Polisi walivyoimarisha ulinzi msikiti anakosali Sheikh Walid
Muktasari:
- Katika hali isiyo ya kawaida, Msikiti wa Kichangani, Magomeni Jiji I Dar es Salaam, umezingirwa na Askari wa Jeshi la Polisi.
Dar es Salaam. Katika hali isiyo ya kawaida, Msikiti wa Kichangani, Magomeni jijini Dar es Salaam, ulizingirwa na Jeshi la Polisi kuimarisha ulinzi, huku waumini wakifurika zaidi ya siku zote wakati wa Swala ya Ijumaa.
Hali hiyo ilijitokeza siku chache baada ya aliyekuwa Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Walid Omari Kawambwa, kusimamishwa uongozi na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata).
Taarifa zilizokuwa zikisambazwa katika mitandao ya kijamii zilidai kuwa Sheikh Walid angehudhuria Swala ya Ijumaa katika msikiti huo ambao amekuwa akiutumia kwa ibada na shughuli za kidini.
Ujumbe huo uliwavutia waumini wengi msikitini hapo, kiasi cha kusababisha wengine wakose nafasi ya kuswali ndani ya msikiti, hivyo wakaswali nje.
Sheikh Walid, alisimamishwa pamoja na masheikh wengine wawili wa mikoa ya Singida na Kigoma kwa tuhuma za mwenendo unaodaiwa kukiuka misingi ya uongozi wa Bakwata.
Askari wa Jeshi la Polisi nchini, wakiwa nje ya Msikiti wa Kichangani uliopo Magomeni leo Ijumaa Julai 17, 2026.
Tangu kutangazwa kwa uamuzi huo, kumekuwa na machapisho mengi katika mitandao ya kijamii yakionesha kumuunga mkono na kumtia moyo kiongozi huyo wa dini.
Waumini wafurika
Tofauti na Ijumaa nyingi za kawaida nje ya Mwezi wa Ramadhani, msikiti huo ulijaa waumini kiasi cha baadhi yao kushindwa kupata nafasi ndani ya jengo na kulazimika kuswali katika maeneo ya nje.
Wakati waumini wakisubiri ibada kuanza, kulisikika minong'ono kutoka kwa baadhi yao wakieleza matarajio ya kumwona Sheikh Walid akihutubia au kuzungumza jambo lolote kuhusu hatua zilizochukuliwa dhidi yake.
Hata hivyo, Swala ya Ijumaa iliyoanza saa 6:30 mchana iliendeshwa bila uwepo wa Sheikh Walid. Hakushiriki kuongoza ibada, hakuhubiri na hakuonekana kabisa katika eneo la msikiti huo.
Polisi walivyozingira
Nje ya msikiti, magari matatu ya Jeshi la Polisi yalionekana yakiwa yameegeshwa katika maeneo tofauti huku askari wenye silaha wakisambazwa kuzunguka eneo hilo.
Baadhi walikuwa karibu na mlango mkuu wa msikiti, wengine katika kona ya barabara inayoelekea katikati ya jiji, huku kundi jingine likiwa karibu na eneo la Magomeni Mikumi.
Askari wa Jeshi la Polisi nchini, wakiwa nje ya Msikiti wa Kichangani uliopo Magomeni leo Ijumaa Julai 17, 2026.
Baada ya ibada kumalizika saa 7:49 mchana, aliyesoma dua ya kuhitimisha alilitaja jina la Sheikh Walid na kumuombea busara, hekima na ulinzi katika kipindi anachopitia.
Walichosema waumini
Akizungumza na Mwananchi, mmoja wa waumini wa msikiti huo, Hassan Khalid, alisema idadi kubwa ya watu waliojitokeza haikuwa ya kawaida.
“Kwa kawaida umati wa namna hii huonekana zaidi katika Ijumaa za Ramadhani. Wengi wamekuja kuswali lakini pia walitaka kumwona Sheikh Walid baada ya yaliyotokea,” alisema.
Alisema Sheikh Walid amejijengea ukaribu mkubwa na waumini kutokana na namna anavyowasiliana na kushughulikia masuala yao.
Muumini mwingine, Zubeyda Maalim alisema kuwepo kwa askari wengi wa polisi kumezua maswali kwa waumini kwa kuwa hali hiyo haijawahi kushuhudiwa katika ibada za kawaida za Ijumaa.
“Hawa walijua Sheikh Walid anaungwa mkono na watu wengi. Sisi tunampenda kwa sababu ya uongozi wake na jinsi anavyoshirikiana na waumini,” alisema.
Hata baada ya ibada kumalizika, askari waliendelea kubaki katika maeneo ya nje ya msikiti kwa dakika 18, huku baadhi ya waumini wakisalia wakijadiliana kwa vikundi vidogo.
Sheikh Ponda aguswa
Akizungumzia kusimamishwa kwa Sheikh Walid, Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda alisema hatua hiyo ni sehemu ya taratibu za kiutawala, lakini ana mashaka kuhusu msingi wa baadhi ya tuhuma zilizotolewa dhidi ya viongozi hao.
“Wanaweza kusimamishwa kwa sababu mbalimbali za kiutawala, lakini kuhusu madai ya kukiuka misingi ya uongozi wa Bakwata, hapo nina mashaka. Kwa mtazamo wangu, maelezo hayo yanahitaji ufafanuzi zaidi,” alisema Sheikh Ponda.