Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Polisi Mbeya yaunda kikosi kazi kudhibiti biashara usafirishaji wa binadamu

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya ambaye pia ni Mkuu wa Polisi Jamii, Anthony Mkwawa (katikati) alipofunga mafunzo kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga.

Muktasari:

  • Hatua hiyo imekwenda sambamba na onyo kwa wamiliki wa nyumba kuhakikisha wanajiridhisha kuhusu uraia na uhalali wa nyaraka za wapangaji wao ili kuepuka kuchukuliwa hatua za kisheria, ikiwemo kutaifishiwa nyumba zitakazobainika kutumika.

Mbeya. Mkoa wa Mbeya umeunda kikosi kazi kitakachosimamia uratibu wa shughuli za kuzuia na kupambana na biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu na kuhamasisha jitihada za wananchi kutoa taarifa.

Hatua hiyo inalenga kuimarisha mapambano dhidi ya mtandao wa usafirishaji haramu wa binadamu ambao mamlaka zinasema umeendelea kuwa tishio kwa usalama wa jamii, ustawi wa wananchi na uchumi wa taifa.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya ambaye pia ni Mkuu wa Polisi Jamii, Anthony Mkwawa, amesema hayo Ijumaa, Julai 24, 2026, alipofunga mafunzo kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga.

Mafunzo hayo yaliandaliwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Sekretarieti ya Kuzuia na Kupambana na Usafirishaji Haramu wa Binadamu kwa kushirikiana na Shirika la Comunita Volontari per il Mondo (CVM).

Mkwawa amesema mapambano hayo hayawezi kufanikiwa bila ushirikiano wa wananchi, vyombo vya dola na wadau mbalimbali.

Amesema mafunzo hayo yalilenga kuwajengea uwezo washiriki na kufanikisha kuundwa rasmi kwa kikosi kazi cha ngazi ya mkoa kitakachoratibu juhudi za kuzuia na kupambana na uhalifu huo.

"Kikosi kazi hiki kitakuwa na jukumu la kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya usafirishaji haramu wa binadamu, kuhamasisha utoaji wa taarifa na kuratibu shughuli zinazohusiana na mapambano dhidi ya uhalifu huo ndani ya Mkoa wa Mbeya," amesema Mkwawa.

Mrakibu Mwandamizi wa Uhamiaji Mkoa wa Mbeya, Gerald Mandai, alisema wahamiaji wanaotumia njia zisizo halali hukumbana na hatari mbalimbali, huku Serikali ikibeba gharama za kuwahudumia na kuwarejesha katika nchi zao wanapokamatwa.

Mwakilishi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Sekretarieti ya Kuzuia na Kupambana na Usafirishaji Haramu wa Binadamu, Wakili Chris Mollel, amesema wamejadili masuala ya kuimarisha juhudi za kuzuia uhalifu huo, unaowalenga wanawake na watoto ambao ni miongoni mwa makundi yaliyo katika hatari zaidi.

Aidha, Mollel aliwataka wamiliki wa nyumba kuzingatia sheria kabla ya kumpangisha mtu ili kujiridhisha kuhusu uraia wake na uhalali wa nyaraka zake.

Alionya kuwa kushindwa kufanya hivyo kunaweza kusababisha hatua za kisheria, ikiwemo kutaifishwa kwa nyumba endapo itathibitika kuwa ilitumika katika biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu.

Mafunzo hayo yaliwakutanisha wadau mbalimbali, wakiwemo Jeshi la Polisi, Idara ya Uhamiaji, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS), Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, viongozi wa dini na wadau kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kuzuia na kupambana na biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu.


Kauli za wananchi

Mkazi wa Forest jijini hapa, Sakina Hashim, ameomba Jeshi la Polisi kufanya mikutano ya hadhara ili kupata maoni ya wananchi kufuatia kuwepo kwa kasumba ya wamiliki wa nyumba kupangisha kiholela, jambo linaloleta sintofahamu kwa jamii.