Polisi lawamani, Kinana amng’ata sikio Wambura

Muktasari:

  • Wakati wananchi wa mikoa ya nyanda za juu kusini wakilalamika kuchoshwa na usumbufu wanaodai kuupata kutoka polisi wa usalama barabarani, Makamu Mwenyekiti CCM, Abdulrahman Kinana amemuagiza Kamanda wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Camillius Wambura kufanya tathmini ya utendaji wa jeshi hilo.

Mbeya. Wakati wananchi wa mikoa ya nyanda za juu kusini wakilalamika kuchoshwa na usumbufu wanaodai kuupata kutoka polisi wa usalama barabarani, Makamu Mwenyekiti CCM, Abdulrahman Kinana amemuagiza Kamanda wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Camillius Wambura kufanya tathmini ya utendaji wa jeshi hilo.

Wananchi hao wamemwambia Kinana kuwa trafiki mara kwa mara huyasimamisha magari yanayobeba abiria na yale ya mizigo kwa madai ya kuyakagua muda ambao ni wa watu kuwahi ofisini na maeneo mengine ya kujitafutia riziki, huku wakidai kufanya hivyo kunawapotezea muda.

Kinana alisema kero hiyo imekuwa ikijirudia kila mkoa alikopita kuwasikiliza wananchi.

Akiwa wilayani Mbozi mkoani Songwe jana, Kinana licha ya kupongeza uteuzi wa IGP Wambura, alimshauri aanze kazi ya kushughulika na kero za wananchi zinazoelekezwa kwa trafiki.

“Nimuombe IGP mpya na vyombo vyake kufanya tathmini ya kina juu ya utendaji wa Jeshi la Polisi kitengo cha usalama barabarani, hasa maeneo ya miji na mijini wamejazana sana, wanawasumbua wananchi kila baada ya kilomita moja unakuta wamesimamisha gari.

Alisema vituo vya polisi vilivyoko mijini vina idadi kubwa ya askari wa usalama barabarani, ikilinganishwa na vile vya pembezoni, hivyo alitoa rai kwa IGP Wambura kulitazama jambo hilo na kulifanyia kazi.

Mwananchi lilimtafuta IGP Wambura azungumzie hilo na alisema anaupokea ushauri huo na ataufanyia kazi.

“Ushauri uliotolewa ni mzuri na ninaupokea na ninaenda kuufanyia kazi kwenye taasisi yangu,” alisema Wambura.

Malalamiko ya wananchi

Jerome Mwakibete alisema polisi hao wamekuwa na mtindo wa kusimamisha magari majira ya asubuhi na jioni na maswali wanayoulizwa madereva ni yale yale kila kituo.

“Jambo hili linatukera sisi wananchi, kila kituo gari inasimamishwa, halafu wanajua gari limebeba abiria na wengine tunawahi kwenye majukumu hasa nyakati za asubuhi,” alisema.

Mwakibete alidai kutoka Mbeya mjini hadi Tunduma kuna vituo 15, askari hao huyasimamisha magari na hata wakigundua kosa, hawaruhusu gari kutoka mapema bila kufanya malipo.

“Unakuta wanaoumia ni abiria, sasa kama namba ya gari wanaijua kwa nini wasiandikie gari iendelee na safari na sisi tuwahi kazini badala ya kusimama kwa muda mrefu kusikiliza maswali yao. Kwa kweli wamekuwa shida,” alisema.

Seleman Omary, dereva wa lori alishauri kutokana na usumbufu wanaoupata ni vema wakatenga vituo maalumu vichache ambavyo askari hao watakuwa wanakagua magari, tofauti na mfumo wanaotumia sasa.

“Kila kituo unachosimama wanaulizia leseni na stika za usalama barabarani, inakuwa kero hasa sisi watu wa magari tunagombana sana na mabosi wetu tunachelewa kufikisha mizigo,” alisema Omary.