Polisi, TRA warushiana mpira foleni ya malori Tunduma

Dar es Salaam/Songwe. Kukithiri kwa msongamano wa magari katika mpaka wa Tunduma kwa takribani wiki mbili sasa, imetajwa kuwa imesababishwa na ukosefu wa uadilifu kutoka kwa wasimamizi wa eneo hilo huku vitendo vya rushwa vikitajwa.

Baadhi ya madereva waliokwama katika mpaka huo, waliliambia Mwananchi kuwa kumekuwa na urasimu mwingi wa magari yanayotoka upande wa Tanzania kwenda Zambia baada ya kuanzishwa utaratibu wa kinyemela wa kuwatoza watu fedha ili wapite.

Saimon Mashana aliyesota mpakani hapo kwa siku sita sasa, alidai ili waruhusiwe wanatakiwa kutoa Sh30,000.

Naye Goodlack Materi, aliyekwama mpakani hapo kwa siku saba sasa licha ya kupata kibali cha kuvuka, lakini foleni imekuwa kikwazo na kibali alichopewa kimeshaisha.


Kauli ya Mkuu wa Mkoa

Akizungumza na Mwananchi kwa simu jana, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Dk Francis Michael alisema amekerwa kusikia rushwa inafanyika katika mpaka huo.

“Nataka kukomesha tabia hii. Nimepata taarifa za mawakala wanalazimisha kupewa rushwa, nimetoa maagizo kwa Jeshi la Polisi wawakamate wote waliokuwa wanawatoza madereva Sh30,000 na tujue walikuwa wanazipeleka wapi,”alisema.

Alisema kama wahusika ni Polisi na maofisa wa TRA, atahakikisha wanaondoka kwa kuwa watumishi wa aina hiyo wana nia ya kuchafua taswira ya mpaka huo huku akiwataka madereva watakaoombwa rushwa kuwapiga picha wote wanaomba hongo.

Dk Michael alitoa maagizo kwa jeshi la Polisi kuyalinda magari yalioyopo kwenye foleni kutokana na madereva kulalamika kuibiwa mizigo.

Naye Mwenyekiti wa chama cha wafanyakazi wa madereva (TADWU) Shubert Mbakizao alisema mpaka huo una matatizo makubwa manne likiwamo la kutokuwa na kiongozi mwenye sauti ya mwisho.


TRA wakana

Hata hivyo alipoulizwa Meneja wa TRA Mkoa wa Songwe, Dickson Kamara, alikana maofisa wake kujihusisha na rushwa kwa kuwa wanaohusika na kuongoza magari ni polisi.

Alisema kinachosababisha foleni ni upande wa Zambia kunakotengenezwa barabara.

Alisema changamoto hiyo imedumu kwa wiki mbili sasa hata hivyo juzi walizungumza na wenzao wa Zambia waone namna ya kutatua changamoto hiyo.

“Tumewaomba wasawazishe kwenye geti magari yaruhusiwe kupita, wamekubali tunatarajia hali ya kawaida itarejea,”alisema.


Polisi warusha mpira kwa TRA

Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Songwe (RTO), Joseph Bukombe alisema nategemeana na TRA wanavyofanya kazi mpakani hapo na si vinginevyo.

“Barabara yangu inatembea ukiona wamekaa kwenye Yadi ujue wanasubiri njia kule mpakani, mamlaka kati ya Tanzania na Zambia ziwaambie njia inafunguka ndiyo wapite.” alisema

“Hata juzi tulilazimika kwenda kumuona mkuu wa mkoa aje kujionea hali halisi, kwa siku nne mfulilizo, kontena zinalala barabarani na zingine zimejaa kwenye yadi.”

“Msimamizi wa TRA mpaka wa Tunduma ni mpole, kuna mazingira anatakiwa kutumia amri na kuelekeza, lakini yeye anaomba, sasa wavivu ukishaanza kuwaomba wanarudisha nyuma kasi ya utendaji,”alisema.

Sababu ya pili alitaja baadhi ya watumishi mpakani hapo si wazalendo wanataka kuona nchi inaingia hasara.

Alisema tatizo lingine Scana ya upande wa Tanzania kuna wakati huwa inashindwa kufanya kazi kutokana na mifumo yake.


Wananchi wazungumza

Wakazi wa Songwe wamedai msongamano huo umegeuka tishio la usalama wa afya zao na hata biashara hazifanyiki kama mwanzo kutokana na wageni kutofika kuepuka usumbufu.

Mfanyabiashara wa Tunduma, Joseph Haonga alisema biashara zimezorota kwa sababu hakuna wageni wapya kwa sababu ya msongamano.

Naye mkulima mwekezaji wa Kahawa, George Nzunda alisema hali hiyo imesababisha mnada wa Kahawa Mbozi kudorora baada ya wanunuzi wa Kahawa kutokwenda Songwe kushiriki.

"Mnada ulianzishwa kwa lengo la kuwapa nafasi wazalishaji wa Kahawa kushiriki lakini imekuwa vigumu, nashauri Serikali itoe ulinzi kwa wanunuzi wa kahawa wanaokuja Ili wasipoteze muda kusafiri" alisema Nzunda

Mariam Kabuye alisema; "hatujui hawa madereva wakibanwa haja kubwa wanaenda wapi, asubuhi tunakutana na makopo yenye mikojo yametupwa hovyo,” alisema Kabuje.

Naye Daud Kapungu alitaja maeneo korofi zaidi kuwa ni kutoka Mpemba kupitia Kastamu kwenda transifoma hayapitiki na hivyo abiria wanashushwa mbali.