Polisi aua kwa risasi akijiami
Muktasari:
- Tukio hilo lilitokea juzi saa 9:45 alasiri eneo la Ikungi madukani.
- Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Debora Magiligimba alisema jana kuwa siku ya tukio Joseph alimfuata mke wake ambaye ni mama lishe katika vibanda vilivyoko kando ya Barabara Kuu ya Singida-Dodoma.
Singida. Mkazi wa Kijiji cha Ikungi, Herman Joseph (32) amefariki dunia papo hapo baada ya kupigwa risasi tumboni na askari polisi aliyekuwa akijihami.
Tukio hilo lilitokea juzi saa 9:45 alasiri eneo la Ikungi madukani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Debora Magiligimba alisema jana kuwa siku ya tukio Joseph alimfuata mke wake ambaye ni mama lishe katika vibanda vilivyoko kando ya Barabara Kuu ya Singida-Dodoma.
Alisema alipofika kibandani alimwomba mkewe, Maria Jacob (28) amwandalie chakula cha mchana lakini kulizuka malumbano yaliyosababisha mwanaume huyo kuchomoa kisu kutoka kwenye mfuko wa suruali.
“Alipoona kisu, Maria alikimbia huku akiwa amembeba mtoto mgongoni. Wakati akiendelea kukimbia, Joseph alimchoma kisu mkewe kwenye makalio,” alisema.
Kamanda alisema baada ya kuchomwa kisu mwanamke huyo alikwenda kujificha kwenye kibanda cha Janeth Mathias.
“Baada ya kupiga yowe, Shaban Jumanne na Issa Shaban walifika eneo la tukio. Jumanne alijeruhiwa mkono wa kulia na Issa wa kushoto. Baada ya hapo, taarifa ilifika kituo kidogo cha polisi Ikungi. Askari wanne walifika eneo la tukio,” alisema.
Alifafanua kuwa askari hao walipofika walikuta Joseph amejificha ndani ya kibanda na baada ya muda alitoka na kutangaza kuwa haogopi chochote na yupo tayari kuuawa.
“Baada ya kutakiwa kujisalimisha, hakutii badala yake alimfuata askari aliyekuwa na silaha na kutaka kumchoma kisu kifuani, askari alikikwepa na alipiga risasi mbili hewani kwa lengo la kumfanya aogope,” alisema.
Kamanda alisema Joseph hakuogopa badala yake aliendelea kumfuata na wakati askari huyo akirudi nyuma aliteleza na kuanguka ndipo Joseph alipotaka kumchoma kisu kifuani naye alijihami kwa kumpiga risasi.