Polisi wadaiwa kumuua muuza madini na kuchukua Sh70 milioni

Muktasari:

 Maofisa saba wa Jeshi la Polisi, wanashikiliwa na jeshi hilo mkoani Mtwara kwa tuhuma za kumpora mfanyabiashara mmoja wa madini Sh70 milioni na kisha kudaiwa kumuua kwa kumchoma kwa sindano ya sumu na kuutupa mwili wake baharini.

  

Dar/Mtwara. Maofisa saba wa Jeshi la Polisi, wanashikiliwa na jeshi hilo mkoani Mtwara kwa tuhuma za kumpora mfanyabiashara mmoja wa madini Sh70 milioni na kisha kudaiwa kumuua kwa kumchoma kwa sindano ya sumu na kuutupa mwili wake baharini.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, Mark Njera alisema jana kuwa tukio la mauaji lilitokea Januari 5 baada ya Hamis (Mussa) kufuatilia fedha zake zilizochukuliwa na maofisa wa polisi.

Alisema maofisa hao walikwenda kumpekua hapo lodge, zilipatikana Sh2.3 milioni, lakini katika mahojiano alieleza kuwa hizo fedha alikuwa akifanya kazi zake Dar es Salaam na marafiki zake walifanya tukio huko wakapata fedha hizo.

“Pia, alikiri kuwa na fedha wilayani Nachingwea; na maofisa niliowataja walikwenda kumpekua na walipata Dola 13,500 za Marekani (Sh33,748,980). Baadaye wakarudi Mtwara, wakamweka mahabusu kwa siku tatu kisha wakampa dhamana.

Hata hivyo, wakati polisi hao wakiwa mahabusu, mtuhumiwa mwenzao mwenye cheo cha mkaguzi wa msaidizi wa Polisi, Grayson Gaitan Mahembe anadaiwa kujinyonga Januari 22, 2022 akiwa mahabusu.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo Mwananchi ilizipata jana, maiti ya askari huyo tayari imeshasafirishwa kutoka Mtwara na kupelekwa nyumbani kwao Tabata Segerea jijini Dar es Salaam kwa maziko.

Wanaodaiwa kushikiliwa na polisi kwa mahojiano ni Kaimu Mkuu wa Upelelezi wa Polisi wa Wilaya (OC-CID) Mrakibu wa Polisi (SP) aliyetajwa kwa jina moja la Kalanje, Mkuu wa kituo (OCS) Charles Onyango, Nicholaus Kisinza wa kitengo cha intelijensia na wakaguzi wanne wa Polisi.

Danadana

Juhudi za Mwananchi kupata undani wa sakata hilo ziligonga mwamba baada ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Mark Njera kutokuwa tayari kulizungumzia.

Licha ya mwandishi kumfuata ofisini kwake, RPC huyo alisema hawezi kuzungumzia suala hilo hadi atakapoitisha mkutano na waandishi wa habari.

Hata hivyo, RPC Njera hakuwa tayari kueleza ni lini ataitisha mkutano huo wa waandishi wa habari

Naye Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Camillus Wambura alipoulizwa kwa simu alimtaka mwandishi kurudi kwa RPC Njera.

“Hii issue (suala) hata kama ingekuwa kubwa kwa vipi ni issue ya mkoa, msemaji wa mkoa ni Kamanda.

“Nadhani kama Kamanda atakuwa na press (mkutano na wanahabari) sijui kama atakuwa tayari kuongea na chombo kimoja kimoja, sidhani. Kwa hiyo endeleeni kucheki kama atakuwa na press itakuwa lini,” alisema DCI Wambura.

Vyanzo mbalimbali vya uhakika kutoka ndani ya Jeshi la Polisi, vinadai mauaji hayo yanadaiwa kufanyika katika hospitali ya Jeshi la Polisi Mtwara mjini Oktoba mwaka jana, lakini taarifa za mauaji hayo zikavuja kuanzia wiki iliyopita.


Mazingira ya tukio hilo yanafananishwa na mauaji ya wafanyabiashara watatu wa Mahenge mkoani Morogoro, Sabinus Chigumbi, Ephraim Chigumbi, Mathias Lunkombe na dereva taxi Juma Ndugu walioua kwa risasi Januari 14,2006.

