Polisi Pwani yafafanua uvumi wa miili sita kuonekana Mto Ruvu
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase
Muktasari:
- Polisi wamesema taarifa hizo zimekuwa zikijirudia kusambazwa tangu 2016 licha ya kufanyiwa uchunguzi na kutolewa ufafanuzi mara kadhaa. Laonya kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wanaoendelea kuzisambaza.
Kibaha. Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limewataka wananchi kupuuza taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu madai ya kuokotwa kwa miili ya watu sita katika Mto Ruvu, Wilaya ya Bagamoyo mkoani humo.
Jeshi hilo limesema kuwa taarifa hizo si za kweli na zimekuwa zikijirudia kusambazwa kwa nyakati tofauti, licha ya kutolewa ufafanuzi mara kadhaa.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa leo, Juni 9, 2026 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase, taarifa hiyo imekuwa ikisambazwa kupitia majukwaa ya Instagram na Facebook ikidai kuwa watu sita wameokotwa katika mto huo.
Polisi wamesema kuwa taarifa hizo zilianza kusambazwa kwa mara ya kwanza Desemba 21, 2016 na kufanyiwa uchunguzi na mamlaka, kisha kutolewa ufafanuzi kwa wakati huo.
Aidha, Septemba 13, 2025 taarifa hiyo ilisambazwa tena katika mitandao ya kijamii, na Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani likatoa ufafanuzi wake Septemba 14, 2025, likibainisha kuwa madai hayo hayakuwa ya kweli.
Hata hivyo, Juni 8, 2026 taarifa hizo zimeanza kusambazwa tena licha ya uchunguzi uliofanyika mara mbili kubaini kuwa hakuna ukweli wowote kuhusu madai hayo.
Kutokana na hali hiyo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limetoa wito kwa wananchi kuacha kusambaza taarifa zisizo na ukweli, na badala yake kuthibitisha taarifa wanazopokea kabla ya kuzieneza kwa wengine.
Jeshi hilo pia limesemalimeanza kushughulikia suala hilo kwa kufanya uchunguzi wa kubaini chanzo cha taarifa hizo na watu waliohusika katika kuzisambaza.
“Tumeanza uchunguzi kuhusu watu wanaojihusisha na kusambaza taarifa hizo, na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wahusika,” imeeleza taarifa hiyo.