Serikali yapata mwarobaini foleni ya malori Tunduma

Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Waziri Kindamba (wa sita kushoto) akikata utepe kuashiria Uzinduzi wa Mashine ya mdaki ya ukaguzi wa shehena za mizigo katika mpaka wa Tunduma Mkoa wa Songwe. Picha na Hawa Mathias.

Muktasari:

Ni kutokana na uzinduzi wa mashine ya mdaki (scan) yenye uwezo wa kukagua maroli ya shehena za mizigo 100 mpaka 150 ndani ya saa moja.

Songwe. Mkuu  wa  Mkoa  wa   Songwe,  Waziri   Kindamba   amesema kitendo cha Serikali kuwekeza Mradi wa Mdaki (Scan) ya ukaguzi wa shehena za mizigo kupitia mpaka wa Tanzania na nchi jirani ya Zambia utakuwa mwarobaini wa kuondokana na msongamano wa malori katika mpaka wa Tunduma.

Kindamba amesema leo Ijumaa Novemba 25, 2022 baada ya kuzindua mradi huo  uliogharimu Dora za Marekani bilioni 9 kwa ufadhili wa  Shirika la Trade Mark East Afrika ambao pia  utasaidia kudhibiti   shehena   za  mizigo iliyokuwa ikiingizwa nchini  kinyume  na  taratibu.


“Mradi huo umetekelezwa na Trade Mark East Afrika kupitia Idara ya Forodha kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambao una uwezo wa kukagua magari makubwa ya mizigo 100 mpaka 150 kwa saa moja,”amesema.


Amesema utakuwa chachu ya   kuongeza mapato  ya nchi na kudhibiti   uingizaji wa bidhaa  kama vipodozi, magendo visivyoruhusiwa kuingizwa nchini kisheria.

Kamishna  Mkuu  wa   Mamlaka  ya  Mapato  Tanzania   (TRA),  Alphayo  Kidata   amesema kupitia mradi huo  watahakikisha  wanatengeneza mahusiano mazuri ya kibiashara na    kulinda  mfumo  ambao una uwezo wa kufanya kazi kwa kipindi cha miaka 10 ijayo.

“Serikali kwa kushirikiana na TRA tunaendelea na kuboresha vituo vya pamoja vya forodha kwa kuboresha mifumo ya kaguzi ndogo na kubwa sambamba na kufunga vifaa maalum ili kuzuia uingizaji holela wa bidhaa zisizofuata utaratibu,” amesema.


Naye Mkurugenzi mkazi wa Trade Mark kupitia program ya Tanzania, Monica Hangi amesema kuwa mradi huo umetekelezwa kwa kipindi cha miaka sita mpaka kukamilika huku ukiwa umegharimu Dola bilioni 9 sawa na Sh20 bilioni za Tanzania.


“Tunandelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha na kufunga mifumo ya ukaguzi wa shehena za mizigo katika vituo vya forodha mipakani ili kukuza shughuli za mwingiliano wa kiuchumi katika mataifa ya Jumuiya ya nchi za SADC,”amesema.


Mwenyekiti wa  madereva nchini Zambia, Frayier Simbaya amesema wana kila sababu ya kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwani mradi huo utakuwa na tija kubwa ya kuongeza mapato ya nchi na  uvushaji wa shehena kwa wakati na kuondoka na na malalamiko ya madereva.


“Hili nimelibeba nawasilisha kwa viongozi wa nchini Zambia ili kuona ni namna gani wanaunga mkono kwa kuweka mradi huo ambao italeta mabadiliko makubwa ya kiuchumi katika sekta ya usafirishaji na kibiashara.