Wafanyabiashara hao walikamatwa na Polisi eneo la Sinza Palestina jijini Dar es Salaam wakibambikiwa kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha, na kisha kupelekwa msitu wa Pande na kupigwa risasi.

Tayari Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Dar es Salaam ilishamhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa, aliyekuwa mkuu wa upelelezi wilaya ya Kinondoni, Christopher Bageni na jitihada za kujinasua na kitanzi zimekuwa zikigonga mwamba.


Taarifa za mauaji Mtwara

Taarifa zinadai kuwa Oktoba mwaka jana, mmoja wa watuhumiwa saba wanaoendelea kushikiliwa, alikwenda kwa Kaimu mkuu wa Upelelezi mkoa (RCO), na kumjulisha kuwa huko Nachingwea kuna mfanyabiashara ameuza madini.

“Huyo mkaguzi alimfuata bosi wake na kumweleza hayo kwamba huyo jamaa (marehemu) ana pesa nyingi inaonekana ameuza madini. Walitengeneza mazingira kwa kushirikiana na watuhumiwa wengine na kumkamata,” kilidai chanzo kimoja.

Chanzo hicho kimedai kuwa baada ya kumkamata, polisi walifanya upekuzi katika nyumba yake na kumkuta na Sh70 milioni na kumchukua pamoja na fedha hizo na kwenda naye Mtwara mjini ambako walimweka mahabusu kwa siku tatu.

“Baada ya siku tatu walimwachia bila masharti lakini wakawa wamebaki na zile pesa zake sasa alipotoka akakutana na ndugu yake, akamwelezea huyo ndugu yake akamwambia kama wamekuachia twende ukadai vitu vyako,” ilielezwa.

Inadaiwa kuwa alivyofika polisi, Mkuu wa kituo (OCS), Mkuu wa Upelelezi Wilaya (OC-CID), Kaimu RCO naMkuu wa Intelijesia (RCIO) wakamkamata tena na kumshikilia kwa mahojiano huku ndugu aliyemsindikiza akibaki nje.

“Huyo ndugu yake baada ya kuona jamaa hatoki alienda kumwangalia kule ndani polisi akakuta kama wanahojiwa hivi akarudi nje lakini baada ya muda alipata SMS (ujumbe mfupi) kutoka kwa ndugu yake akimjulisha kuwa ameachiwa.”

Hata hivyo, tangu siku hiyo mfanyabiashara huyo hakuonekana tena hivyo ndugu wakawa wanaendelea kufuatilia kwa kuwa mara ya mwisho alikuwa mikononi mwa polisi, hivyo wakawa wana shuku kuwa kuna jambo huenda limemtokea.

“Wanasema damu ya mtu ni nzito. Imekuwa siri tangu Oktoba lakini wiki iliyopita ndio kukaanza fununu kwamba polisi walimuua na ndipo uchunguzi ukaanza hadi kuwalenga hao maofisa wa Polisi,”kilieleza chanzo chetu.

Taarifa hizo zinadai kuwa mmoja wa maofisa wa polisi mwenye cheo cha mkaguzi wa Polisi ambaye naye ni mtuhumiwa, alipobanwa na makachero inadaiwa alifunguka kila kila, nani walioshiriki na mwili walipoutupa baharini.

“Ndio sasa ikagundulika kumbe siku ile hata ile SMS kwamba ameachiwa haikutumwa na marehemu bali mmoja wa watuhumiwa. Baadaye walimchukua hadi hospitali ya polisi huko ndio walimchoma sindano ya sumu”

Inaelezwa kuwa askari aliyejinyonga akiwa mahabusu, ndiye anatajwa kuwa alinyoosha maelezo ya tukio zima lilivyokuwa, nani wahusika na wapi mwili ulipotupwa, lakini amejinyonga baada ya kufanikisha uchunguzi huo.

Taarifa zilizopatikana jana kutoka Mtwara zilieleza kuwa tayari mabaki ya mwili wa mfanyabiashara huyo, yamepatikana na unafanyika uchunguzi wa vinasaba (DNA) ili kuthibitisha kama ni mwili wake ili upelelezi uende hatua ya pili.