Polisi wa kike watahadharishwa kuhusu misuko yao

Muktasari:

  • Polisi wa kike Tanzania wametakiwa kuzingatia maadili ya uvaaji wa sare za jeshi hilo ikiwemo kusuka mitindo ya nywele itakayowezesha kofia kuvaliwa kwa usahihi.

  

Moshi. Polisi wa kike Tanzania wametakiwa kuzingatia maadili ya uvaaji wa sare za jeshi hilo ikiwemo kusuka mitindo ya nywele itakayowezesha kofia kuvaliwa kwa usahihi.

Hatua hiyo inafuatia uwepo wa baadhi ya askari wa kike kusuka mitindo ya nywele ambayo imekuwa ikisababisha uvaaji wa kofia za jeshi hilo, kikiuka taratibu.

Rai hiyo imetolewa na Kamishna wa polisi ushirikishwaji wa jamii, Dk Mussa Ali Mussa wakati akifunga mafunzo ya uongozi mdogo ngazi ya koplo namba 2/2021/2022, katika shule ya polisi Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Kamisha Mussa amesema baadhi ya misuko wanayosuka askari wa kike inaharibia sare za jeshi hilo na kuwataka wachague moja, kuwa polisi au kuwa wasukaji saluni.

"Niwakumbushe misuko ya nywele ya askari wa kike, najua hamlipendi kwa kuwa misuko iko ya aina nyingi na mingine inawafurahisha, lakini ningeomba mchague moja, katika ya mawili uwe polisi au uwe msukaji wa saluni.

"Maana misuko yenu inatuharibia sare, hazikai vizuri hasa kofia, kwa sababu baadhi ya misuko inasukwa halafu nyuma kuna ua linalolingana na mkia wa tausi.

“Sasa ukianza kuvaa kofia, haikai, utaiweka unavyotaka wewe hivyo inakuwa haijavaliwa kipolisi na badala yake, imefuata msuko wa nywele zako," amesema.

Amewataka pia kuwa na nidhamu na kuzingatia maadili ya jeshi hilo.


Jumla ya askari 4,260 wa cheo cha coplo, wamehitimu katika shule hiyo ya polisi Moshi na kutunukiwa vyeo.