Polisi wakamata wawili kwa kilimo cha bangi ekari 10 Sengerema
Jeshi la Polisi likiwa kwenye mashamba hayo Wilaya ya Sengerema, Mkoani Mwanza. Picha na Polisi
Muktasari:
- Ukamataji huo ni mwendelezo wa mikakati thabiti na endelevu ya Jeshi la Polisi katika kudhibiti na kutokomeza kilimo, mtandao wa usafirishaji na biashara haramu ya dawa za kulevya.
Mwanza. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limefanikiwa kuwakamata watu wawili kwa tuhuma za kujihusisha na kilimo cha bangi kwenye shamba lenye ekari 10 pamoja na kukutwa na shehena ya dawa hiyo ikiwa tayari imefungashwa kwa ajili ya kusafirishwa kwenda maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumzia mafanikio hayo jana Jumamosi Mei 23, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa amesema operesheni hiyo ni mwendelezo wa mikakati thabiti na endelevu ya Jeshi la Polisi katika kudhibiti na kutokomeza kilimo, mtandao wa usafirishaji na biashara haramu ya dawa za kulevya.
Kamanda Mutafungwa amesema Mei 23, 2026, Jeshi la Polisi lilipokea taarifa kutoka kwa wananchi wema zikieleza uwepo wa shamba hilo katika Kitongoji cha Nyerere, Kijiji cha Busekeseke, wilayani Sengerema.
Amesema baada ya kupokea taarifa hizo, askari polisi walifika eneo la tukio mara moja na kufanikiwa kumkamata mmiliki wa shamba hilo, aliyefahamika kwa jina la Mudumuka Kabika(60) anayefahamika kwa jina la Ziliona Tibakula, mkazi wa eneo hilo.
Amesema katika msako huo, polisi walifanikiwa kumtia mbaroni mtuhumiwa wa pili aliyefahamika kwa jina la Mawazo Manisha(50), mkulima na mkazi wa Kijiji cha Busekeseke. Mtuhumiwa huyo alikamatwa eneo la tukio akiwa na mafurushi ya bangi yaliyokuwa tayari kwa kusafirishwa.
Kamanda Mutafungwa amesema katika operesheni hiyo, askari walibaini uwepo wa magunia na vifurushi vingine vilivyoandaliwa kwa ajili ya kufungasha zao hilo haramu, huku sehemu kubwa ya shamba hilo ikiwa bado imesheheni mmea huo uliopigwa marufuku kisheria.
Hivi sasa watuhumiwa wote wawili wanashikiliwa na Jeshi la Polisi huku wakiendelea kuhojiwa.
Baada ya taratibu zote za kisheria kukamilika, watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.
Kamanda Mutafungwa ametoa onyo kali na rai kwa jamii kuacha mara moja kujihusisha na kilimo cha bangi badala yake wajikite katika kilimo cha mazao halali ya chakula na biashara yatakayowaletea maendeleo.
Aidha, amewataka viongozi wa Serikali za mitaa na wananchi kwa jumla kuendelea kutoa ushirikiano wa karibu kwa kufichua vitendo vya uhalifu katika maeneo yao.