisa wa mamlaka mbalimbali, likiwamo Jeshi la Polisi waliojitambulisha na kufanya upekuzi kabla ya kukutana na shehena za vinywaji hivyo.

Inadaiwa mtuhumiwa mwingine ambaye ni mwanamke alikutwa na mitambo inayodaiwa kutumika kutengeneza pombe hizo bandia.

Joseph Mwaikasu, Meneja wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) mkoani Arusha, wenye umiliki wa utengenezaji wa Konyagi, amesema wamesikitishwa na taarifa hizo akiahidi kufuatilia kwa ukaribu tukio hilo.

“Tumeshindwa kuelewa jambo hilo, ila tumesikitishwa na kitendo kinachofanywa na wafanyabiashara wasio waaminifu kwa lengo la kujipatia kipato kwa njia ya udanganyifu, hii ni kuhujumu bidhaa zetu na uchumi pia," amesema Joseph.

Amesema suala la bidhaa bandia linawaathiri kwa kiasi kikubwa kwa kupoteza wateja na kushusha mauzo, hivyo kuipunguzia pia Serikali mapato ambayo wangelipa kama kodi.

"Naiomba Serikali kuwachukulia hatua kali wale wote wanaojihusisha na mtandao wa kutengeneza na kusambaza bidhaa feki ili kuepusha viwanda vya ndani kushindwa kujiendesha," amesema.

Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Arusha, Eva Rafael amesema wanasuburi taarifa ya Jeshi la Polisi, baada ya kukamilisha uchunguzi kuhusu kutumika kwa nembo za mamlaka kwenye bidhaa hizo.

"Ni kweli nimesikia kuna nembo zetu zimekamatwa zikitumiwa kinyume cha sheria kutengeneza bidhaa feki, hivi sasa polisi wanakamilisha uchunguzi ili watupatie taarifa kamili nitawajulisha," amesema Eva.

Mmoja wa wateja wa Konyagi, Stephano Mushi amesema yapo madhara ya kutumia bidhaa yoyote bandia isiyothibitishwa na mamlaka kwa matumizi ambayo hayawezi kuonekana kwa haraka.

Amesema hivi karibuni alitumia kinywaji hicho akahisi maumivu ya kichwa na kukosa nguvu kwa baadhi ya viungo ikiwamo mikono na miguu.

Alitumia nafasi hiyo kuomba Serikali kufanya msako wa mara kwa mara kukamata watu wanaojipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kwa kutengeneza bidhaa bandia ili kunusuru maisha ya Watanzania.